Prime
Kivuli cha Yanga chatua Chamazi
WAKATI Yanga ikiendelea kupiga hesabu kali za kusajili winga wa kigeni, kwa upande wa mawinga wa ndani macho ya mabosi wa klabu hiyo yako kwa Idd Seleman ‘Nado’ ambaye mkataba wake na Azam FC unamalizika msimu huu.
Unaweza kusema kwenye suala la usajili msimu huu Yanga imeamua kuivamia Azam hasa upande wa mawinga, kwani matajiri hao wa Chamazi walitua DR Congo ndani ya FC Lupopo kumsaka Henock Molia. Ghafla Yanga nao pia wakatua hapohapo.
Azam imeshaanza hesabu za kuongeza nguvu msimu ujao na kwa kuanza walienda DR Congo kusaka winga, lakini Yanga nao wakatua kumtaka mchezaji huyo huyo tena wakiweka dau kubwa zaidi.
Mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Bara, kwa sasa wamehamia kwa Idd Nado, winga ambaye ameitumikia Azam FC kwa misimu saba mfululizo akitoka Mbeya City mwaka 2019.
Nado ambaye mkataba wake unamalizika msimu huu, amekuwa na mazungumzo na mabosi zake lakini bado hajafikia uamuzi wa mwisho kusaini kandarasi ya kuendelea kuwatumikia matajiri hao wa Chamazi.
Winga huyo anayekiwasha timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, amekuwa na kiwango bora wakati wote, huku msimu huu akiendelea kuonyesha ubabe wake mbele ya kocha Florent Ibenge kwa kufanya vizuri hali iliyomuwezesha kupangwa kikosi cha kwanza takribani mechi zote.
Ni mara chache kwa Azam kutua uwanjani halafu Nado asicheze kikosi cha kwanza, kwani msimu huu katika mechi 25 ambazo Azam imecheza amekosekana kwenye michezo sita pekee, huku akiweka rekodi ya kufunga mabao manane.
Taarifa za ndani kutoka Yanga zililiambia Mwanaspoti, klabu hiyo inasaka winga wa kigeni lakini kwa nafasi ya mawinga wa ndani wametua kwa Idd Seleman ‘Nado’.
“Nado amependekezwa na Moallin (Abdihamid) akiwaambia mabosi wa Yanga kwamba ni mchezaji aliyekomaa akili na kwamba wakati huu bado hajakubali kuongeza mkataba Azam ndio muda mzuri wa kumchukua,” kilisema chanzo.
Kama Yanga itafanikiwa kunasa saini ya winga huyo basi ana nafasi nzuri ya kucheza kwenye kikosi hicho kwani wachezaji wazawa wako wachache, huku baadhi yao wakielekea kumaliza mikataba yao akiwemo Farid Mussa.
Mawinga wengine wazawa ndani ya Yanga ni Denis Nkane na Offen Chikola waliotolewa kwa mkopo dirisha la Januari 2026, huku Edmund John akibaki kukiwasha.
Yanga kwa sasa inapambana kumaliza ligi kutetea taji lao ambapo inaongoza msimamo kwa pointi 60, ikifuatiwa na Simba yenye 58 na Azam 52, zote zikicheza mechi 25, bado tano kumaliza msimu