Nishimura: Azua gumzo Brazil kwa maamuzi yake tata

Muktasari:
- Kwenye mchezo huo, Oscar alihusika kwenye mabao yote matatu ya Brazil, ambapo mawili yalifungwa na Neymar na moja alifungwa kiungo huyo na hivyo kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza anayecheza soka kwenye Ligi Kuu England kufunga kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia mwaka huu.
SAO PAULO, BRAZIL
KIUNGO, Oscar aling’ara juzi Alhamisi usiku wakati Brazil ilipoichapa Croatia 3-1 kwenye mechi ya ufunguzi ya fainali za Kombe la Dunia iliyofanyika mjini Sao Paulo.
Kwenye mchezo huo, Oscar alihusika kwenye mabao yote matatu ya Brazil, ambapo mawili yalifungwa na Neymar na moja alifungwa kiungo huyo na hivyo kuweka rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza anayecheza soka kwenye Ligi Kuu England kufunga kwenye fainali hizo za Kombe la Dunia mwaka huu.
Lakini, wakati Neymar na Oscar wakiing’arisha Brazil, kuna mtu mmoja amegeuka kuwa gumzo karibu dunia nzima na kutawala kwenye vichwa vya habari vya magazeti mbalimbali baada ya mechi hiyo iliyopigwa Sao Paulo. Mtu huyo ni mwamuzi, Mjapani Yuichi Nishimura.
Mwamuzi huyo anadaiwa kuwa ndiye mtu aliyetibua zaidi fainali hizo za Kombe la Dunia ikiwa ni mechi ya kwanza tu kutokana na uchezeshaji wake kuwa na mambo mengi yenye utata kiasi cha kupondwa na Croatia pamoja na waamuzi wastaafu wa mchezo huo wa soka.
Ashindwa kumwonyesha kadi nyekundu Neymar
Kwenye mchezo huo, Mjapani Nishimura anashutumiwa kwa kushindwa kuchukua uamuzi wa kumwonyesha kadi nyekundu staa wa Brazil, Neymar, ambaye alioneka wazi kumpiga kiwiko kiungo wa Croatia, Luka Modric.
Kocha Mkuu wa Croatia, Nico Kovac alisema alianza kumtilia shaka mwamuzi huyo baada ya kushindwa kuchukua uamuzi uliostahili kufuatia tukio hilo la Neymar kumchezea madhambi kwa kumpiga kiwiko Modric wakati wa kipindi cha kwanza.
Kitendo hicho kiliibua mjadala mkubwa baada ya mechi huku kocha huyo wa Croatia akifika mbali zaidi kwa kudai hakuwa refa mwafaka kwa mechi ngumu kama hiyo ya ufunguzi ambayo mara nyingine imekuwa na presha kubwa kutoka pande zote mbili za timu zinazochuana.
Ampa Fred penalti ya utata, akataa bao
Kwenye kipindi cha pili, mwamuzi Nishimura alidaiwa kutibua zaidi hali nzima ya mchezo baada ya kutoa adhabu ya penalti kwa wenyeji Brazil kufuatia mshambuliaji kuangusha kwenye eneo la hatari.
Refa huyo Mjapani alitoa penalti hiyo kwa maadai kwamba Fred alikuwa ameshikwa wakati alipopokea pasi kutoka kwa Oscar akiwa ndani ya eneo la penalti la goli la Wacroatia. Baada ya kupiga filimbi ya kuashilia kwamba ni penalti, wachezaji wote wa Croatia walikwenda kumzonga mwamuzi huyo wakilalamikia uamuzi wake kitu ambacho kiliwaacha pia kwenye mshangao wa wengi kutokana na uamuzi huo kwa sababu haikuonekana kuwa ni tukio ambalo lingesababisha penalti kwenye mechi ngumu kama hiyo.
Penalti hiyo iliifanya Brazil kuongoza kwa mabao 2-1 na hivyo kuwa na nguvu ya kuibuka na ushindi kabla ya Oscar kuongeza bao la tatu ambalo liliwapa ushindi mnono. Lakini, kama haitoshi, Nishimura anashutumiwa na Wacroatia kwamba aliwanyima bao lao lililokuwa la kusawazisha kwa madai kwamba Ivica Olic alimchezea rafu kipa Julio Cesar wakati waliporuka kuwania mpira wa juu.
Aliwahi kumpa kadi nyekundu Melo
Mwamuzi Nishimura mechi hiyo ya juzi haikuwa ya kwanza kwake kuchezesha kwenye fainali za Kombe la Dunia. Kwenye Kombe la Dunia 2010 zilizofanyika nchini Afrika Kusini, alichezesha mechi ya robo fainali kati ya Uholanzi la Brazil iliyofanyika kwenye Uwanja wa Nelson Mandela Bay mjini Port Elizabeth.
Kwenye mechi hiyo, Nishimura alimtoa kwa kadi nyekundu kiungo wa Brazil, Felipe Melo kwenye dakika 73 na kuwafanya Wabrazili kucheza pungufu mchezo huo ambao uliishia kwa kukumbana na kichapo.
Kwenye fainali hizo pia, Nishimura alikuwa mwamuzi wa akiba katika mechi ya fainali iliyozikutanisha timu za Uholanzi na Hispania, huku akiwa amechezesha pia mechi kati ya Ufaransa na Uruguay kwenye fainali za Kombe la Dunia 2010 nchini Afrika Kusini.
Chanzo cha vurugu mechi ya TP Mazembe
Nishimura anatajwa kuwa ni bingwa wa maamuzi tata ambayo yalisababisha mashabiki wa klabu ya TP Mazembe kufanya fujo nchini Japan baada ya mechi yao ya fainali dhidi ya Inter Milan kwenye Klabu Bingwa ya Dunia mwaka 2010.
Refa huyo aliripotiwa kuwa chanzo cha vurugu hizo baada ya mashabiki wa TP Mazembe kukerwa na maamuzi yake ambapo alipuliza kipyenga mara 21 akidai kwamba TP Mazembe imecheza faulo, wakati alipuliza filimbi yake mara tisa tu kwa upande wa kikosi cha Inter Milan.
Kwa hasira, mashabiki wa timu hiyo ya DR Congo waliamua kufanya vurugu kwenye mgahawa wa Kijapani kutokana na hasira zilizotokana na uamuzi wa uwanjani wa Nishimura.
Apingwa na mwanamke, achemsha Japan
Nishimura ana historia ya aina yake. Desemba mwaka jana wakati alipokuwa akikabidhiwa tuzo ya Mwamuzi Bora wa Ligi Kuu Japan, mwanamke mmoja aliyekuwa kwenye kundi la mashabiki waliohudhuria tuzo hizo alipiga kelele akipinga tuzo kwenda kwa Nishimura huku akidai amekuwa akiukosea heshima utamaduni wa Kijapani.