Fufuni bila Mani Gamera’ ni mateso
Muktasari:
- Timu hiyo inakutana na dhoruba hiyo siku chache baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Suleiman Mohamed ‘Mani Gamera’ kuachana nayo.
Fufuni imeanza kupoteza uelekeo wa kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) baada kushindwa kupata ushindi katika mechi mbili zilizopita ikiambulia pointi moja.
Timu hiyo inakutana na dhoruba hiyo siku chache baada ya aliyekuwa Kocha Mkuu wa kikosi hicho, Suleiman Mohamed ‘Mani Gamera’ kuachana nayo.
Wakati akizungumza na Mwanaspoti, Gamera amesema chanzo cha kuondoka ni uongozi haukuridhishwa na kikosi alichopanga katika mechi ya Kombe la FA kikiwa tofauti na kile kinachocheza Ligi Kuu Zanzibar, hali iliyofanya kupoteza.
Tangu Gamera aachane na timu hiyo, imecheza mechi mbili ikitoka sare ya 1-1 dhidi ya New King, kisha kufungwa 2-1 na KVZ, zote zikichezwa kisiwani Pemba.
Katika hesabu za kocha huyo, amesema sababu ya kuchezesha kikosi namba mbili kwenye Kombe la FA ni kuona ugumu wa mechi zilizofuatana za ligi dhidi ya New King, KVZ na JKU ili kujihakikishia ubingwa wa ZPL.
Kwa sasa timu hiyo ipo chini ya Kocha Msaidizi, Suleiman Abdalla ikiendelea kusalia nafasi ya tatu ikiachwa pointi saba na vinara KVZ yenye 55, huku yenyewe ikiwa na 48.
Inaelezwa, kuondoka kwa kocha huyo, Fufuni imekosa uelekeo na baadhi ya wadau kukatisha misaada kwani alikuwa nguzo imara klabuni hapo.
Fufuni iliyobakisha michezo minne kumaliza msimu huu dhidi ya JKU, KMKM, Muembe Makumbi na Uhamiaji, inatakiwa kushinda mbili kati ya hizo ili kujihakikishia kubaki nne bora.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mani Gamera amesema licha ya timu hiyo kupitia kipindi kigumu bila ya uwepo hana mpango wa kurudi kwa sababu viongozi hawajamfuata kutaka suluhisho lolote upande wake.
“Viongozi wa timu hawajanitafuta na mimi nimekaa kimya, nimeamua kuwaachia timu yao wafanye wanavyotaka,” amesema.
Gamera amesema zipo baadhi ya tabia ambazo viongozi au makocha hawazitaki zitokee kwenye timu hususani katika kipindi kama hiki cha lala salama, ndio maana wengine wanaanzisha migogoro kupata nafasi.
Ofisa Habari wa timu hiyo, Ame Ali amesema bado uongozi upo kwenye mazungumzo kumrudisha kocha huyo kwani ameondoka bila ya baraka za klabu.