Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Pamba Jiji yapata ajali, wachezaji wapo salama

Muktasari:

  • Hii ni ajali ya tatu kwa timu za Ligi Kuu Bara msimu huu, baada ya awali JKT Tanzania kupata ajali Oktoba mwaka jana na kusababisha mechi dhidi ya Simba kuahirishwa, kama ilivyokuwa kwa Dodoma Jiji iliyopata ajali ikitokea mkoani Lindi katika mechi dhidi ya Namungo na hivyo, mchezo dhidi ya Simba kusogezwa mbele hadi Ijumaa hii, Machi 14.

MSAFARA wa Pamba Jiji uliokuwa unatoka Dodoma kwenda Morogoro kwa ajili ya mchezo wa hatua ya 32 Bora wa Kombe la Shirikisho la CRDB (FA) dhidi ya Kiluvya United, umepata ajali alfajiri ya jana na mchezaji Mwaita Ngereza ndiye aliyejeruhiwa kwa kupata michubuko huku wengine wakiwa salama.

Hii ni ajali ya tatu kwa timu za Ligi Kuu Bara msimu huu, baada ya awali JKT Tanzania kupata ajali Oktoba mwaka jana na kusababisha mechi dhidi ya Simba kuahirishwa, kama ilivyokuwa kwa Dodoma Jiji iliyopata ajali ikitokea mkoani Lindi katika mechi dhidi ya Namungo na hivyo, mchezo dhidi ya Simba kusogezwa mbele hadi Ijumaa hii, Machi 14.

Daktari wa Pamba Jiji, Joseph Chacha aliliambia Mwanaspoti,  wachezaji wako sawa kiafya baada ya ajali hiyo iliyotokea jana mkoani Dodoma na kikosi hicho kimeendelea na safari yao ya kwenda Morogoro.

Basi la Pamba Jiji lililokuwa limewabeba wachezaji na benchi la ufundi likiwa linatokea mjini Bukoba, Mkoa wa Kagera liligongwa kwa nyuma na Semi Truck saa 11 alfajiri wilayani Bahi, Dodoma na kusababisha mshtuko kwa wachezaji.

Pamba Jiji ilikuwa safarini baada ya kumaliza mchezo wake wa Ligi Kuu Bara dhidi ya wenyeji wao Kagera Sugar, uliomalizika kwa kufungwa mabao 2-1.

Akizungumzia hali za wachezaji hao, Dk Chacha alisema wamepata mshtuko wa kawaida isipokuwa mchezaji, Mwaita Gereza aliyekuwa amekaa eneo ambalo gari liligongwa na lori hilo, hivyo vioo vilivyopasuka kumsababishia mikwaruzo.

Dk Chacha alisema mchezaji huyo alipelekwa Hospitali ya Wilaya ya Bahi kwa uchunguzi zaidi na ameruhusiwa na msafara wa kikosi hicho umeendelea na safari.

“Imetokea tu kama ajali zingine zinavyotokea gari imepata shida na wachezaji wetu wamepata tu mshtuko wa kawaida ingawa mchezaji mmoja (Mwaita Ngereza) alipata mikwaruzo kidogo na maumivu ya kawaida kwa sababu ya mshtuko wa ajali lakini amepata huduma kwa kufanyiwa ‘check up’ (uchunguzi) na yuko vizuri na timu imeendelea na  safari kama kawaida,” alisema Dk Chacha na kuongeza;

“Wachezaji walipata mshtuko wa kawaida tu hatukuwa na sababu ya kuwacheki wote isipokuwa tu yule aliyekuwa amekaa kule nyuma ambako gari imegongwa ndiye amepata shida kidogo kwa sababu ya vile vioo vilivyopasuka vilimsababishia mikwaruzo.”

Daktari huyo alisisitiza licha ya kujiridhisha kwa sasa wachezaji hao wako sawa lakini wataendelea na uangalizi wa karibu kwa saa 24 hadi 72 ili kujiridhisha zaidi.