Minziro: Ni ‘do or die’ dhidi ya Tabora United

Muktasari:
- Pamba Jiji inashika nafasi ya 13 kwenye msimamo wa ligi ikiwa imevuna alama 23 katika michezo 24, huku ikishinda mitano, sare nane na kupoteza 11, imefunga mabao 15 na kuruhusu 26.
Baada ya kuambulia sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya Namungo FC katika mchezo uliopita kwenye Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza, Kocha Mkuu wa Pamba Jiji, Fredy Felix ‘Minziro’ amesema kesho ni kufa au kupona watakapocheza dhidi ya Tabora United.
Mchezo huo wa raundi ya 25 Ligi Kuu Bara utachezwa kuanzia saa 8:00 mchana katika Uwanja wa CCM Kirumba, ambapo mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa Ali Hassan Mwinyi mjini Tabora wenyeji walipata ushindi wa bao 1-0.
Akizungumzia maandalizi ya kikosi chake leo Ijumaa Aprili 4, 2025 kwenye mkutano na waandishi wa habari jijini Mwanza, Minziro amesema mchezo uliopita waliwaangusha mashabiki wao hivyo hawana kisingizio chochote kwenye mchezo wa kesho lazima wapambane kufa kupona kuwapa furaha.
Amesema baada ya mchezo huo benchi lake limejaribu kufanya baadhi ya masahihisho kujiandaa na mchezo wa kesho huku akitamba kuwa maandalizi mpaka sasa yamekwenda vizuri.
“Jambo la muhimu ni kwamba sisi tuko nyumbani mechi ya juzi hatukupata matokeo mazuri lakini hii ya kesho tumejipanga kuhakikisha tunaingia Do or Die kupata alama tatu hakuna maongezi mengi zaidi ya hilo,” amesema Minziro.
Ameongeza: “Tunajua tunakutana na timu ambayo ni nzuri iko juu haina presha kama sisi wengine ambao tuko chini tunafahamu kwamba tunakutana na timu ya aina gani. Ligi imekuwa ngumu kwa timu ambazo bado ziko chini kila mmoja anapambana kuhakikisha anatoka chini kwenda juu.”
Minziro amesema mchezo wa kesho ni miongoni mwa michezo mitano ya nyumbani ya kimkakati wanayohitaji kwa udi na uvumba ushindi kwani utakuwa mchezo wa pili baada ya ule wa Namungo, hivyo, hawahitaji tena kuharibu mipango kwa kupata matokeo mabaya.
“Fatiki imekuwa kubwa kutokana na tunacheza mfululizo ratiba iko hivyo mpaka Aprili 8, 2025 tunacheza hivyo kila baada ya siku mbili tunacheza mechi, kwahiyo plan ambayo tutaingia nayo kesho tunategemea kupata matokeo mazuri,” amesema Minziro.
Mchezaji wa Pamba Jiji, Abal Kassim amesema wachezaji, viongozi na walimu wanajilaumu kwa kutopata ushindi katika mchezo uliopita jambo ambalo hawataki lijirudie kwenye mchezo wa kesho dhidi ya Tabora United.
“Sisi wachezaji tumejiandaa vizuri kutokana na matokeo ya mchezo uliopita hata kama tulipata sare lakini kwa upande wetu ni kama tulipoteza kwahiyo tumejiandaa vizuri kupata matokeo mazuri ambayo yatatusogeza kutoka pale tulipo,” amesema Kassim.