Waliofukuzwa Junguni kwa tuhuma za kubeti, wageuza kibao

Muktasari:
- Wachezaji saba wa kikosi cha Junguni United waliosimamishwa na kufukuzwa katika kikosi hicho kwa tuhuma za kubeti, kupitia wanasheria wao wametoa siku 14 kwa klabu ya Junguni kutoa ushahidi juu ya tuhuma hizo na wakishindwa iwalipe wachezaji hao fidia ya Sh300 milioni kwa kuwachafua.
Saa chache tangu uongozi wa timu ya Junguni United iliyopo Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) kutangaza kuwafukuza wachezaji saba kwa tuhuma za kujihusisha kubeti, wachezaji wameugeuzia kibao klabu hiyo wakitoa siku 14 kuombwa radhi na kulipwa fidia ya Sh300 milioni.
Wachezaji hao wametoa msimamo huo kupitia taarifa ilitolewa na mawakili wanaowasimamia.
Pia, taarifa hiyo imesema wateja hao wametoa siku 14 kwa utekelezaji wa barua hiyo na ikiwa watashindwa kukubali madai hayo watachukua hatua za kisheria.
Taarifa hiyo imetolewa leo Ijumaa Aprili 25,2025 na Mwanaspoti kuwa na nakala imesema ikieleza imetokana na maagizo ya wachezaji hao ambao ni wateja wa kampuni hiyo ya uwakili.
Taarifa hiyo imesema kuwa, wateja hao wameachishwa kazi bila kufuata taratibu ikiwemo kupewa haki ya kusikilizwa na kupewa adhabu ya kufukuzwa kazi bila ushahidi wa madai hayo ya kubeti kama ilivyooneshwa katika barua ya uongozi wa Junguni.
"Umeandika barua ya kuwaachisha wateja wetu bila kufuata taratibu, uliposti katika mitandao ya kijamii, hivyo kuwachafua na kuonekana kuwa ni vijana wa hovyo wanaojishughulisha na kubeti wakati sio sahihi na hakuna ushahidi," imesema taarifa hiyo.
Taarifa hiyo imeongeza kuwa, wateja hao hawajahi kuitwa wala kupewa nafasi ya kujitetea au kuonesha ushahidi namna ambavyo wameshiriki katika tuhuma zao.
"Wateja wetu wamesikitioa kwa kuwa taratibu na kanuni za miongozo, ipo wazi kuwa kila mtu ana haki ya kusikilizwa, na barua hizo zimetumwa katika mitandao bila kuwatumia wahusika," imesema taarifa hiyo.
Barua hiyo imeitaka timu hiyo kuomba radhi kwa vyombo vya habari vinavyotambulika kama ilivyofanya awali.
Wachezaji saba ambao wamesimamishwa na kufukuzwa Junguni ni; Salum Athumani Chubi, Ramadhan Ally Omar, Abdallah Sebastian, Danford Moes Kaswa, Bakari Athumani Jomba( Jomba Jomba), Rashid Abdalla Njete na Iddi Said Karongo.