Kocha JKT Tanzania apiga hesabu kali

Muktasari:
- Kocha Ally alisema pointi walizonazo kwa sasa bado haziwapi dhamana ya kuendelea kusalia katika Ligi Kuu, hivyo anajipanga na wachezaji kuona kila mchezo wanautumia vyema kuvuna pointi tatu ili hadi mwisho wa msimu wasalie katika ligi kwa msimu ujao na hata kuingia 5 Bora.
MAAFANDE wa JKT Tanzania, wapo katika nafasi ya saba kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara wakikusanya pointi 32 kupitia mechi 25, huku kocha wa timu hiyo, Ahmad Ally akipiga hesabu kali kwa mechi za tano zilizosalia ili kuhakikisha wanavuna pointi za kutosha zitakazowaacha salama.
Kocha Ally alisema pointi walizonazo kwa sasa bado haziwapi dhamana ya kuendelea kusalia katika Ligi Kuu, hivyo anajipanga na wachezaji kuona kila mchezo wanautumia vyema kuvuna pointi tatu ili hadi mwisho wa msimu wasalie katika ligi kwa msimu ujao na hata kuingia 5 Bora.
Akifafanua kauli iyo, kocha huyo alisema kwa hali ya sasa ni makocha kutumia mbinu kushinda mechi kuliko ufundi mwingi uwanjani ambao hautakuwa na msaada kwa kipindi hicho.
Dhidi ya wapinzani iliobaki kuwakabili, raundi ya kwanza zilipokutana JKT ilifungwa 1-0 na Simba, kabla ya kushinda 1-0 dhidi ya Fountain Gate na (1-0 vs) TZ Prisons, huku ikitoka suluhu na timu za Pamba Jiji na Mashujaa.
“Tuna hesabu za kumaliza nafasi ya 5.”
“Ufundi upo lakini siyo jambo unaloweza ukalitegemea sana katika mechi hizi za mwisho, labda itategemea na mechi yenyewe uwe umeshinda mabao mengi, nje na hapo mchezo ukiwa mgumu lazima mbinu zitahusika zaidi,” alisema kocha Ally.
Katika mechi 25 ilizocheza hadi sasa maafande hao wameshinda michezo saba, wamepata sare 11 na kupoteza saba, wakifunga pia mabao 22 na kufungwa 21 na kumiliki pointi 32.