Juma Abdul ataja 'Top 5' ya mastraika hatari

Muktasari:
- Aliwataja washambuliaji hao waliowahi kuibuka vinara wa mabao Ligi Kuu Bara, Mussa Hassan Mgosi aliyeibuka mfungaji Bora msimu wa 2019/10 akifunga mabao 18), Fiston Mayele aliyetamba na Yanga kwa misimu miwili, 2022/23 akifunga mabao 16 na 2022/23 alipoibuka kinara na mabao 17).
BEKI wa zamani wa Mtibwa Sugar, Yanga na Singida Big Stars, Juma Abdul ameitaja 5-Bora ya washambuliaji aliowashudia ubora wao kwa namna walivyokuwa wanawaliza mabeki waliokuwa wanaidharau mipira iliyokufa na kujikuta wakiruhusu mabao ya kizembe.
Aliwataja washambuliaji hao waliowahi kuibuka vinara wa mabao Ligi Kuu Bara, Mussa Hassan Mgosi aliyeibuka mfungaji Bora msimu wa 2019/10 akifunga mabao 18), Fiston Mayele aliyetamba na Yanga kwa misimu miwili, 2022/23 akifunga mabao 16 na 2022/23 alipoibuka kinara na mabao 17).
Pia amemtaja Amissi Tambwe aliyewahi kutamba na Simba kabla ya kuhamia Yanga akiibuka Mfungaji Bora msimu wa 2013/14 akiwa na Simba akifunga mabao 19 na 2015/16 akiwa Yanga akiibuka pia kinara kwa mabao 21) na Meddie Kagere aliyetamba Simba na kuwa mfungaji bora misimu miwili mfululizo 2018/19 (mabao 23) ma 2019/20 alipofunga 22) pamoja na John Bocco, kinara wa mabao wa Ligi Kuu kwa muda wote akiwa na 156 akitumika kwa misimu 17 mfululizo.
Beki huyo aliyestaafu kwa sasa, alisema washambuliaji hao walikuwa bora katika mipira ya kutengwa ambayo mara nyingi mabeki wanaipuuzia, ilhali mastraika hao walikuwa ni wataalamu wa kukaa maeneo ya hatari na kufunga kwa kuwashtukiza.
“Nafahamu kuna washambuliaji bora kabla yao, ila hao nawataja nilikuwa nakutana nao katika mechi najua shughuli yao, siyo washambuliaji wavivu muda wote wakiwepo uwanjani walionyesha wanahitaji kucheka na nyavu,” alisema Juma na kuongeza;
“Wengine wanaendelea kucheza kama Bocco yupo JKT Tanzania, Kagere anaitumikia kwa sasa Namungo na wanaocheza nao kwa sasa timu moja wajifunze nidhamu kwa hao jamaa, Mayele anacheza Pyramids, Mgosi ni kocha msaidizi wa Simba Queens na Tambwe ni meneja wa Singida BS, uwepo wao katika timu hizo utasaidia kuibua vipaji vya wengine.”
Abdul aliyeichezea Yanga kuanzia msimu wa 2012 -2020, akitokea Mtibwa baada ya hapo akaenda kujiunga Indeni ya Zambia (2021) akarejea nchini na kucheza Singida Fountain Gate, amezungumzia nyota wa kizazi cha sasa na kuwataja Pacome Zouzoua wa Yanga aliye na mabao tisa na asisti nane, Feisal Salum ‘Fei Toto’ wa Azam aliye na asisti 13 na kipa wa Simba, Maussa Camara mwenye clean sheet 15.
“Kipindi hiki kuna wachezaji ambao wanafanya vizuri na wamekuwa vipenzi vya mashabiki baadhi yao ni hao niliowataja, ingawa wapo wengi nje ya Simba, Yanga na Azam mfano kipa wa Pamba Jiji, Yona Amos ana clean sheet tisa,” alisema Abdul aliyetwaa ubingwa wa Ligi Kuu akiwa na Yanga katika misimu 2012-2013, 2014-2015, 2015-2016 na 2016-2017.