Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Mpaka kieleweke

Yanga ilipata bao la kuongoza dakika ya 14 kupitia kwa straika wake Mrundi, Didier Kavumbagu, aliyemalizia mpira uliowababatiza mabeki wa Azam FC wakati wanaokoa shuti la fowadi mwenye nguvu Hamis Kiiza.PICHA|MAKTABA

Muktasari:

Yanga ilipata bao la kuongoza dakika ya 14 kupitia kwa straika wake Mrundi, Didier Kavumbagu, aliyemalizia mpira uliowababatiza mabeki wa Azam FC wakati wanaokoa shuti la fowadi mwenye nguvu Hamis Kiiza.

VITA ya Azam na Yanga kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara imefikia patamu baada ya timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 jana Jumatano katika mechi iliyofanyika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ambayo ilikumbwa na tukio la huzuni baada ya shabiki mmoja wa Jangwani kufariki dunia uwanjani hapo.

Yanga ambayo ni mabingwa watetezi, kwa matokeo hayo imefikisha pointi 40 na kusalia nafasi ya pili huku Azam ikifikisha 44 na kuzidi kujikita kileleni ikionekana kusisitiza kwamba haitulii mpaka itwae ubingwa wake wa kwanza la ligi hiyo.

Lakini Yanga baada ya kusikia tambo hizo, imeapa kwamba itapambana mpaka kieleweke katika mechi zake za nyumbani na ugenini zilizosalia kuhakikisha inalinda heshima yake na kupata tiketi ya kurejea kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.

Awali kocha wa Yanga, Hans van Pluijm, alikuwa amewaambia wachezaji wake kwamba wasikubali kwa vyovyote kuiachia Azam pointi tatu akisema litakuwa kosa kubwa kwao. Lakini mpinzaniwake, Joseph Omog wa Azam alipoingia vyumbani wakati wa mapumziko huku Yanga ikiwa mbele, aliwaambia wachezaji wake kwamba wakomae na wasiipe Yanga nafasi ya kutawala mchezo.

Yanga ilipata bao la kuongoza dakika ya 14 kupitia kwa straika wake Mrundi, Didier Kavumbagu, aliyemalizia mpira uliowababatiza mabeki wa Azam FC wakati wanaokoa shuti la fowadi mwenye nguvu Hamis Kiiza.

Azam ambayo ni klabu pekee Afrika Mashariki inayomiliki uwanja wake binafsi unaotambuliwa na Shirikisho la Soka la Afrika (CAF), ilisawazisha dakika ya 83 kwa shuti la Kelvin Friday aliyeunganisha pasi safi ya Aboubakary Salum ‘Sure Boy’. Friday aliingia kipindi cha pili kuchukua nafasi ya Khamis Mcha.

Kocha wa Yanga hakuridhika na ushindi huo, lakini akasema:

“Tulifanya makosa na wakayatumia, lakini ni mchezo. Bado tuna nafasi ya kutetea ubingwa wetu kwa matokeo haya.”

Naye Omog alisema: “Yanga ilitawala kiungo kipindi cha kwanza, lakini dakika 45 za mwisho tukawabadilikia, tukawakamata. Kwa matokeo haya ya sare bado tunaendelea kuongoza msimamo na nafasi ya ubingwa tunayo, sina wasiwasi.”

Nadir Haroub ‘Cannavaro’ ambaye ni nahodha wa Yanga, alisema:

“Tunashukuru kwa hii sare, lakini haikuwa dhamira yetu, tulitaka ushindi.”

John Bocco wa Azam ambaye amekuwa na rekodi za kumfunga mara nyingi kipa wa Yanga, Juma Kaseja ila jana alichemsha.

Katika mchezo huo, Yanga ilionekana kuwa na kasi zaidi ikiwatumia viungo wake na washambuliaji wenye kasi; Hamis Kiiza, Emmanuel Okwi na Simon Msuva katika kulishambulia goli la wapinzani wao hususani kipindi cha kwanza.

Lakini safu ya ulinzi ya Azam inayoongozwa na Said Morad na David Mwantika, iliwadhibiti licha ya kwamba Morad alibabaika dakika 70 baada ya mpira wa Kavumbagu kumgonga mkononi na Yanga kupewa penalti iliyopigwa na Kiiza ambaye alikosa. Kipa Aishi Manula aliipangua na mabeki wakaosha.

Dakika ya 20 ya mchezo huo mshambuliaji wa kigeni, Kipre Tchetche, alikwamisha mpira wavuni lakini mwamuzi wa kati, Hashimu Abdallah alikataa kutokana na kumwangusha beki wa pembeni wa Yanga, Juma Abdul nje kidogo ya 18.

