Brandts ataka Yanga iweke kambi Hispania

Kocha wa Yanga, Ernest Brandts.PICHA|MAKTABA
Muktasari:
- Hata hivyo Brandts amesisitiza kuwa angependa timu yake iweke kambi nchi za Ulaya na hasa Hispania au Uturuki katika kujiandaa na Ligi ya Mabingwa Afrika.
KOCHA wa Yanga, Ernest Brandts, amefurahia usajili wa wachezaji wawili walionaswa hivi karibuni, lakini akasema: “Hapa bado straika mmoja tu mkali, ili tufanye vizuri Afrika.”
Hata hivyo Brandts amesisitiza kuwa angependa timu yake iweke kambi nchi za Ulaya na hasa Hispania au Uturuki katika kujiandaa na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Brandts anaongoza mazoezi ya wachezaji wasiozidi 15 yaliyoanza Jumatatu iliyopita huku wasiokuwapo ni wale walio katika timu zao za taifa zinazoshiriki Kombe la Chalenji au wengine walio majeruhi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Brandts, alisema amefurahi kukuta Kamati ya Usajili imesajili wachezaji wawili mahiri ambao ni Juma Kaseja na kiungo, Hassan Dilunga, akisema anawafahamu wachezaji hao kuwa wana uwezo mkubwa wa kuimarisha nguvu kikosini.
“Namjua Kaseja na Dilunga, ni wachezaji wazuri wanaoweza kuichezea Yanga na timu ikapata mafanikio nafurahi kuwa nao,” alisema Brandts.
“Kazi iliyobaki ni kumpata mshambuliaji mmoja atakayeongeza nguvu kikosini.”
Brandts alisema anatarajia viongozi watafanya kazi vizuri kuhakikisha wanasajili straika atakayeisaidia Yanga katika Ligi ya Mabingwa Afrika na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.
Alipoulizwa kama anaweza kumsajili straika wa zamani wa Simba, Emmanuel Okwi, Brandts alisema: “Yanga inapenda kuwa na mchezaji mzuri kama Okwi, lakini tayari kuna mambo niliyozungumza na viongozi wangu kuhusu mchezaji ninayemtaka.”
Hata hivyo Brandts ameendelea kukomalia timu hiyo iweke kambi nchini Hispania au Uturuki mwezi ujao huku pia akitaka mechi nyingi za kirafiki.
Brandts ambaye amesema ameridhika na makubaliano ya mkataba wake mpya na Yanga ingawa hadi jana Jumatano asubuhi alikuwa bado hajausaini, aliiambia Mwanaspoti akisema: “Tuko kwenye maandalizi kwa ajili ya mashindano yote yanayotukabili na hasa Ligi ya Mabingwa Afrika na mzunguko wa pili wa Ligi Kuu.
“Ili tuwe vizuri zaidi, maandalizi yetu napenda yafanyike katika nchi za Uturuki au Uhispania kwa sababu ni tulivu, kuna kila kitu lakini pia itaongeza morali kwa wachezaji.”
Brandts alienda mbali na kusema, wiki hii atafanya mazungumzo na wenzake wa benchi la ufundi pamoja na uongozi kupanga mechi za kirafiki, lakini nyingi ziwe za kimataifa ili kuijenga timu yake.
Yanga imekuwa na tabia ya kuweka kambi Ulaya ambapo Desemba mwaka jana ilijichimbia Uturuki kwa wiki mbili na iliporudi ikachukua ubingwa wa Bara.
Timu hiyo inaendelea na mazoezi kwenye Uwanja wa Bora, Kijitonyama, jijini Dar es Salaam tangu Jumatatu. Wachezaji ambao wamekuwa wakihudhuria mazoezi hayo ni nahodha Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Nizar Khalfan, Oscar Joshua, Reliants Lusajo, Said Bahanuzi, Hussein Javu, Jerry Tegete, Ibrahim Job, Rajab Zahir, Abdallah Mguhi, Simon Msuva, Hamis Thabit na Bakari Masoud.
Majeruhi ni David Luhende aliyekuwa akisumbuliwa na nyama za paja, Juma Kaseja anayeumwa kifundo cha mguu, Salum Telela anayesumbuliwa na goti pamoja na chipukizi Yusuph Abdul anayeumwa bega la kulia.