Kocha Aykhan Farzukh amtabiria makubwa Mabula

Muktasari:
- Mabula amejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Serbia alikokuwa na FK Spartak Subotica ya Ligi Kuu ya huko maarufu kama Serbian SuperLiga.
KOCHA Aykhan Farzukh wa timu ya Shamakhi FK anayoitumikia Mtanzania Alphonce Mabula amemtaja staa huyo kama kiungo atakayekuja kufanya makubwa kwani bado umri unamruhusu.
Mabula amejiunga na timu hiyo msimu huu akitokea Serbia alikokuwa na FK Spartak Subotica ya Ligi Kuu ya huko maarufu kama Serbian SuperLiga.
Chama hilo linashiriki Ligi Kuu ya Azerbaijan na Mabula amejiunga kwa mkataba wa miezi sita wenye kipengele cha kuongeza mwaka mmoja.
Akizungumza na chombo kimoja cha habari nchini humo, Farzukh alisema nyota huyo ana jitihada binafsi na cha zaidi anatumia miguu yote miwili kwa usahihi.
"Ninaona kipaji kikubwa kwa Mabula, kama ataendelea hivi katika siku zijazo ninaamini atakuwa mmoja wa wachezaji bora wa kizazi hiki," alisema kocha huyo.
"Changamoto kubwa kwake hasa ni namna ya kutoa pasi za mbele na tumekuwa tukilifanyia kazi mazoezini."
Kiungo huyo wa chini hadi sasa amecheza mechi 11 tangu ajiunge na timu hiyo akifunga bao moja.