Kipre Tchetche nitarudi kucheza Tanzania

Muktasari:
Tcheche alijiunga na Azam, 2011 akitokea Jeunesse ya nchini kwao, aliwahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2012/13, akiifungia klabu hiyo mabao17.
Dar es Salaam. Mshambuliaji wa Kedah FA ya Malaysia, Kipré Tchetche ameanza kuyakumbuka maisha ya soka la Tanzania kwa kusema ikitokea nafasi kwa miaka ya mbele anaweza kurejea nchini.
Tcheche mwenye miaka 32, msimu huu wa 2019/20, ameifungia klabu yake mabao matatu katika michezo miwili ya kuwania nafasi ya kucheza Ligi ya Mabingwa Asia.
Nyota huyo wa zamani wa Azam, alisema kuna muda amekuwa akikumbuka namna ambavyo Watanzania walivyokuwa wakimsapoti licha ya kutozichezea klabu za Simba na Yanga ambazo zimekuwa zikitawala soka la Tanzania.
“Msisimko wa Tanzania katika mpira ni mkubwa, nakumbuka vile ambavyo tulikuwa tukishindana, ilikuwa ni Azam, Simba, Yanga na Mtibwa, ambao tulikuwa tukikabana koo katika nafasi nne za juu.
“Naweza kurejea Tanzania kucheza soka, lakini sio kwa sasa. Niliishi vizuri na kila mmoja lakini baada ya kucheza kwa muda mrefu nilipenda kukabiliana na changamoto nyingine za soka kwingine,” alisema mshambuliaji huyo ambaye ni Muivory Coast.
Akizungumzia utofauti wa maisha kwa wachezaji kati ya Tanzania na Malaysia, alisema, “Huku hakuna mambo ya kukaa kambini, wachezaji wamekuwa wakijiongoza wenyewe kwa Tanzania hapakuwa na huo uhuru, ni mara chache kuingia kambini.”
Tcheche alijiunga na Azam, 2011 akitokea Jeunesse ya nchini kwao, aliwahi kuwa mfungaji bora wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu wa 2012/13, akiifungia klabu hiyo mabao17.
Nyota huyo, aliondoka nchini Julai, 2016 baada ya kupata dili la kujiunga na Al-Nahda ya Oman, hakudumu ndani ya klabu hiyo, aliichezea kwa mwaka mmoja, akasajiliwa na Al-Suwaiq ya nchini humo kabla ya kutimkia zake Malaysia anakocheza soka hadi sasa.