Prime
WAJE TUONE: Wanasubiriwa kwa hamu Ligi Kuu England

Muktasari:
- Mastaa wengi wanahusishwa na mpango wa kutua kwenye Ligi Kuu England, lakini mashabiki wanawasubiri kwa hamu wakali hawa kuona ni kitu watakwenda kufanya kwenye mikikimikiki hiyo endapo kama watanaswa katika dirisha lijalo.
LONDON, ENGLAND: LIGI Kuu England inaelekea ukingoni, ikiwa imebakiza miezi michache kufika tamati na sasa mipango ya makocha imeshaanza kuelekezwa kwenye usajili wa mastaa wapya kwa ajili ya msimu ujao.
Mastaa wengi wanahusishwa na mpango wa kutua kwenye Ligi Kuu England, lakini mashabiki wanawasubiri kwa hamu wakali hawa kuona ni kitu watakwenda kufanya kwenye mikikimikiki hiyo endapo kama watanaswa katika dirisha lijalo.

Xavi Simons
Manchester United ilionyesha dhamira ya kutaka huduma ya Xavi Simons kwenye dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi la mwaka jana, lakini Mdachi huyo kwa wakati huo hakuwa na mpango wa kuhamia England, aliamua kujiunga na RB Leipzig akitokea Paris Saint-Germain. Lakini, mambo yamekuwa tofauti kwa sasa, ambapo fowadi huyo yupo tayari kuhama Red Bull Arena kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi. Man United bado inahitaji huduma yake, lakini Liverpool nao wanapiga hesabu za kumnasa mkali huyo, ambaye anaweza kupatikana kwa Pauni 67 milioni.

Angel Gomes
Kocha Thomas Tuchel alishangaza wengi baada ya kumtosa Angel Gomes kwenye kikosi chake cha England, lakini zao hilo kutoka kwenye akademia ya Man United kuna timu nyingi zinamtaka katika Ligi Kuu England, hivyo anaweza kurudi. Kiungo huyo mwenye kipaji kikubwa cha soka ataendelea kubaki Lille hadi mwisho wa msimu wake, licha ya kwamba kwa siku za hivi karibuni amekuwa hapati sana nafasi ya kucheza, kitu kitakachomfanya aondoke bure kabisa mwishoni mwa msimu. Gomes bado kuna kitu anataka akakifanye England na ndiyo maana West Ham na Tottenham zinamtaka.

Moise Kean
Straika Moise Kean kipindi chake alichokuwa Goodison Park hakikwenda vizuri wakati Everton ilipomnasa kwa Pauni 25 milioni kutokea Juventus, ambapo aliishia kufunga mabao mawili tu kwenye mechi 32 alizocheza kwenye Ligi Kuu England. Lakini, Kean anatarajia kurudi kwenye Ligi Kuu England kwa mara ya pili baada ya kuonekana kufanya vizuri huko Fiorentina, ambako amefunga mabao 20 katika mechi 34 alizocheza katika michuano yote msimu huu na alifunga mara mbili kwenye sare ya 3-3 iliyopata Italia dhidi ya Ujerumani, Jumapili iliyopita. West Ham na Arsenal zinamsaka.
Benjamin Sesko
Inavyoonekana ni kwamba straika Benjamin Sesko ameshajiweka tayari kwa ajili ya kwenda kujiunga na moja ya klabu za Ligi Kuu England katika dirisha lijalo la majira ya kiangazi huko Ulaya. Hata hivyo, kunasa saini ya mchezaji huyo itahitajika pesa ya kutosha kutokana na mkataba wake kwenye kikosi cha RB Leipzig kufika ukomo 2029. Ubora wake wa ndani ya uwanja, hasa kwenye kufunga mabao huku timu kibao za Ligi Kuu England zikiwa na uhitaji mkubwa wa washambuliaji, ambapo Arsenal, Chelsea, Tottenham, Man United na Liverpool zitapambana kumnasa Sesko.

Nico Williams
Kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana, Nico Williams alihusishwa sana na klabu ya Barcelona, anakocheza msh’kaji wake, Lamine Yamal. Lakini, miamba hiyo ya Nou Camp haikuwa na pesa za kutosha kumsajili winga huyo wa Kihispaniola baada ya kufanikiwa kumpata Dani Olmo. Barca inaweza kurudi kwa Williams kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi, licha ya kuwapo na timu kibao za England, ikiwamo Chelsea na Liverpool zinamtaka mkali huyo wa Athletic Bilbao. Kinachoelezwa ni kwamba huduma yake inaweza kupatikana kwa ada ya Pauni 50 milioni tu kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi.

Viktor Gyokeres
Straika Viktor Gyokeres yupo kwenye hatua za mwisho kabisa kuachana na Sporting CP mwishoni mwa msimu huu. Swali pekee linaloulizwa kuhusu mshambuliaji huyo kwa sasa, atakwenda wapi. Miamba ya soka ya Ufaransa, Paris Saint-Germain inaripotiwa kuhitaji saini yake, huku Bayern Munich nayo ikimtazama kama mchezaji sahihi wa kwenda kurithi buti za Harry Kane. Lakini, huko kwenye Ligi Kuu England, kuanzia kwa Man United, Arsenal, Chelsea na Liverpool zote zimekuwa zikihusishwa na mshambuliaji huyo, ambaye saini yake inaweza kugharimu Euro 70 milioni.

