Prime
Moto wa Clatous Chama Simba waibua jambo
UNAFUATILIA kiwango cha kiungo wa Simba, Clatous Chama? Ni kama amezaliwa upya kwani amerudisha kiwango chake akifanya makubwa tangu arejee kwenye kikosi cha Wekundu hao akitumia miezi mitano tu kuuwasha moto wake.
Chama amekuwa wa moto kwa sasa ndani ya Simba akionyesha mabadiliko makubwa kwenye kiwango chake akiwa tishio katika kutengeneza ushindi wa Wekundu hao kwenye mechi mbalimbali za mashindano tofauti.
Ukiangalia Chama aliyekuwa Yanga na hata yule aliyekuwa Singida Black Stars, ni kama watu wawili tofauti na huko nyuma alionyesha kukosa uhuru wa kufanya mambo makubwa uwanjani na muda mwingine kukosa muda wa kucheza kabisa, lakini Simba imekuwa tofauti kwa kumpa anachokitaka.
Chama wa Simba amekuwa akipewa majukumu akicheza kama kiungo huru, akifanya ubunifu wake hatua ambayo wakati wote ilikuwa inamfanya kuwa bora zaidi na hatari akiwa kiwanjani, Yanga ilikuwa ngumu kutokana na msimu uliopita ufalme huo alikuwa nao Stephanie Aziz KI ambaye naye alifanya makubwa wakati huo.
Alipoondoka Aziz KI, ufalme huo hakupewa Chama, ukamuangukia Pacome Zouzoua na kumfanya kuwa chaguo la pili akisotea benchi kwenye mechi nyingi, haikuwa shida kumuona Mzambia huyo akionyesha ni kama hana furaha ndani ya kikosi hicho.
Simba ilimrudisha Chama na kama haitoshi kocha Steve Barker inawezekana aliwasikiliza vizuri wasaidizi wake kama Seleman Matola ambaye aliwahi kufanya kazi na kiungo huyo kabla, huku akirudishiwa ufalme huo ambao sasa unalipa ndani ya timu hiyo.
Ukitazama vizuri kwa sasa Chama kuna maeneo mfumo wa Barker umempa wepesi zaidi akishiriki mpaka kukaba, angalia namna alivyotengeneza bao la kwanza kwenye mchezo dhidi ya Yanga kwenye ile sare ya mabao 2-2, alipeleka presha kwa beki wa upinzani Israel Mwenda na kuunasa mpira.
Msimu mmoja ambao Chama alifanya kazi Yanga alifanikiwa kuifungia timu hiyo mabao sita lakini mpaka sasa tangu arejee Simba ameshafikia idadi hiyo ya mabao, akionyesha kwamba anaweza kufunga zaidi katika mechi zilizosalia.
Wakati Chama anatua Simba akitokea Singida Black Stars kipindi cha dirisha dogo la usajili Januari 2026, alikuwa na mabao mawili lakini ndani ya kikosi cha Wekundu hao akafunga manne na kumfanya sasa kuwa nayo sita, huku akifikisha asisti nne.
Kwa sasa kama timu yako inakwenda kukutana na Simba, lazima uwe na mpango wa namna gani ya kumzuia Mzambia huyo kwani ameshaweka wavuni mabao matatu akiyafunga mfululizo kwenye mechi tatu za timu hiyo zilizopita.
Alitangulia kuwafunga Yanga bao la kideoni, kisha akafunga dhidi ya JKT Tanzania na juzi akaweka lingine kambani kwenye ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Prisons. Katika mechi zote hizo tatu, Chama ameibuka mchezaji bora.
Kiwango bora cha kiungo huyo, kimewafanya viongozi wa klabu hiyo kufungua rasmi mazungumzo ya kumpa mkataba mpya baada ya ule wa sasa kubakiwa na takribani mwezi mmoja na nusu kabla ya kumalizika.
Taarifa kutoka ndani ya Simba zinaeleza kuwa mabosi wa klabu hiyo wameonyesha kuridhishwa na mchango wa nyota huyo raia wa Zambia ndani ya kikosi hicho, hasa katika kipindi hiki muhimu cha mwisho wa msimu.
Chanzo hicho kilidai kuwa Simba ipo tayari kumpa Chama mkataba mpya wa mwaka mmoja ili kuendelea kubaki Msimbazi huku mazungumzo ya awali kati ya pande hizo yakielezwa kwenda vizuri kutokana na utayari wa mchezaji huyo kuendelea kuitumikia timu hiyo.
Akizungumzia kiwango cha Chama, kocha wa Simba, Barker amesema: “Chama ameonyesha kiwango bora tangu alipojiunga nasi na kwa kweli amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu sana ndani ya kikosi hiki. Ana ubora mkubwa wa kiufundi, anajua kutengeneza nafasi na pia ana uwezo wa kubadili matokeo ya mchezo muda wowote.
“Bao alilofunga dhidi ya Yanga lilikuwa la kiwango cha juu sana. Kwa upande wangu ni moja ya mabao bora ambayo nimeyaona katika kipindi cha hivi karibuni kutokana na namna alivyokuwa mtulivu mbele ya lango na kumalizia kwa ubora mkubwa.
“Chama ameonyesha kiwango bora tangu alipojiunga nasi na kwa kweli amekuwa mmoja wa wachezaji muhimu sana ndani ya kikosi hiki. Ana ubora mkubwa wa kiufundi, anajua kutengeneza nafasi na pia ana uwezo wa kubadili matokeo ya mchezo muda wowote.”
Wakati huohuo, mchezaji wa zamani Simba, Dua Said amesema: “Huwa nashangaa sana mtu akisema Chama ni mkubwa kwa umri wakati anawaacha mbali vijana wengi sana kwenye ligi yetu hii, kwa hiyo jambo la msingi ni kutoa kile ambacho kinahitajika kwenye klabu.
“Chama anaweza kucheza hata misimu minne pale anachotakiwa ni kulinda afya yake ili tu asishuke kiwango, lakini si nje na hapo anauwezo wa kufanya makubwa sana na kuisaidia timu.”