Fountain Gate na rekodi mpya Ligi Kuu

Muktasari:
- Fountain Gate imepoteza mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Jumatatu wiki hii kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa mkoani Manyara.
KICHAPO cha mabao 4-0 ilichopokea Fountain Gate kutoka kwa Yanga, kimeweka rekodi mpya ndani ya Ligi Kuu Bara msimu huu ikiipiku Mashujaa.
Fountain Gate imepoteza mchezo huo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Jumatatu wiki hii kwenye Uwanja wa Tanzanite Kwaraa mkoani Manyara.
Kwa kipigo hicho, imeifanya Fountain Gate kufungwa na Yanga jumla ya mabao 9-0 katika mechi mbili walizokutana ndani ya Ligi Kuu Bara msimu huu baada ya ile ya kwanza kuchapwa 5-0.
Yanga inayoongoza kwa kufunga mabao mengi Ligi Kuu Bara msimu huu ikifikisha 68 huku ikiwa ndiyo timu pekee iliyotikisa nyavu za wapinzani wake wote iliokutana nao, kabla ya kuifunga Fountain Gate, Mashujaa ndiyo ilikuwa imeruhusu mabao mengi zaidi dhidi yao msimu huu.
Katika mechi mbili ambazo timu hizo zimekutana msimu huu, matokeo ya jumla yalikuwa Yanga 8-2 Mashujaa. Hiyo ni baada ya mechi ya kwanza Yanga kushinda 3-2 na ile ya pili kuibuka na ushindi mwingine wa 5-0.
Timu inayofuatia kwa kufungwa mabao mengi na Yanga kwenye ligi msimu huu baada ya Mashujaa ni Pamba Jiji iliyopigwa jumla ya mabao 7-0, huku KenGold na KMC zote zikichapwa 7-2.
Matokeo mengine ya jumla ambayo Yanga imeyapata kwa kucheza mechi mbili dhidi ya wapinzani wao hadi sasa ni; Yanga 6-0 Kagera Sugar, Yanga 3-1 Singida BS, Yanga 4-3 Tabora United, Yanga 2-0 JKT Tanzania, Yanga 2-0 Coastal Union na Yanga 2-2 Azam.
Yanga kwa sasa imebakiwa na mechi nne kumaliza msimu huu, bado haijarudiana na Tanzania Prisons (4-0), Dodoma Jiji (4-0), Namungo (2-0) na Simba (1-0) ambapo mechi za duru la kwanza zote ilishinda, hivyo inaweza kuweka rekodi ya mabao kwa timu nyingi kuipiku Fountain Gate.