Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

BRAZIL 2014: JEMBE: Medel awakabili Brazil na kifaa maalumu mguuni

Muktasari:

  • Hatimaye ilipofika juzi Jumamosi, Medel alicheza mechi hiyo ya hatua ya 16 bora kwenye Kombe la Dunia, huku akiwa amebandikwa bandeji maalumu kwenye paja lake la kushoto ili kuzuia maumivu hayo ya misuli.

BELO HORIZONTE, BRAZIL

KWA mujibu wa Kocha wa Chile, Jorge Sampaoli, kama timu yake ingepangwa kucheza na Brazil Ijumaa, basi Gary Medel asingecheza mechi hiyo.

Beki huyo wa nguvu aliumia misuli ya paja Alhamisi iliyopita, lakini akamwambia kocha wake na timu ya madaktari kuhakikisha anacheza mechi hiyo kwa namna yoyote ile.

Hatimaye ilipofika juzi Jumamosi, Medel alicheza mechi hiyo ya hatua ya 16 bora kwenye Kombe la Dunia, huku akiwa amebandikwa bandeji maalumu kwenye paja lake la kushoto ili kuzuia maumivu hayo ya misuli.

Akiwa na kifaa hicho kwenye paja lake, Medel bado aliendelea kuwa beki matata sana kwenye safu ya ulinzi ya timu ya Chile na kuwaweka washambuliaji wa Brazil kwenye wakati mgumu katika kuipenya ngome hiyo. Katika mchezo huo uliofanyika kwenye Uwanja wa Mineirao, Medel alikimbia kilometa 10 uwanjani.

Mchezaji huyo ambaye asili yake ni kiungo, lakini baadaye amerudishwa kuwa beki. Kwenye mchezo huo wa juzi Jumamosi alikimbia kilometa 10 kwa dakika 109 alizokuwa ndani ya uwanja.

Pamoja na kifaa hicho kilichofungwa kwenye paja lake la kushoto, Medel alionyesha kiwango cha maana licha ya kwamba hakuchezeshwa kwenye nafasi yake anayoweza kuimudu vyema.

Hakujali kama ana majeraha kwenye mguu wake na alikuwa akizuia kila mashuti na kuwakaba kwa nguvu zote washambuliaji hatari wa Brazil, Neymar, Oscar na Hulk.

Ngoma yawa nzito dakika ya 90

Baada ya purukushani nyingi dhidi ya wachezaji wa Brazil, Medel akikumbana pia na kiwiko cha mshambuliaji Jo na mambo yalikuwa magumu kwenye dakika 90 baada kuonekana kuzidiwa na maumivu kwenye mguu.

Alianguka akiwa katikati ya uwanja na hivyo kupatiwa matibabu ili aendelee kucheza kwenye muda wa nyongeza. Wakati Kocha Sampaoli akiwa anawahamasisha wachezaji wa Chile kupambana kwenye dakika hizo 30 za nyongeza, Medel alikuwa akipatiwa matibabu ili acheze dakika hizo ndipo hapo zilipoonekana bandeji maalumu zilizokuwa zimefungwa kwenye mguu wake wa kushoto.

Hata hivyo, ujasiri wake wa kupambana ulikomea kwenye dakika 109 baada ya kushindwa kuendelea. Alitolewa uwanjani kwa machela, huku machozi yakimlengalenga.

Alia kama mtoto, Jara alipokosa penalti

Wakati Gonzalo Jara alipokosa mkwaju wa tano wa penalti kwa upande wa Chile, Medel aliangua kilio kama mtoto na kwamba haikuwa rahisi kumnyamazisha. Aligalagala kwenye nyasi za Uwanja wa Estadio Mineirao. Alishindwa kuyazuia machozi yake.

Kipa wa akiba wa Chile, Johnny Herrera, alikuwa wa kwanza kujaribu kumnyamazisha Medel, aliyekuwa akilia kwa uchungu kabla ya wachezaji wengine kumfuata na kumpoza machungu na kuwataka kwa pamoja wawapongeze mashabiki wao ambao muda wote walikuwa wakiwashangilia.  Chile ilitupwa nje kwa penalti 3-2.