Kocha afichua jambo KenGold

Muktasari:
- KenGold imerudi Championship baada ya kupanda msimu huu na kushindwa kuonja nafasi nzuri katika msimamo, kwani tangu imepanda hadi inashuka ilikuwa nafasi ya mwisho.
BAADA ya KenGold kushuka Ligi Kuu ikiwa na mechi tatu mkononi, kocha Omary Kapilima ametaja mambo mawili yaliyowaangusha, huku akisisitiza wanajipanga kurudi msimu ujao.
KenGold imerudi Championship baada ya kupanda msimu huu na kushindwa kuonja nafasi nzuri katika msimamo, kwani tangu imepanda hadi inashuka ilikuwa nafasi ya mwisho.
Akizungumza na Mwanaspoti, Kapilima alisema wameangushwa na ugumu wa ligi na pia usajili mbaya wa mzunguko wa kwanza ambao waliamini kikosi kilichowapandisha kingeonyesha ushindani.
“Tumepigwa na kitu kizito... tumekutana na ligi ngumu tofauti na matarajio. Pia kutoongeza nguvu mara baada ya timu kupanda daraja kwa kuchanganya nyota wazoefu na damu changa. Hizi zinaweza kuwa sababu za kushindwa kuendana na kasi tuliyoikuta,” alisema beki huyo wa zamani wa Majimaji, Yanga, Mtibwa Sugar na Taifa Stars.
“Tulikuwa na wachezaji wengi ambao hawana uzoefu wa kutosha tukiwaamini kutokana na kuipandisha daraja timu na tumekumbuka shuka wakati kumekucha tuliposajili wengi dirisha dogo.”
Kapilima alisema kikosi kimeonyesha mabadiliko baada ya usajili walioufanya wakijaza nyota wengi wakongwe na wazoefu wa ligi.
“Viongozi wamefanya kilichokuwa kinatakiwa mzunguko wa pili, wameipambania timu ili iweze kubaki msimu ujao lakini mambo yalikuwa magumu kwa sababu mzunguko wa kwanza mara nyingi ndio unatumika kukusanya pointi na kujihakikishia nafasi huku wa pili ni kulinda nafasi sisi ndio tulikuwa tunapambana kubaki.”
Kapilima alisema bado hawajamaliza msimu licha ya kushuka daraja wakiwa na mechi mkononi watapambana kujipanga upya kwa Ligi ya Championship.
KenGold imeshuka daraja baada ya kucheza mechi 27 ikishinda tatu pekee, sare saba na vipigo 17 imefungwa mabao 50, ikifunga 22 na kukusanya pointi 16.