First eleven mpya ya Simba na Yanga
Muktasari:
- Kabla ya mechi ya leo Jumamosi itakayozikutanisha Yanga na Mtibwa Sugar, Simba imecheza mechi nane za mzunguko wa pili huku Yanga ikiwa imecheza mechi nne tu.
MZUNGUKO wa pili wa Ligi Kuu Bara unaelekea ukingoni huku kukiwa na ushindani mkubwa kuwania nafasi tatu za juu baina ya timu za Azam, Yanga, Mbeya City na Simba.
Kabla ya mechi ya leo Jumamosi itakayozikutanisha Yanga na Mtibwa Sugar, Simba imecheza mechi nane za mzunguko wa pili huku Yanga ikiwa imecheza mechi nne tu. Wapo wachezaji wenye majina makubwa na ghali waliosajiliwa na Simba na Yanga lakini bado hawajafanya lolote jipya kwenye mzunguko wa pili.
Timu ya Mwanaspoti imefanya tathmini ya utendaji wa wachezaji mbalimbali wa Simba na Yanga uwanjani katika mechi za mzunguko wa pili pekee na kupata kikosi cha kwanza cha mseto cha timu hizo kongwe nchini kilichofanya vizuri mpaka sasa.
1. Deo Munishi ‘Dida’ (Yanga)
Kipa huyu alijiunga na Yanga mwanzoni mwa msimu huu akiwa amemkuta Ally Mustapha ‘Barthez’ akiwa namba moja baadaye Desemba mwaka jana akawasili Juma Kaseja na kumwongezea changamoto ya kucheza kikosi cha kwanza.
Kocha Hans Van Der Pluijm ameonyesha kumwamini na kumpa nafasi akiwapiku Kaseja na Barthez kwani katika mechi kumi za mashindano alizocheza, amefungwa mabao manne tu. Ameonyesha uimara langoni kuliko hata Ivo Mapunda wa Simba.
2.Mbuyu Twite (Yanga)
Kiraka Mbuyu Twite ameonyesha uwezo mkubwa katika kikosi cha Yanga, akicheza beki ya kulia kutokana na uwezo wake mkubwa wa kuzuia na kupandisha mashambulizi huku akisaidia viungo katika kuzuia.
Amekuwa msaada mkubwa kukaba na mabeki wa kati pindi wanapofanya makosa. Twite ndiye mbadala wa kwanza katika beki ya kati endapo Kelvin Yondani au Nadir Haroub ‘Cannavaro’ mmoja wao asipokuwemo kikosini, mipira yake ya kurusha haitofautiani na mipira ya kona.
3.Oscar Joshua (Yanga)
Beki wa kushoto Oscar Joshua wa Yanga hana vitu vingi uwanjani kwani huwa anafanya kazi mbili tu za msingi, kukaba na kupiga krosi za maana huku akiwa na uwezo mkubwa wa kupiga mashuti langoni.
Uwezo wake katika mzunguko wa pili umemshawishi Kocha Pluijm kumpa nafasi kikosi cha kwanza na amekuwa akicheza mechi nyingi za Yanga katika nafasi hiyo. Hana mchezo anapokuwa kazini.
4.Joseph Owino (Simba)
Beki wa kati Joseph Owino alijiunga na Simba mwanzoni mwa msimu huu akitokea URA ya Uganda na moja kwa moja akaingia kikosi cha kwanza. Tangu amesajiliwa Simba hajakosa kikosi cha kwanza. Anacheza kwa kutumia akili sana kuzuia mashambulizi ya timu pinzani huku akiwa na uwezo mkubwa wa kuwaongoza wenzake uwanjani hadi kocha Zdravko Logarusic amempa unahodha sasa. Mwanzo alikuwa anacheza na Gilbert Kaze, sasa yupo na Donald Mosoti. Wameruhusu mabao kadhaa katika mechi za karibuni lakini tathmini ya kiufundi inathibitisha ni kutokana na kupanguliwa kwa ukuta huo mara kwa mara.
5.Kelvin Yondani (Yanga)
Miongoni mwa mabeki bora wa kati kwa sasa ni Kelvin Yondani, katika kikosi cha Yanga anacheza sambamba na Nadir Haroub ‘Cannavaro’. Sifa kubwa ya Yondani ni uwezo mkubwa wa kumiliki mpira na kuzuia bila kusababisha faulo zisizo na maana.
Yondani ni mzuri ndani na nje ya eneo la 18 la timu yake, ana uwezo wa kupiga chenga na kupandisha timu anapoona mambo hayaendi sawa katika sehemu ya kiungo ya timu yake na ndiyo maana hakosekani katika kikosi cha Taifa Stars. Bado amekuwa msaada mkubwa kwa Yanga mzunguko wa pili.
