Chama la Yusuph Athuman lina historia

Muktasari:
- Chama la nyota huyo wa zamani wa Yanga halina muda mrefu kwenye ligi hiyo likianzishwa mwaka 2007 wakati huo ikiitwa Air Bagan.
WIKI iliyopita Mtanzania, Yusuph Athuman alitambulishwa kwenye kikosi cha timu ya Yangon United inayoshiriki Ligi Kuu Asia.
Chama la nyota huyo wa zamani wa Yanga halina muda mrefu kwenye ligi hiyo likianzishwa mwaka 2007 wakati huo ikiitwa Air Bagan.
Miaka miwili baadaye timu hiyo ikabadilishwa jina kutoka Air Bagan na kuitwa Yangon United baada ya kuchukua ubingwa wa Ligi Daraja la Kwanza na kushiriki Ligi Kuu.
Mafanikio makubwa ya klabu hiyo ni kubeba ubingwa wa Ligi Kuu maarufu Myanmar National League mara tano, 2011, 2012, 2013, 2015 na 2018.
Mbali na ubingwa ilimaliza nafasi ya pili mara sita, 2014, 2016,2017, 2022, 2023 na 2024/25.
Athuman anakuwa Mtanzania wa kwanza kuichezea klabu hiyo akijiunga akitokea Tanzania Prisons aliyokuwa anaitumikia kwa mkopo akitokea Fountain Gate ambao hakuwahi kuichezea mchezo hata mmoja.
"Najivunia kuwa sehemu ya timu ya Yangon United, ni moja ya timu zenye mafanikio katika ligi ya Myanmar ikiwa nafasi ya pili kwenye msimamo, nitajitoa kwa uwezo wangu wote kuhakikisha timu hii inatwaa ubingwa," alisema.
Yangon United ipo nafasi ya pili ikikusanya pointi 51 kwenye mechi 22 ilizocheza ikishinda 15, sare sita na kupoteza mchezo mmoja ipo nyuma kwa pointi 11 dhidi ya vinara wa msimamo Shan United wenye pointi 62.
Mbali na chama hilo kuwa nafasi nzuri kwenye msimamo lakini mshambuliaji wao tegemeo, Yan Kyaw Htwe anaongoza kwa ufungaji akiweka mabao 15.