Dakika moja baadaye, Tchetche, alipiga shuti kali nje ya 18 na mpira kugonga mwamba kabla ya kurudi uwanjani kisha kuokolewa na mabeki wa Yanga. Tchetche alifanya hivyo akitumia vyema mpira wa kona uliopigwa na kiungo mshambuliaji wa Azam, Khamis Mcha.

Beki wa Azam, Erasto Nyoni, alionyeshwa kadi ya njano dakika 24 kwa kumchezea vibaya Okwi. Katika ya dakika ya 33 Kavumbagu aliwaduwaza mashabiki baada ya kushindwa kuunganisha mpira wa kona uliopigwa na Msuva kabla ya mabeki wa Azam kuokoa.

Hadi timu hizo zinakwenda mapumziko Tchetche alipiga mashuti mengi yaliyowababatiza mabeki wa Yanga, Nadir Haroub ‘Cannavaro’ na Kelvin Yondani ambao walikuwa ngangari na kutumia zaidi uzoefu kuokoa jahazi.

Kipindi cha pili mpira ulichelewa kuanza baada ya nyavu za goli walilokuwa wanalitumia Yanga kulegea, hivyo kufanyiwa marekebisho kwa zaidi ya dakika 10. Dakika ya 51, Friday wa Azam

FC aliyeingia kuchukua nafasi ya Mcha alishindwa kuunganisha krosi hafifu iliyopigwa na Tchetche akiwa amebaki yeye na goli.

Katika mchezo huo, mabeki wa Azam walionekana kubabaika jinsi ya kumkaba Okwi ambaye wakati fulani alikuwa akipiga krosi zenye macho.

Nyoni alionyeshwa kadi ya pili ya njano na kuwa nyekundu katika dakika 71 baada ya kuzozana na wachezaji wa Yanga wakati akisubiri kona.

Katika mchezo huo, Kavumbagu alitoka na nafasi yake kuchukuliwa na Mrisho Ngassa huku Kiiza naye alitolewa dakika za majeruhi na nafasi yake kuchukuliwa na Hussein Javu ambaye amekuwa akisota benchi.

Rekodi zao

Azam na Yanga zimekutana mara 12 kwenye mechi za Ligi Kuu Bara tangu mwaka 2009 huku kila timu ikiibuka na ushindi mara nne na kutoka sare mara nne.

Katika mechi hizo walizokutana kumekua na rekodi ya aina yake katika idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa kwani kila timu imefunga mabao 15.

Yanga;

Juma Kaseja, Juma Abdul, Oscar Joshua, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Kelvin Yondani, Frank Domayo, Simon Msuva, Hassan Dilunga, Didier Kavumbagu, Hamis Kiiza na Emmanuel Okwi.

Azam FC;

Aishi Manula, Erasto Nyoni, Gadier Michael, Said Morad, David Mwantika, Balou Michael, Himid Mao, Salum Abubakari ‘Sure Boy’, John Bocco, Kipre Tchetche na Khamis Mcha.

Bao la Kavumbagu laua

Wakati huohuo, mtu mmoja anayeaminika kuwa ni shabiki wa Yanga, Deodatus Mwakyangula, alifariki dunia wakati akiwa jukwaani wakati akishuhudia mchezo huo.

Mwakyangula, mwenye umri wa miaka 48, ambaye ni mkazi wa Kipunguni A jijini Dar es Salaam, pia ni Meneja wa Baa ya Rose Hill inadhaniwa kifo chake kimetokana na kuzidiwa na furaha ya bao la straika, Didier Kavumbagu.

Daktari Mkuu wa Kitengo cha Huduma ya Kwanza cha Uwanja wa Taifa, Nassor Matuzya, alithibitisha kifo hicho. Alisema Mwakyangula alianza kujisikia vibaya wakati akishangilia bao hilo na walipompeleka kwenye vyumba vya huduma ya kwanza vya uwanjani hapo kwa ajili ya matibabu ndipo alipofariki.

Alisema baada ya vipimo kuonyesha hivyo, waliuchukua mwili wake kuupeleka Hospitali ya Temeke.

Mke wa marehemu, Rose Lusinde, ambaye pia alikuwapo uwanjani hapo alisikika akilia na kulalamika: “Maskini jamani, bao la Kavumbagu linamuua mume wangu.”

Rose ameelezwa kuwa ni askari wa Jeshi la Magereza.