Beki KMC ajiandaa kutua Al Hilal

Muktasari:
- Ipo hivi. Beki huyo ambaye aliibuka mchezaji bora msimu uliopita 2023/24 yupo katika hatua za mwisho kumalizana na Al Hilal ya Sudan.
BEKI wa KMC, Raheem Shomary akiwa katika harakati za kuipambania timu hiyo ishishuke daraja ikiwa imebakiza mechi nne mkononi huenda akawa sehemu ya kikosi kitakachoshiriki Ligi ya Mabingwa Afrika msimu ujao.
Ipo hivi. Beki huyo ambaye aliibuka mchezaji bora msimu uliopita 2023/24 yupo katika hatua za mwisho kumalizana na Al Hilal ya Sudan.
Chanzo cha kuaminika kutoka kwa rafiki wa karibu wa mchezaji huyo kililiambia Mwanaspoti kuwa mazungumzo ya pande mbili kati ya mchezaji na uongozi wa Al Hilal yanakwenda vizuri na muda wowote beki huyo anaweza kusaini mkataba.
“Raheem anamaliza mkataba mwisho wa msimu huu na uongozi wa timu hiyo umeanza mazungumzo ya kutaka kumbakiza lakini sioni nafasi ya yeye kubaki kwani mpango wake ni kwenda kujaribu maisha mengine nje ya Tanzania,” alisema mtoa taarifa huyo na kuongeza;
“Pia fedha aliyowekewa mezani inamvuta zaidi kuondoka KMC, nina uhakika hadi mwezi ujao Raheem atakuwa amemalizana na timu hiyo mpya kwani mazungumzo na makubaliano yamekamilika.”
Mwanaspoti lilimtafuta Raheem ili azungumzie dili hilo ambapo alisema bado ni mchezaji wa KMC na kama kuna mazungumzo yoyote basi atafutwe meneja wake ndiye atakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuzungumzia hilo kwani yeye kazi yake ni kucheza.
“Siwezi kuzungumza lolote juu ya taarifa hizo lakini nafikiri mtu sahihi wa kufanya hivyo ni meneja wangu, mimi kazi yangu ni kucheza na bado nina mkataba na timu yangu hadi mwisho wa msimu,” alisema Raheem.
Hakuna kiongozi yeyote wa juu wa KMC aliyepatikana kuthibitisha taarifa hizo, lakini chanzo cha ndani kinasema mabosi nao wanajaribu kupambana kumbakisha ingawa, menejimenti ya mchezaji imeamua beki huyo aendee akatafute maisha Al Hilal kama mchezaji huyo.