Ouma ataja mambo matatu akiikabili Yanga

Muktasari:
- Singida Black Stars kesho Juni 29, 2025 itacheza dhidi ya Yanga katika mchezo wa fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) utakaofanyika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kuanzia saa 2:15 usiku.
KOCHA wa Singida Black Stars, David Ouma amesema kikosi cha timu hiyo kipo tayari kwa mechi ya fainali, huku akitaja mambo matatu waliyojiandaa nayo.
Singida Black Stars kesho Juni 29, 2025 itacheza dhidi ya Yanga katika fainali ya Kombe la Shirikisho (FA) utakaofanyika Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar kuanzia saa 2:15 usiku.
Timu hizo zinakutana huku kila moja ikiwa vizuri katika michuano hii linapokuja suala la kufunga na kuzuia ambapo Singida imefunga mabao 12 na kuruhusu moja, Yanga ikifunga 20 na kuruhusu mawili, zote zikishuka dimbani mara tano kuanzia hatua ya 64 bora hadi sasa zikisubiri fainali.
"Hii ni mechi ya fainali, ili ushinde lazima ufunge bao na usiruhusu, kitu cha pili kama hamuwezi kufunga na kufungwa basi mtaamuliwa na matuta," amesema Ouma na kuongeza;
"Kuna mambo matatu ambayo sisi Singida Black Stars tunajiweka nayo kwenye maandalizi yetu, kushinda ndani ya dakika 90, ikishindikana iwe zile za nyongeza au penalti."
Kuhusu namna kikosi chao kilivyo, Ouma amesema kimeimarika zaidi kiuchezaji huku malengo yakifikiwa, kilichobaki ni nyongeza ili kuleta kitu cha tofauti.
"Ukiangalia vizuri sisi kama Singida Black Stars tumeimarika sana kulingana na mchezo wetu na malengo ya timu.
"Malengo yaliyowekwa mwanzo wa msimu tumeyafikia na tunaendelea nyongeza ambapo tuna nafasi ya kuwa mabingwa.
"Tunataka kushinda ubingwa huu kwa sababu hiyo ndio itaonesha malengo tofauti kwa sababu ukiangalia timu iliyofika fainali kwa ugumu ni Singida Black Stars," amesema Ouma na kuongeza;
"Katika fainali hakuna timu ndogo wala kubwa, kitu muhimu ni matokeo bora. Huwa tunawaheshimu wapinzani.
"Hatuwezi kulinganisha mechi hii na zilizopita, tahadhari kubwa tunayochukua sisi ni kuwa upande wa kushinda."
Msimu huu, Singida Black Stars imepoteza mechi zote mbili ilizocheza dhidi ya Yanga kwenye ligi, ilianza kufunga 1-0, kisha 2-1 na fainali hii ni ya kwanza kwa timu hiyo katika Kombe la FA kwani tangu ikifahamika kama Ihefu, hatua ya juu kufika ilikuwa ni nusu fainali msimu uliopita na kupoteza 1-0 mbele ya Yanga kwa bao la Stephane Aziz Ki.