Simbu ang'ara, ashika nafasi ya pili Boston Marathon

Muktasari:
- Nyota huyo kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mwenye cheo cha Sajenti amemaliza wa pili akitumia muda wa saa 2:05:04, huku Mkenya John Korir aking'ara kwa kushika nafasi ya kwanza kwa muda wa saa 2:04:05
Mwanariadha wa Kimataifa wa Tanzania Alphonce Simbu ameng'ara katika mbio za Boston Marathon ambazo zimemalizika muda mchache uliopita nchini Marekani baada ya kushika nafasi ya pili.
Simbu anakuwa Mtanzania wa pili kumaliza nafasi ya pili katika mbio hizo baada ya Nyota mwingine Gabriel Geay kufanya hivyo mwaka 2023.
Nyota huyo kutoka Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) mwenye cheo cha Sajenti amemaliza wa pili kwa muda wa 2:05:04 huku Mkenya John Korir aking'ara kwa kushika nafasi ya kwanza kwa muda wa saa 2:04:05.
Nafasi ya tatu imekwenda kwa Cybrian Kotut wa Kenya ambaye ametumia muda wa 2:05:08 huku mwenyeji Conner Mentz wa Marekani akimaliza wa nne kwa kutumia saa 2:05:08.
Kwa upande wa Wanawake Sharon Lokedi amemaliza wa kwanza kwa muda wa 2:17:22 huku akifuatiwa na Mkenya mwenzake ambaye ni Malkia wa mbio hizo Hellen Obiri ambaye amemaliza wa pili kwa kutumia muda wa 2:17:41 huku Yalemzerf Yehualaw wa Ethiopia akimaliza wa tatu kwa kutumia saa 2:18:06.
Meneja wa timu ya riadha ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ),Kapten Christopher Masanga amempongeza Simbu kwa kumaliza wa pili huku akiweka wazi kuwa ushindi huo ni jitihada ambazo Mwanariadha huyo anafanya katika kuitangaza.
"Tumefurahi sana kama Jeshi kwa Mwanariadha wetu kufanya vizuri na kuiwakilishi nchi na haya ndio matunda ya JWTZ chini ya Mkuu wetu wa Majeshi kutoa nafasi kwa vijana wenye vipaji kuitangaza nchi Kimataifa kupitia michezo"amesema Masanga.