Feisal akoleza vita ya ufungaji bora Ligi Kuu ya NBC
Muktasari:
- Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa leo Mei 25, 2026 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, Fei Toto alianza kufungua ukurasa wa mabao dakika ya tatu, akimalizia krosi ya beki, Landry Zouzou, kisha kufunga la pili dakika ya 16, akipokea pasi ya kiungo, Idd Seleman 'Nado'.
KIUNGO mshambuliaji wa Azam FC, Feisal Salum 'Fei Toto' ameendelea kukoleza vita ya ufungaji bora ndani ya Ligi Kuu Bara msimu huu 2025-2026, baada ya kuifungia timu hiyo mabao mawili, katika ushindi wa 3-0 dhidi ya KMC FC.
Katika mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara iliyochezwa leo Mei 25, 2026 kwenye Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam, Fei Toto alianza kufungua ukurasa wa mabao dakika ya tatu, akimalizia krosi ya beki, Landry Zouzou, kisha kufunga la pili dakika ya 16, akipokea pasi ya kiungo, Idd Seleman 'Nado'.
Wakati KMC ikipambana kusawazisha mabao hayo, ilishindwa kumudu presha ambapo dakika ya 34, beki wa kati, Yoro Diaby aliifungia Azam bao la tatu kwa kichwa akimalizia Frii-Kii' ya Nado.
Mabao mawili ya Fei Toto yanamfanya kiungo huyo kufikisha 14 katika Ligi Kuu msimu huu akiwa ndiye kinara, akifuatiwa na nyota wa Yanga, Allan Okello mwenye 11, baada ya kuifungia timu hiyo mawili wakishinda 3-1 dhidi ya Namungo FC, leo Mei 25, 2026.
Matokeo hayo yanaiweka KMC katika hatari zaidi na huenda ikashuka rasmi daraja na kushiriki Ligi ya Championship msimu ujao, ikiwa Mbeya City itashinda mechi yake kesho Jumanne Mei 26, 2026 itakapocheza dhidi ya Singida Black Stars kwenye Uwanja wa Airtel mkoani Singida.
Mbeya City inayoshika nafasi ya 14 na pointi 22, ikiwa itaifunga Singida itafikisha pointi 25, ambazo zitaishusha moaj kwa moja KMC ambayo hata ikishinda mechi zote tano zilizobaki, itaishia na pointi 24 na kuendelea kuiacha nafasi mbili za chini.
Katika mechi 25 ilizocheza Azam, imeshinda 14, sare kumi na kupoteza moja, ikifunga mabao 38 na kuruhusu tisa, ikishika nafasi ya tatu ikikusanya pointi 52, nyuma ya vinara Yanga yenye pointi 60 na Simba iliyo nafasi ya pili na pointi 58.
Kwa upande wa KMC, imefikisha mechi 12 za Ligi Kuu Bara bila ya ushindi tangu mara ya mwisho kwa kikosi hicho kilipoifunga Mashujaa bao 1-0, katika pambano lililopigwa Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi, Februari 3, 2026.
Kwa jumla, KMC msimu huu imecheza mechi 25, imeshinda mbili, sare tatu na kupoteza 20, ikifunga mabao 13 na kuruhusu nyavu zake kutikiswa mara 43, ikiburuza mkiani mwa msimamo ikiwa nafasi ya 16 baada ya kukusanya pointi tisa. Bado mechi tano kumaliza msimu huu.