6.Jonas Mkude (Simba)
Hakuna kiungo chipukizi anayecheza kwa malengo kama Jonas Mkude. Alichezea Simba B kabla ya kupandishwa msimu uliopita na sasa amejihakikishia nafasi katika kikosi cha Simba na kuwaacha wakongwe wakisugua benchi.
Tofauti na viungo wengine wa Simba na Yanga, Mkude hana mbwembwe zisizo na maana kwa kucheza na jukwaa bila manufaa, anajua anachofanya uwanjani na anaunganisha vyema safu ya kiungo, mabeki na washambuliaji. Alikuwa kipenzi cha aliyekuwa Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen lakiwa hakuwa akimtumia kikosini kwa kile kilichoelezwa nidhamu ndogo ya kuchelewa kambini kila alipoitwa kikosini. Logarusic anamtumia kwa mambo mengi mzunguko wa pili.
7.Ramadhan Singano ‘Messi’ (Simba)
Ni mfupi huku akiwa na mwili wa wastani lakini ana miguu yenye sumaku inayomwezesha kunasa mpira na kukaa nao mguuni atakavyo. Ana chenga za maudhi zinazowachanganya mabeki wa timu pinzani. Ana mchango mkubwa katika kikosi cha Simba.
Messi atacheza kwa muda mrefu kwenye kikosi cha Simba kutokana na aina ya maisha anayoishi kwani haendekezi anasa kama wachezaji wengine. Ni roho ya timu kwa sasa.
8. Frank Domayo (Yanga)
Kama ilivyo kwa Jonas Mkude, Frank Domayo ni miongoni mwa viungo chipukizi wanaofanya vizuri nchini na hakosi katika kikosi cha Taifa Stars. Tangu alipotua Yanga akitokea JKT Ruvu mwaka juzi, ameonyesha uwezo mkubwa kiasi cha kuhatarisha nafasi ya Athuman Idd ‘Chuji’ kikosini.
Domayo ana uwezo wa kukaba na kupandisha mashambulizi lakini kubwa zaidi ni uhodari wake wa kupiga pasi zenye macho kwenda kwa washambuliaji. Hana mbwembwe zisizo na maana uwanjani, anapendwa na makocha kutokana na kucheza kwa kufuata maelekezo.
9. Amissi Tambwe (Simba)
Hana vitu vingi uwanjani, anaingia kufanya kile alichoajiriwa kufanya. Kufunga magoli timu ishinde. Vyenga watapiga wengine. Huyu jamaa ana akili ya kujua nafasi ya kusimama uwanjani ili apokee pasi na kufunga.
Hadi sasa amefunga mabao 19 katika ligi hii na kuongoza katika orodha ya wafungaji bora, achana na mengine aliyofunga katika michuano tofauti na Ligi Kuu. Tambwe ni mshambuliaji bora pengine anayelipwa tofauti na uwezo wake uwanjani, anapata mshahara wa Dola 800 tu ambazo ni zaidi ya Sh. 1.2 milioni.
10. Didier Kavumbagu (Yanga)
Kavumbagu sasa yupo katika kiwango kizuri ndiyo maana kocha wa Yanga, Pluijm amekuwa hamtupi katika kikosi cha kwanza. Kama ilivyo kwa Tambwe, Kavumbagu anajua kuzifumania nyavu na ana uwezo wa kusumbua mabeki, akisimamishwa kwenye fowadi na Tambwe itakuwa ni habari nyingine.
Kavumbagu amefunga mabao manane tu katika ligi hii lakini ametoa mchango mkubwa wa mabao mengine yaliyofungwa na timu yake, si mchoyo wa pasi za mwisho lakini kubwa zaidi ni uwezo wake wa kukaba kwa kutafuta mwenyewe mipira.
11. Mrisho Ngassa (Yanga)
Bado Mrisho Ngassa anaweza kutajwa kama winga bora nchini kutokana na uwezo wake wa kupiga chenga, kumiliki na kukokota mpira huku akimudu kupiga krosi za maana kwa washambuliaji.
Ana nafasi ya kudumu katika kikosi cha Yanga huku akimudu kucheza winga yoyote, kulia au kushoto. Pia mambo yakiharibika anaweza kucheza kama kiungo mshambuliaji wa kati. Amefunga mabao manane katika ligi sawa na Kavumbagu. Hakuna kocha anayependa ushindi na soka la kushambulia anayeweza kumweka Ngassa benchi.