Kocha mpya Yanga aleta fomesheni ya Barcelona

Benchi hilo linataka timu hiyo kuanzia sasa icheze soka la maana kama lile la Barcelona ya Ligi Kuu Hispania.
Muktasari:
- Kocha Msaidizi mpya wa Yanga, Boniface Mkwasa, ametamba kuwa wana wachezaji wenye viwango vya kucheza mfumo huo na anataka timu ifanye majukumu yote kwa pamoja tofauti na awali ambapo timu ilikuwa ikitumia mifumo anayosema inasababisha timu kukatika uwanjani.
WAKATI washambuliaji Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza wakitarajiwa kuwasili Dar es Salaam jana Jumapili jioni, benchi jipya la ufundi la Yanga limeingia na mambo mapya.
Benchi hilo linataka timu hiyo kuanzia sasa icheze soka la maana kama lile la Barcelona ya Ligi Kuu Hispania. Soka hilo ni la pasi nyingi fupi fupi na kupandisha mashambulizi ya kasi kwa pamoja.
Kocha Msaidizi mpya wa Yanga, Boniface Mkwasa, ametamba kuwa wana wachezaji wenye viwango vya kucheza mfumo huo na anataka timu ifanye majukumu yote kwa pamoja tofauti na awali ambapo timu ilikuwa ikitumia mifumo anayosema inasababisha timu kukatika uwanjani.
Benchi lililopita chini ya Mholanzi, Ernest Brandts, lilikuwa linapenda kutumia mfumo wa 4-4-2, lakini kwa mfumo wa sasa wa makocha hao Yanga itakuwa ikicheza 4-3-3 ambao ni wa soka la kasi.
Mkwasa ambaye anasubiri kuletewa bosi, amesema hata akija kocha mkuu anayetarajiwa mzungu, atamshawishi waendeleze mfumo huo kwa vile ni wa kisasa na wana vijana wa kufanya kazi hiyo.
Ameanza kuufundisha uchezaji huo katika mazoezi ya juzi Jumamosi asubuhi kwenye Uwanja wa Bora, Kijitonyama jijini Dar es Salaam ili kuhakikisha wachezaji wanaushika mapema.
Mkwasa alisema kuwa mfumo huo ni wakushambulia timu nzima kwa kuanzia mabeki, viungo na washambuliaji ambao anaamini utaipa mafanikio.
“Ipo mifumo mingi ya ufundishaji ya Uingereza, Ujerumani na mingine mingi, lakini kwa kuanza kuifundisha Yanga nitaanza na mfumo wa Hispania. Mfumo huu ninaamini utatupa mafanikio katika kupata ushindi popote pale, hata kama akija kocha wetu mpya nitamtaarifu mfumo ninaoutumia katika timu, kama akiukubali basi tutaendelea nao huo katika ligi na mashindano mengine,”alisisitiza Mkwasa ambaye amefanya tathmini ya kina kuhusiana na rekodi na utendaji wa timu hiyo na kuamua kuwafungia kazi mabeki.
“Kikubwa ninataka timu icheze kitimu kwa kushambulia na kukaba kuanzia mabeki, viungo na washambuliaji ndani ya uwanja.”
Mkwasa ameanza kuimarisha safu hiyo ili kuwakomesha washambuliaji wakorofi wa timu pinzani kama vile Mrundi Amissi Tambwe, Betram Mwombeki (wote Simba) pamoja na Muivory Coast wa Azam FC, Kipre Tchetche, wasipate mwanya wa kuwafunga mabao.
Mkwasa ambaye ni beki wa kati wa zamani wa Yanga, anazijua vizuri mbinu za ulinzi na ametamka kuwa ameanza kazi ya kuimarisha safu hiyo pamoja na kuwaweka fiti na ukakamavu kwanza, baadaye ndiyo ushambuliaji na mambo mengine yatafuata. Alisema safu ya ushambuliaji haina mapungufu sana na matatizo yao yapo kwenye pasi za mwishoni.
Kocha huyo amehakikisha mabeki wote wapo mazoezini, mabeki hao ni Kelvin Yondani ‘Vidic’, Mnyarwanda Mbuyu Twite, Oscar Joshua, David Luhende, Rajab Zahir, Hassan Dilunga na Issa Ngao isipokuwa nahodha, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye anauguza goti la kulia.
“Tumeanza na ulinzi kwa sababu ndiko kwenye msingi wa timu, unapoanza kujenga nyumba lazima uanze na msingi, baadaye ndiyo tutaendelea na kwingine,” alisema.
“Nawapa mbinu za namna ya kuzuia, nawasimamisha wanapokosea na kuwaelekeza cha kufanya. Hali siyo mbaya mambo ni mazuri, baada ya muda tutakuwa vizuri zaidi.
“Nataka kuona hakuna makosa ambayo yalikuwa yakitokea huko nyuma ambayo kuna wakati ulikuwa unaona umakini unapungua na kusababisha timu inafungwa mabao ya kizembe, nikimaliza eneo hilo nitakuja katika safu ya kiungo ambako nako kazi ya ukabaji na kupatikana kwa pasi za mwisho nataka kuona inafanyika kwa ufanisi, ukiangalia sasa hakuna pasi ambazo zitazalisha mabao mengi.
“Nataka kuona kama kwenye mechi tunapata nafasi tano basi tunazitumia zote au kama ikitokea tukapoteza basi iwe moja, kikubwa ni umakini na wachezaji wa kufanya kazi hiyo nasisitiza wapo wengi hapa kwa usajili ambao umefanywa.”
Kuhusu ratiba ya mazoezi, Mkwasa alisema huenda Yanga ikahamia Uwanja wa Tanganyika Packers, Kawe na anapenda timu hiyo ifanye mazoezi jioni kwa sababu ndio muda ambao mechi za Ligi Kuu Bara pamoja mashindano mengine huchezwa.