Coastal Union yashikilia roho ya Yanga

Wachezaji 20 wa Yanga jana Jumatatu waliondoka jijini Dar es Salaam alfajiri kwenda Tanga kuwavaa Coastal Union, lakini Kocha Mkuu wa timu hiyo Hans Van Pluijm amewaacha Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza ambao hawezi kuwatumia kwenye mchezo huo.
Muktasari:
- Yanga ina pointi 31 huku Azam na Mbeya City zikiwa na pointi 30 kila moja, matokeo ya ushindi wowote kwenye mechi ya Kagera Sugar na Mtibwa kwenye Uwanja wa Kaitaba hakuweza kubadili msimamo kwenye nafasi nne za juu katika msimamo wa ligi hiyo. Simba itacheza na JKT Oljoro, Februari Mosi.
KUNA mechi nne kesho Jumatano kwenye Ligi Kuu Bara ambazo zitachezwa Kagera, Dar es Salaam, Pwani na Tanga.
Lakini kuna mechi tatu tu ambazo Tanzania nzima itakuwa ikizifuatilia kwa umakini.
Hizo ni Mbeya City dhidi ya Ruvu Shooting itakayochezwa Pwani, Azam na Rhino Rangers inayopigwa Chamazi na ile ya Yanga na Coastal Union mjini Tanga.
Yanga inataka kushinda ili isibanduke kileleni lakini ikiombea Azam na Mbeya City zipoteze au ziambulie japo sare zisihatarishe mbio zake za kutetea ubingwa.
Yanga ina pointi 31 huku Azam na Mbeya City zikiwa na pointi 30 kila moja, matokeo ya ushindi wowote kwenye mechi ya Kagera Sugar na Mtibwa kwenye Uwanja wa Kaitaba hakuweza kubadili msimamo kwenye nafasi nne za juu katika msimamo wa ligi hiyo. Simba itacheza na JKT Oljoro, Februari Mosi.
Wachezaji 20 wa Yanga jana Jumatatu waliondoka jijini Dar es Salaam alfajiri kwenda Tanga kuwavaa Coastal Union, lakini Kocha Mkuu wa timu hiyo Hans Van Pluijm amewaacha Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza ambao hawezi kuwatumia kwenye mchezo huo.
Katika orodha ambayo Mwanaspoti, imeipata Pluijm ameondoka na kikosi kizima ambacho kilicheza na Ashanti United, Jumamosi iliyopita, katika Uwanja wa Taifa jijini Dar na kushinda mabao 2-1 huku akiongezeka kipa Juma Kaseja na beki Rajab Zahir.
Pluijm amewaacha jijini Dar nyota sita wa kikosi hicho, wakiwemo Bakari Masoud, Shaaban Kondo, Reliants Lusajo, Hassan Dilunga, Okwi ambaye amesimamishwa na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kutokana na utata wa usajili wake na Hamis Kiiza ambaye bado mgonjwa wa malaria.
Kikosi kizima ambacho kimetua mkoani Tanga ni pamoja na makipa Juma Kaseja, Ally Mustapha ‘Barthez’ na Deogratias Munishi ‘Dida’ ambaye anapewa nafasi kubwa ya kuanza katika mchezo huo.
Mabeki ni Juma Abdul, Oscar Joshua, David Luhende,Mbuyu Twite, Kelvin Yondani, Rajab Zahir, Nadir Haroub ‘Cannavaro, viungo ni Frank Domayo, Mrisho Ngassa, Haruna Niyonzima,Nizar Khalfan, Hamis Thabit, Simon Msuva wakati washambuliaji ni Jerry Tegete, Said Bahanuzi,Didier Kavumbagu, Hussein Javu.
Katika hatua nyingine, Pluijm amewachimba mkwara wachezaji hao na kuwasisitiza kubadilika. Yanga ilicheza mechi ya kwanza ya mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ashanti United Jumamosi iliyopita na kuibuka na ushindi wa mabao 2-1 kwenye Uwanja wa Taifa.
“Kuna vitu vingine havihusiani na joto wala uchovu, tazama kuna wakati wachezaji wangu hawakucheza katika kiwango kimoja muda wote, kasi waliyoanza nayo si waliyomalizia na muda wote tulikuwa hatuna amani katika benchi,” alisema kocha huyo kusisitiza kuwa kitu ambacho wachezaji wa Yanga wanapaswa kufahamu ni kwamba wanacheza katika timu kubwa ambayo inahitaji matokeo.
“Kuna wakati tulitakiwa kucheza kwa kasi na kushtukiza, lakini tukawa tunachelewa kuchukua uamuzi, nitashughulikia hali hii kwani inaonekana timu nyingi zimejiandaa ili zibaki katika ligi,” alisema Pluijm aliyewahi kuinoa Belekum Chelsea ya Ghana.