Azam FC morali juu, Kocha atamba

Muktasari:
- Presha ndani ya Azam ilianza kupanda baada ya kikosi kushindwa kupata ushindi katika mechi tatu zilizopita, wakitoa sare dhidi ya Coastal Union (0-0), Simba (2-2), na Namungo (1-1).
USHINDI wa mabao 4-0 walioupata Azam dhidi ya Tanzania Prisons umeleta ahueni kubwa kwa kikosi cha matajiri hao wa Chamazi, baada ya kupitia kipindi kigumu cha kutoa sare tatu mfululizo katika Ligi.Matokeo hayo yamezidi kuwaweka katika mbio za kusaka nafasi mbili za juu.
Presha ndani ya Azam ilianza kupanda baada ya kikosi kushindwa kupata ushindi katika mechi tatu zilizopita, wakitoa sare dhidi ya Coastal Union (0-0), Simba (2-2), na Namungo (1-1).
Matokeo hayo yaliwafanya kushuka kwenye kasi yao ya ushindani, lakini ushindi dhidi ya Prisons umeibua tena matumaini mapya kwa mashabiki na wachezaji.
Kwa ushindi huo, Azam FC sasa wamefikisha pointi 48, wakijipanga kuendelea kupanda juu kwenye msimamo wa ligi. Kwa sasa wanashikilia nafasi ya tatu wakiwa mbele kwa pointi nne dhidi ya Singida BS inayoshika nafasi ya nne. Lengo lao kuu ni kumaliza ndani ya nafasi mbili za juu ili kupata tiketi ya kushiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.
Katika mchezo huo uliochezwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, mabao ya Azam yalifungwa na Nassoro Saadun, Pascal Msinodo (aliyefunga mawili) na Lusajo Mwaikenda.
Kocha wa Azam, Rachid Taoussi, hakuficha furaha yake baada ya mchezo huo, akisema timu yake ilionyesha kiwango bora ambacho kinatakiwa kuwa sehemu ya mwendelezo wao.
“Timu ilicheza kwa nidhamu kubwa, tulitengeneza nafasi nyingi na tulizitumia vizuri. Ushindi huu ni muhimu sana kwa morali ya wachezaji wetu na tunapaswa kuendelea na ari hii kwenye michezo inayofuata,” alisema Taoussi.
Kocha huyo kutoka Morocco alisisitiza kuwa bado wana nafasi kubwa ya kumaliza msimu ndani ya nafasi mbili za juu iwapo wataendelea kucheza kwa kiwango bora kama walivyoonyesha dhidi ya Tanzania Prisons.
“Tunajua ushindani ni mkubwa, lakini tuna kikosi bora ambacho kinaweza kupambana hadi mwisho wa msimu. Tunahitaji ushindi mfululizo ili kufanikisha malengo yetu,” aliongeza.
Kocha wa Prisons, Amani Josiah alikiri kuwa walikumbana na changamoto kubwa katika mchezo huo, huku akisema makosa ya kikosi chake yaliwagharimu.
“Azam walikuwa bora zaidi, walitumia makosa yetu na wakapata mabao. Tunahitaji kurekebisha makosa yetu kabla ya mechi inayofuata,” alisema kocha huyo.
Ushindi huu umeifanya Azam kuendelea kuwa bado na nafasi kwenye mbio za kuwania ubingwa wa ligi. Ingawa wanahitaji juhudi zaidi kuwapiku vinara wa ligi, Simba na Yanga ambao leo watakutana kwa Mkapa.