Juhudi za kuondoa maji zashika kasi Kwa Mkapa

Muktasari:
- Katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, juhudi kubwa zinaendelea kuondoa maji kwa uchache yaliyotuama kwenye baadhi ya maeneo ya kuchezea.
WAKATI umesalia muda mfupi kabla ya mchezo wa robo fainali ya pili kupigwa, hali ya hewa ya mvua iliyoanza kunyesha mapema leo imeleta changamoto katika maandalizi ya mchezo huo.
Katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, juhudi kubwa zinaendelea kuondoa maji kwa uchache yaliyotuama kwenye baadhi ya maeneo ya kuchezea.
Watu wanaoonekana kuwa na utambulisho maalum kwa kuvaa bips wamejigawa maeneo tofauti ya uwanja huo. Kila kundi linafanya kazi kuhakikisha maji yanayotuama hayataathiri ubora wa mchezo unaosubiriwa kwa hamu.

Baadhi yao wanaonekana wakitumia magodoro madogo kujaribu kunyonya maji kwenye sehemu za nyasi ambazo zimeathirika zaidi.
Wengine, wakiwa na mifagio maalum ya kusukuma maji, wanafagia kujaribu kuyasukuma maji kuelekea pembeni mwa uwanja. Kazi yao inafanywa kwa haraka kutokana na muda wa mchezo kuwqdia.
Licha ya mvua kuacha kunyesha kwa muda, uwanja bado unaonekana kuwa na unyevu, jambo linalowalazimu waandaaji kufanya kazi ya ziada kuhakikisha kila kona inakuwa salama kwa mchezo.

Mashabiki wachache waliowahi kuingia mapema uwanjani wamekuwa mashahidi wa juhudi hizo, wengine wakichukua picha na video, huku wengine wakionekana kuwa na wasiwasi iwapo mchezo huo utaweza kuchezwa katika hali ya kuridhisha.
Waamuzi wa mchezo walionekana wakikagua baadhi ya maeneo ya uwanja, huku wakiwasiliana na maofisa wa CAF kuhakikisha masharti ya uchezaji katika hali ya mvua yanazingatiwa.

Timu zote zinazokutana leo, Simba na Al Masry zinaripotiwa kuwa tayari zimeshafika uwanjani na zinajiandaa kwa mechi hiyo muhimu. Hali ya hewa kwa sasa ni ya mawingu, lakini hakuna dalili za mvua nyingine kunyesha katika muda mfupi ujao.

Huku mashabiki wakizidi kumiminika uwanjani, Simba inahitaji ushindi wa mabao 3-0 ili kutinga hatua ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.