Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Miamba ya soka kuitikisa dunia

Kipute cha mwaka

Muktasari:

Si hizo tu kesho Jumatano usiku Manchester United itacheza na Olympiacos huku Borussia Dortmund ikiikabili Zenit St. Petersburg. Lakini kabla hujakaa kwenye runinga yako usiku kuangalia mambo ya Ulaya, majira ya saa 10 kwenye Uwanja wa Taifa kuna kasheshe jingine, wababe wawili Yanga na Azam wanapambana kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara.

NDANI ya saa 48 Duniani kuna mechi tano muhimu ambazo ni pata potea. Ushinde ubaki au ufungwe ile kwako. Kuna mechi mbili kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya leo usiku Chelsea itarudiana na Galatasaray huku Real Madrid ikikwaana na FC Schalke 04.

Si hizo tu kesho Jumatano usiku Manchester United itacheza na Olympiacos huku Borussia Dortmund ikiikabili Zenit St. Petersburg. Lakini kabla hujakaa kwenye runinga yako usiku kuangalia mambo ya Ulaya, majira ya saa 10 kwenye Uwanja wa Taifa kuna kasheshe jingine, wababe wawili Yanga na Azam wanapambana kwenye mechi ya Ligi Kuu Bara.

Kocha wa Yanga, Hans Pluijm amewaambia wachezaji wake kauli moja tu; “Muishinde Azam au mpoteze ubingwa.” Bosi huyo ambaye timu yake inashikilia nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 39, nyuma ya Azam yenye pointi 43 amewaambia wachezaji wake wachague moja. Jambo ambalo litafanya mchezo huo uwe na utamu wa aina yake.

Wakati Pluijm akitangaza ushindi katika mechi hiyo, wapinzani wao Azam nao wamesema watahakikisha wanaifunga Yanga ili kujikita zaidi kileleni kwenye msimamo wa ligi hiyo na kuziacha mbali Yanga na Mbeya City.

“Mchezo dhidi ya Azam ni lazima tushinde kama tunahitaji ubingwa msimu huu, tusiposhinda mechi ya kesho ni dhahiri kuwa tutajiweka kwenye nafasi ngumu zaidi.

“Sifahamu rekodi za mechi kati ya Yanga na Azam ila nimewaona Azam mara moja kwenye ya Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya Ferreviario Da Beira, ni timu nzuri na ninategemea ushindani mkubwa japo ni lazima tushinde mechi hiyo,” alisema Pluijm ambaye ameanza kuinoa Yanga mwezi Januari mwaka huu.

Manahodha

Nahodha wa Yanga Nadir Haroub ‘Canavaro’ alisema; “Mechi itakuwa ngumu sana kwetu kwani mchezo uliopita hatukuwa na matokeo mazuri, Azam wao walishinda mechi yao lakini tunaamini tutafanya vizuri kuhakikisha tunashinda kwani lengo letu pia ni kutetea ubingwa.”

Nahodha msaidizi wa Azam, Himid Mao alisema kuwa: “Ni mchezo muhimu kwetu kushinda ukizingatia tunafukuzana katika mbio za kutwaa ubingwa, hivyo ni lazima tuhakikishe tunashinda.”

Kocha Omog

Kocha wa Azam, Joseph Omog alisema; “Tuna kila sababu ya kuwafunga Yanga, tuna kila kitu, kwa upande wangu nimeandaa timu vizuri kiufundi kuhakikisha tunashinda.”

Kocha msaidizi na mchezaji wa zamani wa kikosi hicho, Mkenya Ibrahim Shikanda alisema: “Naijua vizuri ligi ya Tanzania, Yanga ni nzuri ni moja ya timu bora kwenye ligi, kwanza wana wachezaji wazoefu, lakini kiufundi ni wazuri na zaidi kwenye safu ya ushambuliaji.”

“Wana washambuliaji wazuri ambao kama beki haiko vizuri mtawatambua, wana kasi na zaidi mashambulizi yao wanafanya kupitia pembeni ambako kuna wachezaji wenye kasi sana kama wakina Simon Msuva,”alisema Shikanda.

“Hatuna wasiwasi sana na safu ya ulinzi kwa sababu ni wachezaji walewale, kikubwa tumejiandaa kwa kila kitu kuhakikisha tunashinda,”aliongeza.

Straika wao, John Bocco ‘Adebayor’ ametamka kuwa, anataka kuwafunga Yanga kwenye mechi hiyo: “Mimi ni straika kazi yangu ni kufunga mabao tu, hayo ndiyo malengo yangu na nitajitahidi kadri niwezavyo na namwomba Mungu anisaidie, nitawafunga tu.”

Rekodi zao

Azam na Yanga zimekutana mara 11 kwenye mechi za Ligi Kuu Bara tangu mwaka 2009 huku kila timu ikiibuka na ushindi mara nne na kutoka sare mara tatu.

Katika mechi hizo walizokutana kumekua na rekodi ya aina yake katika idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa kwani kila timu imefunga mabao 14.

Yanga watakua na kazi moja hiyo kesho ya kuvunja rekodi ya Azam kucheza michezo 19 ya ligi msimu huu bila kupoteza mchezo hata mmoja. Azam imeshinda mechi 12 na kutoka sare saba huku Yanga ikishinda mechi 11 imepata sare 6 na kupoteza mchezo mmoja. Yanga ilifungwa na Azam 3-2 kwenye mechi ya mzunguko wa kwanza wa ligi msimu huu.

Tchetche apania

Straika mwenye uchu wa mabao wa Azam FC raia wa Ivory Coastal, Kipre Tchetche alisema: “Tunataka rekodi mbili katika msimu huu wa Ligi Kuu, kuwafunga Yanga mara mbili , pia kuchukua ubingwa kwa mara ya kwanza baada ya muda mrefu tena bila kupoteza mchezo.”

Beki wa kati kisiki, Aggrey Moris alisema: “Siyo mechi nyepesi kwetu kupata ushindi, kikubwa kinachohitajika ni kuhakikisha tunacheza kwa bidii na kujituma.”

Niyonzima na Ngassa

Kiungo Haruna Niyonzima na mshambuliaji Mrisho Ngassa wa Yanga, jana jioni walianza mazoezi na timu hiyo baada ya kuwa nje kwa wiki moja.

Daktari wa Yanga, Juma Sufiani alithibitisha kwamba wako tayari kwa mchezo.

Vikosi Yanga: Juma Kaseja, Mbuyu Twite, Oscar Joshua, Cannavaro, Kelvin Yondani, Frank Domayo, Msuva, Niyonzima, Emmanuel Okwi, Ngassa na Hamis Kiiza.

Azam FC; Mwadini Ally, Mao, Erasto Nyoni, Said Morad, Moris, Kipre Balou, Hamis Mcha, Salum Abubakari ‘Sure Boy’, Bocco, Tchetche na Brian Umony.