Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

KVZ, Fufuni jino kwa jino, Malindi shaka ZPL

Muktasari:

  • Ushindani katika mbio za ubingwa unatokana na tofauti ndogo ya pointi kati ya vinara KVZ yenye pointi 55, ikifuatiwa kwa karibu na JKU (pointi 49) na Fufuni (pointi 48).

WAKATI Ligi Kuu Zanzibar (ZPL), ikielekea ukingoni, maji na mafuta vianza kujitenga kutokana na ushindani wa kila eneo kutoka wasaka ubingwa hadi wale wanapigana kubaki katika ligi hiyo msimu huu.

Ushindani katika mbio za ubingwa unatokana na tofauti ndogo ya pointi kati ya vinara KVZ yenye pointi 55, ikifuatiwa kwa karibu na JKU (pointi 49) na Fufuni (pointi 48).

Licha ya ushindani huo vinara KVZ, ipo katika nafasi nzuri ya kutwaa ubingwa msimu huu ikiwa na michezo mitano mkononi inahitaji kushinda mechi tatu na sare moja ili kumefikisha pointi 65 ambazo JKU haiwezi kuzifikia.

JKU ipo nafasi ya pili ikiwa na pointi 49, na mechi tano mkononi iwapo itashinda mechi zote itafikisha pointi 64. Naye wafuata kwa karibu ni Fufuni pamoja na kufanya vibaya katika mechi mbili za mzunguko wa 25 na 26, lakini bado ipo kwenye mbio hizo kwani ina uwezo wa kumaliza msimu na pointi 60 kama itashinda katika mechi nne zilizobakia huku ikiomba mbaya kwa wapinzani wake.

Kibarua kizito kipo kwa timu hizo tatu zinazowania ubingwa wa ZPL ambapo kuna mechi ya uamuzi inayozikutanisha Fufuni dhidi ya JKU, zilipokutana mzunguko wa kwanza, JKU iliibuka na ushindi wa bao 1-0.

Mechi hiyo itakuwa na mambo mawili muhimu, JKU ikishinda maana yake itazidi kuweka hai matumaini ya kubeba ubingwa, huku Fufuni ikitolewa katika mbio hizo taratibu. Kinyume chake, itaibeba KVZ ambayo yenyewe inaomba iwe sare.

Hatua ya kubaki timu tatu kwenye mbio hizo za ubingwa imekuja baada ya zingine mbili zilizokuwepo mwanzo kutofanya vizuri mechi mbili zilizopita.

Kwa kushika nafasi ya tatu na kuendelea kuwa kwenye mbio za ubingwa, zinaifanya Fufuni kuwa miongoni mwa timu zilizofanya vizuri zaidi msimu huu ikiwa ni msimu wake wa kwanza baada ya kupanda daraja ikiwa na New Stone Town, Polisi na New King ambazo hali zao sio nzuri. New Stone imeshashuka, Polisi na New King hazina uhakika wa kubaki.


TIKETI YA MAPINDUZI MOTO

Mbali ya vita ya ubingwa ipo vita ya kusaka kumaliza nafasi ya nne ya kupata tiketi ya kushiriki mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu ujao.

Mabingwa watetezi Mlandege, Zimamoto na Uhamiaji baada ya kupoteza matumaini ya kutwaa ubingwa zimeingia katika vita ya kumaliza nne bora.

Mlandege ikifanikiwa kupanda hadi nafasi ya nne katika msimamo ikikusanya pointi 43 sawa na Zimamoto iliyoshuka hadi nafasi ya tano, huku Uhamiaji sare zake mbili mfululizo dhidi ya Kipanga (0-0) na JKU (1-1), imeporomoka hadi nafasi ya sita ikiwa na pointi 42.

Timu hizo zinapambana kumaliza nafasi nne za juu ili msimu ujao zipate tiketi ya kushiriki Kombe la Mapinduzi.


VITA YA KUSHUKA DARAJA

Wakati kule juu hali ikiwa ya moto, huku chini pia kuna vita ya kujinusuru kushuka daraja ambapo tayari timu mbili zimeshatangulia kushiriki Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao ambazo ni Junguni United na New Stone. Zinasubiriwa zingine mbili kukamilisha idadi ya timu nne zinazopaswa kushuka.

Timu ambazo zipo mahututi na zinafanya jitihada za kujinusuru kushuka daraja msimu huu ni Malindi iliyopo nafasi ya 14 ikiwa imeshacheza mechi 25 na kuvuna pointi 25. Nyingine ni Polisi iliyopo nafasi ya 13 na pointi 29.

Kibarua cha Malindi inatakiwa kushinda mechi zote tano ili kuwa na pointi 40, kisha iiombee mabaya Polisi kwani yenyewe ikishinda mechi nne tu, basi uhakika wa kubaki inao kutokana na kufikisha pointi 41.

Timu ya Chipukizi, Muembe Makumbi na New King, yoyote inaweza kushuka endapo Malindi na Polisi zikifanikiwa kufanya vizuri, kisha zenyewe zikateleza.

Baada ya kuanza vizuri msimu huu wa Ligi Kuu Soka Zanzibar, Malindi ghafla kibao kimegeuka kwa kutoka kuwania ubingwa wa ZPL hadi sasa kupambana kujinusuru isishuke.

Malindi ambayo baada ya mechi sita za kwanza ilikuwa kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu Soka Zanzibar ikikusanya pointi 14, kwa sasa imeporomoka hadi nafasi ya 14 ikifikisha pointi 25.

Kesho kutawakutanisha timu mbili zinazojinusuru kushuka daraja ambapo vita ya jasho na damu itapigwa kati ya Polisi na Malindi. Mtanange mwingine utachezwa Mei 26, 2026 kati ya Malindi na Muembe Makumbi.

Mei 27, 2026, vita nyingine itapigwa kisiwani Pemba kati ya Polisi na Chipukizi na Juni 13, 2026, itakuwa Mafunzo dhidi ya Polisi.

Mechi hizo zinaonesha namna ambavyo timu zilizopo kwenye hatari ya kushuka daraja zinahitaji kuchanga vizuri karata zao kipindi hiki cha kuelekea mwisho wa msimu.

Msimamo wa ligi hiyo kwa sasa unatukumbusha msimu wa 2024-2025 namna ambavyo timu zinavyokimbizana kule juu. Msimu uliopita Mlandege ilitwaa ubingwa kwa tofauti ya mabao, ikimaliza kileleni na pointi 62 sawa na KVZ.

Mlandege ilimaliza msimu na jumla ya mabao 67 ya kufunga na kufungwa 21, ikiwa na tofauti ya mabao 46, wakati KVZ ilifunga mabao 35 na kufungwa 12, tofauti yake ni mabao 23.