KITAYOSCE FC : Wababe wa Lipuli wanaoitamani Azam FC

Muktasari:
Mwanaspoti limekuwa likifuatilia kwa karibu maendeleo ya chama hili, mabosi wake na hata benchi zima la ufundi na hapa tajiri wa chama hili Yusuph Kitumbo, amefunguka mikakati mbalimbali.
KITAYOSCE FC inazidi kubamba kimyakimya. Kwa baadhi ya mashabiki jina hili linaweza kuwa jina geni, lakini kwa wanaofuatilia Ligi Daraja la Pili mbona wanaifahamu vizuri sana shughuli yake.
Chama hilo la mkoani Tabora kwa sasa ndio vinara kwenye Kundi B likiwa na pointi 17 ikiwaacha wapinzani wao, Usalama FC wenye alama 14 baada ya kucheza mechi saba.
Kitayosce imeingia kwenye soka la ushindani katika kipindi kifupi sana, lakini imekuwa maarufu kutokana na shughuli yake uwanjani ikijitofautisha kabisa na klabu nyingine kwenye ligi na hata michuano ya Kombe la FA.
Mwanaspoti limekuwa likifuatilia kwa karibu maendeleo ya chama hili, mabosi wake na hata benchi zima la ufundi na hapa tajiri wa chama hili Yusuph Kitumbo, amefunguka mikakati mbalimbali.
IlIKOTOKA
Tajiri na mmiliki wa klabu hiyo, Kitumbo anaeleza timu hiyo ilinunuliwa Mei, mwaka jana kutoka mkoani Kilimanjaro wakati huo ikiwa imepanda Ligi Daraja la Pili.
Kitayosce ni kifupi cha ‘Kilimajaro Talent Youth Sports Centre’ na baada ya dili la ununuzi kukamilika ikabadili makao yake na kuhamia mkoani Tabora.
“Kwa kushirikiana na wakurugenzi wenzangu tuliinunua kutoka Kilimanjaro na kuihamishia Tabora ambapo, ndipo makao makuu yake kwa sasa,” anasema Kitumbo.
Uamuzi wa kuileta Tabora umelenga kuwapa burudani wakazi wa Tabora ambao, ni wapenzi wakubwa wa soka na wanaisapoti mwanzo mwisho ili kuona inafikia malengo yake.
Hata hivyo, amefichua kuwa wako kwenye harakati za mwisho kabisa kuibadili jina kutoka Kitayosce hadi kuwa Tabora United.
MIKAKATI IKOJE?
Kitumbo anaeleza kwa amshaamsha wanayoifanya huko wanataka kuona wanamaliza Ligi Daraja la Pili wakiwa kileleni mwa msimamo ili kupata nafasi ya kuipandisha Ligi Daraja la Kwanza msimu ujao.
Anasema kama viongozi wamejipanga vyema kutoa sapoti ya kutosha ili kila mmoja ndani ya timu atoe mchango wa kuibeba na hatimaye kufikia malengo.
“Kwa sasa tumejipanga vyema kufikia malengo yetu ya ndani na nje ya uwanja. Tumetenga Sh 102 milioni ambazo zitatumika kwa msimu huu kuiwezesha timu kufanya vizuri kuanzia hatua ya makundi hadi ligi ya mchujo.
“Pia, tuna mipango endelevu kujenga miundombinu na baadaye mwaka huu tumepanga kununua eneo la heka 50 kwa ajili ya kujenga uwanja wa mazoezi na wa mechi kama ulivyo Azam Complex.
“Hapo kutakuwa na kambi kwa ajili ya wachezaji, shughuli za kiofisi na hoteli ya kisasa ambayo tunaweza pia kukodisha klabu nyingine kwa ajili ya kambi,” alisema Kitumbo na kuongeza kwamba,: “Tuko makini na tumenunua basi kwa ajili ya safari za timu kwa maana ya wachezaji na benchi la ufundi.”
KUHUSU USAJILI
Katika kuhakikisha wanapanda daraja la kwanza msimu ujao, Kitumbo amesema wanaendelea kujenga kikosi imara kwa kuwasajili wachezaji wenye uzoefu, vipaji na wapambanaji uwanjani.
Benchi la ufundi la klabu hiyo, linaongozwa na Kocha Waziri Mahadhi, ambaye ni staa wa zamani wa Yanga akisaidiwa na Boniface Kiwale.
“Tuna kikosi kipana na benchi la ufundi imara, wachezaji wengi wana uzoefu, lakini tumewapa majukumu walimu wetu ambao wamecheza na wanajua kutengeneza timu ya ushindani,” alisema Kitumbo.
MAAJABU
Timu hii mbali na kuwa changa, lakini uwanjani inauwasha moto sio kitoto kwani, mpaka sasa imecheza mechi saba na kushinda tano na sare mbili ikiwa haijapoteza.
Kama haitoshi, Kitayosce imedhihirisha ubora kwenye Kombe la FA kwa kuzitoa timu kadhaa zikiwamo za Ligi Kuu Bara, ambapo imetinga hatua ya 16 bora kwa kuichapa Lipuli FC.
Katika mchezo huo ambao ulipigwa mkoani Iringa, Lipuli ikiwa nyumbani ililazimishwa sare ya mabao 2-2 ndani ya dakika 90 kabla ya kukubali mabao 5-4 kwa mikwaju ya penalti na kutupwa nje ya michuano hiyo.
Kwa matokeo hayo, yaliifanya timu hiyo ya Ligi Daraja la Pili kufuzu hatua ya 16 bora na sasa inajipanga kuikabili Ndanda FC kule Nangwanda Sijaona, Mtwara.
Kwa upande wake, Kocha Msaidizi Kiwale anasema mwenendo wao upo vizuri na wamejipanga ili kufikia malengo na kamwe hawatabweteka na matokeo wanayopata.
“Bado tuna mechi nyingi za ligi ambazo tumepanga kufanya vizuri, lakini kuna mchezo wa mtoano dhidi ya Ndanda wa Kombe la FA, michezo yote tunaitazama kwa jicho la tatu kuhakikisha tunapata matokeo mazuri na kuweza kusonga mbele,” anasema Kiwale.
Kiwale, ambaye amepata uzoefu mkubwa wa mchezo wa sok baada ya kuzifundisha klabu za Mshikamano, Abajalo FC na Geita Gold anafichua kuwa, kwa uzoefu wa benchi la ufundi na wachezaji ni lazima watatoboa kwenye mashindano yote wayakayokabiliana nayo.