Prime
Clatous Chama avunja ukimya, agusia kiwango chake
KIUNGO mshambuliaji wa Simba, Clatous Chama, ameendelea kuonyesha kiwango bora msimu huu wa 2025-2026 baada ya kuibuka mchezaji bora wa mechi mara nne mfululizo, akiongeza matumaini ya Wekundu hao wa Msimbazi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara.
Chama anaamini Simba bado ina nafasi kubwa ya kupindua mbio za ubingwa, hasa baada ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Mashujaa kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mkoani Kigoma, juzi Alhamisi, uliowasaidia kupunguza tofauti ya pointi kati yao na Yanga zilizobaki mbili.
Kwa sasa Simba ambayo ipo nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 52 imezidiwa na Yanga yenye 54, huku zikisalia mechi saba kabla ya msimu kumalizika.
Katika mchezo huo, Chama alifunga mabao mawili, hali iliyomfanya kuwa mmoja wa wachezaji muhimu zaidi kwa Simba katika kipindi hiki cha msimu akihusika na mabao 12, akifunga manane na asisti nne.
Akizungumza na Mwanaspoti, kiungo huyo amesema: “Ninaamini bado tuna nafasi ya kutwaa ubingwa, niliamini hivyo tangu wakati ambao tulikuwa nyuma kwa pointi tano, tupo kwenye mwelekeo mzuri na ukitazama utofauti wa pointi ni mdogo sana kwa sasa hivyo tunatakiwa kuendelea kupambana.
"Nadhani inaonekana wazi kiwango cha timu namna ambavyo kimekuwa kikikua na naamini tunaweza kuendelea kufanya makubwa kwa sababu hii timu asilimia kubwa inaundwa na vijana, sisi wazoefu tupo hapa kwa ajili ya kutoa uzoefu wetu."
Takwimu zinaonyesha kuwa Chama amekuwa katika kiwango bora katika mechi nne zilizopita, akiwa amehusika katika mabao saba kati ya 10 ya Simba, akifunga matano na kutoa pasi mbili za mabao.
Kwa ujumla, kiungo huyo sasa ana mabao manane na pasi nne za mabao msimu huu, akionekana kuwa mchezaji muhimu katika mfumo wa ushambuliaji wa Simba inayonolewa na Steve Barker.
Miongoni mwa mechi alizong’ara ni dhidi ya Yanga ambapo alifunga na kutoa asisti katika sare ya 2-2, pamoja na mchezo dhidi ya JKT Tanzania ambapo alifunga bao moja lililoipa Simba ushindi wa 1-0.
Mei 10, 2026 dhidi ya Tanzania Prisons, Chama pia alifunga na kutoa asisti moja katika ushindi wa 4-0, kabla ya kuendeleza makali yake kwa kufunga mabao mawili katika mchezo wa juzi.
Kiwango hicho kimemfanya Chama kuwa miongoni mwa wachezaji hatari zaidi kwa sasa Ligi Kuu Bara huku akila sahani moja na Allan Okello wa Yanga mwenye mabao saba na asisti saba, Mossi Nduwumwe wa Singida Black Stars mwenye mabao manane pamoja na Feisal Salum 'Fei Toto' wa Azam mwenye mabao 11 na asisti saba.