Martin Zubimendi
Kiungo Martin Zubimendi aligomea ofa ya kujiunga na Liverpool kwenye dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi mwaka jana baada ya kuamua kubaki zake kwenye kikosi cha Real Sociedad. Lakini, kwe-nye dirisha la Januari mwaka huu, kiungo huyo wa Kihispaniola aliripotiwa kukubaliana na ofa ya kwenda kujiunga na Arsenal mwishoni mwa msimu huu. Kutokana na hilo, mkali huyo wa San Sebastian kwa sasa anasubiriwa kwa hamu kuona ni kitu gani kilimfanya akatae kwenda Liverpool na kukubali kujiunga na Arsenal mwaka huu. Hilo ni dili linalosubiriwa kwa hamu.

Andrea Cambiaso
Mashabiki wa Juventus walikuwa na furaha kubwa baada ya dirisha la uhamisho wa majira ya baridi kufungwa na mchezaji wao kipenzi Andrea Cambiaso kuendelea kuwapo kwenye kikosi chao. Hata hivyo, presha nyingine inatarajiwa kuwafika kutokana na dirisha la majira ya kiangazi kubakiza miezi michache kabla ya kufunguliwa, huku staa wao huyo akiwa kwenye rada za Manchester City, ambayo haijawahi kuwa na masihara kwenye mipango yake ya usajili. Man City, inamtazama staa huyo mwenye umri wa miaka 24 Cambiaso kama chaguo lao sahihi katika kukirudisha kwenye makali yake kikosi hicho.

Victor Osimhen
Mara kadhaa kwa miaka ya hivi karibuni inapofika kipindi cha usajili wa majira ya kiangazi jina la straika Victor Osimhen limekuwa likihusishwa na klabu za Ligi Kuu England. Pengine ilishindikana huko nyuma, lakini mambo yanaweza kutiki kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi, ambapo straika huyo wa Kinigeria, anayecheza kwa mkopo Galatasaray, amefungua milango yake ya kwenda kukipiga Ligi Kuu England, ambako kuna timu kibao zinamtaka ikiwamo Chelsea, Man United na Arsenal. Napoli hawatasimama kumzuia fowadi huyo asitimkie England kwenye dirisha lijalo.

Dusan Vlahovic
Arsenal ilikaribia kumsajili straika Dusan Vlahovic kwenye dirisha la majira ya kiangazi la mwaka jana, kabla ya mkali huyo kuchagua kwenda kujiunga na Juventus. Lakini, sasa mambo yanavyokwenda fowadi huyo yupo tayari kuachana na miamba hiyo ya soka la Italia baada ya usajili wa mchezaji Randal Kolo Muani kutoka PSG, jambo lililomfanya Vlahovic kufanya siku zake kuhesabika katika kikosi hicho. Kwenye orodha ya washambuliaji wanaosakwa na timu za Ligi Kuu England, Vlahovic jina lake linahusishwa, ambapo kama si Arsenal basi Spurs itacheki namna ya kumsajili dirisha lijalo.

Jeremie Frimpong
Kutokana na Trent Alexander-Arnold kutimkia Real Madrid kwenye dirisha lijalo, Liverpool itahitaji mchezaji wa kuja kuziba pengo lake na kwenye hilo Jeremie Frimpong kura inaweza kuangukia kwake ili akakipige Anfield. Mdachi huyo amekuwa akicheza kwenye kiwango bora kabisa huko Bayer Leverkusen na kinachofurahisha ni kwamba Arne Slot, ambaye ni Mdachi pia, ndiye kocha wa Liverpool jambo linaloweza kufanya usajili huo kuwa mwepesi kukamilika. Kitu kingine kizuri ni kwamba Anfield kuna Wadachi kibao, akiwamo Cody Gakpo na Ryan Gravenberch.

Ademola Lookman
Mashabiki wa Ligi Kuu England wamekuwa wakimfuatilia Ademola Lookman kwa kile anachokifanya huko Italia na anapokwenda kuitumikia timu yake ya taifa ya Nigeria. Staa huyo aliwahi kucheza kwenye Ligi Kuu England, lakini aliondoka kipindi bado akiwa hajajipata tofauti na sasa, ambapo amekuwa kwenye kiwango bora sana na kuwa kivutio kwa mashabiki wengi wanaomtazama ndani ya uwanja, akiwatesa makipa kwa penalti zake za panenka. Kuna timu nyingine zinamtaka Lookman, ikiwamo Newcastle United na Man United zikifikiria kumnasa katika dirisha lijalo.

Jorell Hato
Arsenal inajutia uamuzi wa kushindwa kumnasa Jorrel Hato kwenye dirisha la uhamisho wa majira ya kiangazi mwaka jana. Beki huyo wa Ajax, thamani yake kwa sasa imekuwa kubwa kutokana na ubora wake ambao umemfanya apate nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha Uholanzi chini ya kocha Ronald Koeman. Arsenal inaamini itanasa saini yake kwenye dirisha lijalo la majira ya kiangazi, lakini beki huyo mwenye umri wa miaka 19, yupo kwenye rada ya Liverpool, ambao wanamtazama kama mtu sahihi wa kwenda kumchukua mikoba ya beki wa kushoto, Andy Robertson.

Rafael Leao
Rafael Leao ni moja ya wachezaji wanaocheza soka la kiwango bora duniani kwa sasa. Kitu kingine, Mreno huyo ana mashabiki wake kibao ambao wanashangilia timu za Ligi Kuu England na hilo linalowafanya wengi watamani kumwona winga huyo akienda kuwashika kwenye Ligi Kuu England. Msimu huu kwenye kikosi cha AC Milan amefunga mabao 10 na kuasisti mara tisa, kitu ambacho kinavutia timu nyingi za Ligi Kuu England wakihitaji saini yake. Chelsea ni kati ya timu zinamtaka winga huyo, lakini pia Man United, ambayo inanolewa na kocha Mreno.