Brandts awatupa jukwaani Cannavaro, Barthez

Nadir Haroub ‘Cannavaro’ akizungumza na Kocha wa Yanga, Ernest Brandts wakati wa mazoezi
Muktasari:
Kama hiyo haitoshi, Kocha wa Yanga, Ernest Brandts ambaye timu yake imefikisha pointi 19, alionyesha jeuri ya aina yake baada ya kuwapiga kwenye benchi wachezaji mahiri Didier Kavumbagu, Athuman Idd Chuji na Jerry Tegete.
YANGA iliipiga Rhino ya Tabora mabao 3-0 kwenye Uwanja wa Taifa jana Jumatano lakini beki Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na kipa Ally Mustapha ‘Barthez’ wanaosengenywa na mashabiki wameingia mitini na hawakukanyaga uwanjani.
Kama hiyo haitoshi, Kocha wa Yanga, Ernest Brandts ambaye timu yake imefikisha pointi 19, alionyesha jeuri ya aina yake baada ya kuwapiga kwenye benchi wachezaji mahiri Didier Kavumbagu, Athuman Idd Chuji na Jerry Tegete.
Cannavaro, Barthez wamekuwa wakilaumiwa na mashabiki wa Yanga kwamba ndiyo chanzo cha sare ya mabao 3-3 na Simba wikiendi iliyopita ingawa benchi la ufundi pamoja na wataalamu wa soka wamekuwa wakiwatetea na kudai kwamba lawama hizo ni za timu nzima.
Katika mechi hiyo ya watani wa jadi, Yanga ilipata mabao matatu kipindi cha kwanza lakini kipindi cha pili Simba ikajipanga na kurudisha yote na kuacha Yanga wakianguka kilio na kukosa mamilioni waliyokuwa wameahidiwa na uongozi na wanachama matajiri wa klabu hiyo.
Barthez na Cannavaro inadaiwa kwamba waliomba udhuru kwa madai kwamba hawako vizuri kisaikolojia ingawa, nafasi zao zilizibwa na Deo Munishi na Mbuyu Twite. Mchezaji mwingine aliyekuwa benchi ni Ahmed Kikumbo, Renatus Lusajo ingawa Nizar Khalfan na Oscar Joshua walikuwa benchi lakini baadaye walipewa shavu na kuingia.
Brandts alisema alifanya mabadiliko hayo ili kujaribu wachezaji wengi na kujua ufanisi wao.