Prime
Njia ya Siri Inayomtoa Camara Simba
WAKATI Simba ikiendelea kufanya tathmini ya kikosi chake kuelekea msimu ujao, kipa wake raia wa Guinea, Moussa Camara, ameibua na kudai tayari ana ofa mbili kutoka Ulaya ambazo zinaweza kumbeba iwapo mabosi wa Msimbazi hawatafikia makubaliano ya kumuongezea mkataba.
Camara alijiunga na Simba msimu wa 2024/25 akitokea Guinea na hakuchukua muda mrefu kuonyesha uwezo wake ambapo msimu uliopita aliifikisha Simba kwenye fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Katika msimu wake wa kwanza akiwa Simba, Camara aligeuka kuwa mmoja wa wachezaji muhimu kutokana na uwezo wake wa kuokoa mipira ya hatari, kuongoza safu ya ulinzi na kuonyesha utulivu katika mechi kubwa, jambo lililomfanya aongezewe mkataba wa mwaka mmoja lakini mwanzoni mwa msimu huu Simba ilimuondoa kwenye usajili wake ili apate nafasi ya kujiuguza baada ya kuumia na kusajiliwa Djibril Kassali ambaye anaitumikia timu hiyo hadi sasa.
Taarifa ambazo Mwanaspoti imezipata kutoka kwa mmoja wa watu wa karibu wanaomsimamia kipa huyo zimeeleza kuwa Camara kwa sasa anasubiri kusikia msimamo rasmi wa Simba kuhusu mustakabali wake, huku klabu kutoka Ufaransa na Kazakhstan zikionyesha nia ya dhati ya kumtaka.
Chanzo hicho kilisema kuwa kipa huyo hana haraka ya kufanya uamuzi kwa sasa kwa sababu anaiheshimu Simba na anataka kwanza kujua mipango ya klabu hiyo kabla ya kuamua hatua inayofuata katika maisha yake ya soka.
“Ni kweli mkataba wake unaelekea mwisho na tunasubiri kuona Simba watasema nini. Wakihitaji aendelee, tutakaa chini tuzungumze, lakini kama kutakuwa na mwelekeo tofauti, basi tutalazimika kuangalia ofa zilizopo,” kilisema chanzo hicho.
Kiliongeza kuwa tayari kuna klabu mbili kutoka Ulaya, katika nchi za Ufaransa na Kazakhstan.
“Kuna njia mbili mbele yake kwa sasa. Anaweza kwenda Kazakhstan au Ufaransa. Kote huko kuna timu zinazomfuatilia kwa karibu. Kazi aliyofanya Simba kila mtu ameiona. Huyu ni kipa wa kiwango kikubwa na hawezi kukosa timu nzuri ya kucheza,” kiliongeza chanzo hicho.
Ikumbukwe Simba imekuwa ikifanya maboresho katika kikosi chake kuelekea msimu mpya, hivyo hatma ya Camara inaweza kuathiri mipango mingine ya usajili wa makipa, licha ya uwepo wa Kassali Djibril ambaye mkataba wake unamalizika mwishoni mwa msimu.
Hata hivyo, mmoja wa viongozi wa Simba ambaye hakutaka kutajwa jina amesema kuwa bado wanasubiri taarifa ya kocha itakavyosema mwishoni mwa msimu.
“Tunaangalia jinsi ya kupambana na kutwaa ubingwa wa ligi, unajua kuna mechi tano ngumu na hatuwezi kuchanganya mambo mengi.”