Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Josiah, TZ Prisons lolote litatokea

Muktasari:

  • Timu hiyo iliyopo nafasi ya 15 kwa pointi 18, haijawa na mwenendo mzuri tangu kukabidhiwa majukumu, kocha Aman Josiah aliyerithi nafasi ya Mbwana Makata aliyesitishiwa mkataba.

KIPIGO cha mabao 4-0 walichokumbana nacho Tanzania Prisons kutoka kwa Azam FC, huenda kikaondoka na kichwa cha mtu kufuatia mfululizo wa matokeo yasiyoridhisha kwa maafande hao.

Timu hiyo iliyopo nafasi ya 15 kwa pointi 18, haijawa na mwenendo mzuri tangu kukabidhiwa majukumu, kocha Aman Josiah aliyerithi nafasi ya Mbwana Makata aliyesitishiwa mkataba.

Katika mechi nane alizoongoza ikiwamo ya Kombe la Shirikisho na Ligi Kuu, kocha huyo aliyetokea Geita Gold iliyombeba kutoka Biashara United, alishinda moja dhidi ya Mashujaa 2-1, sare moja mbele ya Tabora United na kupoteza sita.

Walipoteza dhidi ya Simba 3-0, Namungo 0-1, Dodoma Jiji 3-2, Fountain Gate 1-0 na Azam 4-0 huku wakiondoshwa kwa penalti 4-3 dhidi ya Bigman ya Championship katika Kombe la Shirikisho.

Maafande hao waliowahi kushuka daraja msimu wa 2011/12 kisha kupanda msimu uliofuata, wametia hofu mashabiki kwani zinaonekana ni moja ya timu zilizopo katika hatari ya kushuka daraja moja kwa moja au kupitia play-off kama haitaweza kutumia vyema mechi saba zilizosalia za Ligi Kuu.

Taarifa ilizopata Mwanaspoti kutoka katika moja ya chanzo cha timu hiyo, zimeeleza kuwa, kocha Josiah huenda asifike mchezo ujao dhidi ya KMC, Aprili 2.

Imeeleza kuwa kwa sasa vikao vinaendelea kufanya tathmini ya mwenendo na huenda ukatoka uamuzi mgumu wa kuachana na kocha huyo kabla au baada ya mechi na KMC.

“Haijawa rasmi kwa kuwa vikao vinaendelea, hivyo tunaweza kupata taarifa kabla au baada ya mechi dhidi ya KMC, zaidi ni suala la matokeo kutokuwa mazuri,” kilisema chanzo hicho.

Mtendaji Mkuu wa TZ Prisons, John Matei alipoulizwa kuwapo kwa mipango ya kuachana na kocha huyo, alisema hana taarifa hizo akieleza kuwa wanaenda kujipanga kwa ajili ya mchezo ujao dhidi ya KMC.

Alikiri matokeo kutokuwa mazuri akieleza kuwa uongozi unajipanga kuweka mambo sawa ikiwamo hamasa kwa wachezaji kuhakikisha michezo saba iliyobaki wanafanya vizuri.

“Taarifa za kuachana na kocha sijazipata, lakini ni kweli matokeo si mazuri na yanatuumiza, uongozi unaenda kufanya liwezekanalo kuhakikisha mechi zilizobaki kuanzia KMC tunashinda,”  alisema bosi huyo.

Katika mechi saba ilizobakiza Prisons itacheza michezo minne nyumbani dhidi ya Kagera Sugar, JKT Tanzania, Coastal Union na Yanga na mitatu ugenini dhidi ya KMC, Ken Gold na Singida BS.

Kwa sasa timu hiyo ipo mapumziko na inatarajia kurejea kambini kuendelea na mazoezi Jumatatu ya wiki ijayo kujiandaa na mechi dhidi ya KMC ugenini KMC Complex, Dar es Salaam Aprili 2 mwaka huu.