Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

 Pacome aweka rekodi mpya Yanga ikipaa zaidi kileleni

Muktasari:

  • Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha pointi 64 ikicheza michezo 24 ikiiacha Simba nyuma na pointi zao 57 lakini Wekundu hao wakiwa na michezo miwili mkononi.

BAO la kichwa dakika ya 34 likifungwa na kiungo Pacome Zouzoua, limetosha kuipa Yanga ushindi wa 1-0 dhidi ya Coastal Union ikiendelea kujichimbia juu ya msimamo wa Ligi Kuu Bara huku kiungo huyo akiweka rekodi mpya.

Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha pointi 64 ikicheza michezo 24 ikiiacha Simba nyuma na pointi zao 57 lakini Wekundu hao wakiwa na michezo miwili mkononi.

Kwa kufunga bao hilo, inamfanya Pacome kufikisha mabao manane msimu huu moja zaidi ya aliyofunga msimu uliopita hivyo kuweka rekodi mpya akizidi kusogea juu akiwafuata washambuliaji wa timu yake Prince Dube na Clement Mzize wenye 11 kila mmoja. Pia ana asisti nane hivyo kuhusika kwenye mabao 16.

Kabla ya kuruhusu bao hilo, Coastal Union ilifanikiwa kuibana vizuri Yanga katika dakika 33 za kwanza ikifunga njia za mipira ya hatari ya wenyeji na kuwaweka kwenye wakati mgumu.

Licha ya juhudi hizo za Coastal Union ambayo ilicheza mechi hiyo bila ya uwepo wa kocha wake mkuu Juma Mwambusi ambaye inaelezwa ameondolewa, ikajikuta inaruhusu bao dakika ya 34 kwa kichwa cha Pacome akimalizia krosi nzuri ya kiungo mwenzake Maxi Nzengeli kilichogonga mwamba na kujaa wavuni.

Wakati timu hizo zinaelekea kumaliza kipindi cha kwanza, Yanga ikapata pigo dakika ya 45 baada ya kiungo wake Khalid Aucho kushindwa kuendelea na mchezo akiomba kutoka mwenyewe kufuatia kupata maumivu.

Aucho alikuwa anarejea kwenye mchezo huo akitoka kwenye majeraha baada ya kukosa mchezo uliopita dhidi ya Tabora United kutokana na kuumia alipokuwa timu ya Taifa lake ambapo nafasi yake ikachukuliwa na Mudathir Yahya.

Kipindi cha pili Yanga ilirudi na hesabu zake za kutaka kutanua ushindi wao ikiganda langoni kwa Coastal Union lakini ikakosa umakini wa kutumia nafasi zake.

Yanga kwa matokeo hayo imemalizana na Coastal Union msimu huu kwa kuchukua ushindi wa pili huku mechi zote zikimalizika kwa ushindi mwembamba wa bao 1-0.                            

Kipigo hicho kimeendelea kuifanya Coastal Union kubaki nafasi ya 13 kwenye msimamo ikiwa na pointi 25 baada ya kucheza mechi 25, ikibakiwa na michezo mitano kupambania nafasi ya kuepuka kushuka daraja kwani hivi sasa ipo kwenye mstari wa kucheza play-off.