Prime
Fadlu ageuka mbogo Simba, acharukia mastaa

Muktasari:
- Simba ilicheza na kushinda mechi hizo za viporo dhidi ya Mashujaa iliyoifunga mabao 2-1, ikailaza JKT Tanzania kwa bao 1-0 kisha kuicharaza Pamba Jiji 5-1 na juzi ikailaza KMC mabao 2-1 na kuvuna pointi 12 zilizopunguza pengo la pointi baina ya timu hiyo na vinara Yanga kutoka 13 hadi kuwa moja.
KOCHA wa Simba, Fadlu Davids amegeuka mbogo kwa kuwacharukia mastaa wa timu hiyo kutokana na matokeo ya mechi nne za viporo vya Ligi Kuu Bara, akiwakumbusha pia kazi iliyopo mbele yao katika fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane ya Morocco wikiendi hii ugenini.
Simba ilicheza na kushinda mechi hizo za viporo dhidi ya Mashujaa iliyoifunga mabao 2-1, ikailaza JKT Tanzania kwa bao 1-0 kisha kuicharaza Pamba Jiji 5-1 na juzi ikailaza KMC mabao 2-1 na kuvuna pointi 12 zilizopunguza pengo la pointi baina ya timu hiyo na vinara Yanga kutoka 13 hadi kuwa moja.
Lakini pamoja na ushindi huo wa mechi hizo nne mfululizo, kocha Fadlu ameonyesha kuchukizwa na kitendo cha ngome ya timu hiyo kuruhusu mabao katika mechi tatu, huku moja tu ndio wakipata clean sheet dhidi ya JKT Tanzania, jambo linalomtia presha wanapoenda kuikabili RS Berkane.
Simba iliyoondoka leo kwenda Morocco itavaana na Berkane Jumamosi kwenye mechi ya kwanza na fainali ya Kombe la Shirikisho itakayopigwa kuanzia saa 4:00 usiku kabla ya kurudiana wiki moja baadaye Kwa Mkapa, huku Kombe likiwa uwanjani na Fadlu alisema kiu yake ni kuhakikisha kila kitu kinamalizika ugenini Morocco.
Kocha huyo alisema kuruhusu mabao matatu katika mechi hizo za Ligi Kuu kunaonyesha kujisahau kwa wachezaji na ndio maana amelazimika kukaa nao ili kuwakumbusha kabla ya kuifuata Berkane kuwa wanatakiwa kuwa makini kwa nia ya kutengeneza mazingira mazuri ya kubeba taji la Afrika.
Akizungumza na Mwanaspoti, Fadlu alisema licha ya kikosi chake kubeba pointi 12 katika mechi hizo, bado kuna makosa yaliyofanyika ambayo ni lazima yarekebishwe kabla ya mechi mbili za fainali dhidi ya Berkane ambayo ina rekodi ya kushinda kwa idadi kubwa hya mabao katika mechi za CAF ikiwa nyumbani.
Fadlu alisema moja ya makosa makubwa ni kuruhusu wapinzani kukufunga, hata kama hatabeba pointi, lakini inaonyesha wewe una udhaifu na siku zote timu imara ni ile isiyopoteza wala kuruhusu bao.
“Haikuwa sawa kwa mechi nne kupata ‘clean sheet’ moja tu, na makosa kama haya hayatakiwi kuonekana hasa katika mechi tunazokwenda kucheza,” alisema Fadlu na kuongeza;
“Kuanzia eneo la kati hadi ulinzi, kumekuwa na makosa ya kutoa nafasi kwa wapinzani kufanya uamuzi, kitu kisichotakiwa kitokee dhidi ya Berkane.”
Kuhusu safari ambayo Simba imeianza leo kuifuata Berkane, Fadlu alisema; “Timu itaondoka alfajiri ya kuamkia kesho (leo) kwa sababu wanataka kuwahi ili kuzoea hali ya hewa huko na kupata utulivu wa mwili na akili kabla ya mechi hiyo muhimu.”
Hadi inaondoka, Simba imecheza jumla ya mechi 26 za Ligi Kuu Bara sawa na Yanga, ikishinda 22 kutoka sare tatu na imepoteza mmoja, ikikusanya pointi 69, moja nyuma ya ilizonazo Yanga yenye 70, lakini ikifungwa mabao 11 na kufunga 62, huku kipa Moussa Camara akiwa na clean sheet 16, akimzidi Diarra Djigui wa Yanga mwenye 14.
Idadi hizo za clean sheet alizonazo Camara zimemfanya kipa huyo kutoka Guinea kuvunja rekodi iliyowekwa misimu uliopita na aliyekuwa kipa wa Coastal Union, Ley Matampi aliyemaliza msimu akiwa na clean sheet 15, moja zaidi ya alizokuwa nazo Diarra aliyemaliza na 14.