Hello

Your subscription is almost coming to an end. Don’t miss out on the great content on Nation.Africa

Ready to continue your informative journey with us?

Hello

Your premium access has ended, but the best of Nation.Africa is still within reach. Renew now to unlock exclusive stories and in-depth features.

Reclaim your full access. Click below to renew.

Namungo yavunja mwiko wa dakika 270

NAMUNGO Pict

Muktasari:

  • Tangu Mashujaa FC ipande daraja kucheza Ligi Kuu Bara msimu wa 2022-23, ilikuwa haijawahi kupoteza mchezo wa michuano hiyo dhidi ya Namungo, kabla ya Jumapili iliyopita kukutana na mshangao.

USHINDI wa mabao 2-1 ilioupata Namungo dhidi ya Mashujaa katika mchezo wa Ligi Kuu Bara, umeifanya timu hiyo kuvunja mwiko wa dakika 270 na kushinda kwa mara ya kwanza dhidi ya wapinzani wao hao baada ya kushindwa kufanya hivyo katika mechi tatu zilizopita.

Tangu Mashujaa FC ipande daraja kucheza Ligi Kuu Bara msimu wa 2022-23, ilikuwa haijawahi kupoteza mchezo wa michuano hiyo dhidi ya Namungo, kabla ya Jumapili iliyopita kukutana na mshangao.

Mara ya kwanza katika ligi timu hizo zilikutana Septemba 30, 2023 ambapo zilitoka 0-0, huku mchezo wa pili uliopigwa Machi 2, 2024, Mashujaa ilishinda bao 1-0 lililofungwa na Adam Adam.

Mchezo wa tatu kukutana ulikuwa wa msimu huu duru la kwanza uliopigwa Novemba 23, 2024 kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika mjini Kigoma, ambapo wenyeji Mashujaa walishinda bao 1-0 kupitia Abrahaman Mussa.

Kitendo cha kuchapwa michezo miwili huku mmoja ikitoka suluhu, kikaifanya Namungo kuvunja uteja katika mchezo wa nne uliopigwa kwenye Uwanja wa Majaliwa mkoani Lindi, kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-1, Aprili 20, 2025.

Katika mchezo huo, Mashujaa ilipata bao la dakika ya 25 lililofungwa kwa mkwaju wa penalti na Jaffary Kibaya, lilidumu kwa dakika tatu, baada ya Mrundi Derrick Mukombozi kuisawazishia Namungo katika dakika ya 28.

Wakati mchezo huo ukionekana kumalizika kwa sare, shujaa wa Namungo alikuwa beki mkongwe, Erasto Nyoni aliyepeleka furaha baada ya kupiga frii-kiki safi ya dk87, iliyomshinda kipa wa Mashujaa, Patrick Munthary na kuzama wavuni.

Akizungumzia mchezo huo, kocha wa Namungo, Juma Mgunda alisema ni matokeo mazuri kwa sababu yanazidi kuwapa morali ya kuendelea kufanya vizuri, japo bado kumekuwa na kutoelewana zaidi katika safu ya ulinzi jambo analoendelea kupambana nalo taratibu.

“Kwa hatua tulipofikia kwa sasa tunaangalia zaidi pointi tatu, ni kweli tumekuwa na makosa mengi katika safu ya ulinzi, ila hili ni suala la timu nzima, ushindi kwetu ulikuwa muhimu kuliko kitu kingine na tumefanikiwa hilo,” alisema Mgunda.

Ushindi huo unakuwa ni wa nane kwa Namungo FC msimu huu, baada ya kutoka sare michezo saba na kupoteza 12, kati ya 27 iliyocheza, ikiwa nafasi ya nane kwa pointi 31, ikijiweka katika mazingira mazuri ya kukwepa kushuka daraja.