Pluijm alivyoishi miezi sita Yanga

Aliyekuwa Kocha wa Yanga, Hans Pluijm
Muktasari:
Wakati akiwa katika hatua za mwisho za kupanda ndege kurudi kwake Ghana anapoishi na familia yake, Pluijm ambaye ni raia wa Uholanzi alizungumza na Mwanaspoti kuhusiana na mambo kadhaa aliyokutana nayo katika soka la Tanzania na zaidi klabuni Yanga.
ALIYEKUWA Kocha wa Yanga, Hans Pluijm amebakiza wiki moja kuanza kibarua chake kipya katika klabu ya Al Sholah ya Saudi Arabia ambayo ilikuwa inamwinda kwa zaidi ya miezi sita.
Wakati akiwa katika hatua za mwisho za kupanda ndege kurudi kwake Ghana anapoishi na familia yake, Pluijm ambaye ni raia wa Uholanzi alizungumza na Mwanaspoti kuhusiana na mambo kadhaa aliyokutana nayo katika soka la Tanzania na zaidi klabuni Yanga.
Anavyoiacha Yanga
“Ninafurahi kuona nimeweza kufanya maboresho makubwa kupitia falsafa yangu ya kutaka soka la kushambulia. Naamini sisi ndio tulikuwa vizuri pengine kuliko timu nyingine yoyote katika Ligi Kuu Bara japo tulifanya makosa kidogo mwishoni hadi tukapoteza malengo yetu (kukosa ubingwa),” anasema.
“Yanga wana kikosi bora, ndiyo maana nilikwambia kuwa tulikuwa vizuri. Kuna wachezaji jasiri sana, ukizungumzia ubora kwa jumla naweza kusema kuna sehemu tulitaka kufika, lakini ikashindikana kidogo kutokana na sababu mbalimbali.”
Tatizo la wachezaji wa Tanzania
Kuhusu hilo, anasema: “Kubwa ni ukosefu wa elimu ya darasani na hata msingi wa soka wengi wameukosa. Ukiwa kocha Tanzania na sio hapa karibu nchi nyingi za Afrika ni lazima ulitambue hili, nafikiri kuna kazi kubwa inatakiwa kufanyika katika kukuza vipaji vya watoto ili wasije kuwa na tatizo hilo, kwa sasa ni vigumu kupata mafanikio makubwa katika aina hii ya wachezaji.”
Vipaji vya nyota wa Yanga
“Kuna baadhi wana vipaji vya uhakika, lakini wengine nafikiri hawakutakiwa kuja kuichezea Yanga. Sitaki kutaja majina, lakini nafikiri ningekuwa naendelea kuifundisha wengi wangeondolewa, hata hivyo katika ripoti yangu nimewapendekeza kutolewa. Yanga ni timu kubwa, inahitaji wachezaji mahiri,” anasema.
Kuhusu kocha mpya Yanga
“Nimewaahidi Yanga kuwatafutia kocha, naipenda hii klabu ndiyo maana nikafanya ustaarabu kuwaaga vizuri na hata hili la kuchukua kadi ya uanachama nalo ni uthibitisho wa mapenzi yangu kwa Yanga,” anaweka wazi.
“Ni hivi, ukimpenda mke wako huwezi kumsaliti. Nitawatafutia Yanga kocha anayepaswa kuwanoa kulingana na ushindani wa soka la Tanzania.”
Kuondoka kwa Domayo, Kavumbagu
“Sioni tatizo kubwa tofauti na watu wengine wanavyofikiria. Frank (Domayo) ni kijana mdogo anayetakiwa kujifunza mengi, utajifunza katika timu kubwa, ni jambo zuri kwamba Yanga walimpatia nafasi kubwa ya kucheza, lakini nasema hakuwa aina ya kiungo mkabaji ambaye utasema akiondoka kwako utachukia,” anasema.
“Inawezekana ni kwa Tanzania pekee lakini wapo viungo wengi wazuri hapa Afrika, huwezi kuitwa kiungo mzuri kwa kuzuia pekee vipi kuhusu kutengeneza nafasi na hata kufunga?
“Hata Didier (Kavumbagu), mara nyingi nilikuwa nazungumza naye juu ya uchezaji wake, kuna siku shabiki mmoja aliniambia nisithubutu kumwacha Didier, nilimwitikia lakini kwangu mimi mchezaji mzuri kama yeye ni lazima awe na uwezo mwingine wa kukaba kidogo, unaweza kumwona anakaba, lakini ni mpaka umwambie kufanya hivyo.”
Mchezaji Bora wake Yanga
“Moja kwa moja nitakutajia kuwa ni nahodha (Nadir Haroub ‘Cannavaro’). Ni mchezaji wa aina yake, sikuwahi kumpa majukumu halafu akashindwa kuyatekeleza. Ni mpiganaji wa kweli, ninajivunia kufanya kazi naye,” anaongeza.
“Pia anapenda kujifunza, mara kadhaa tulipomaliza mazoezi aliweza kuja kwangu na kutaka kujua nini amepungukiwa ili akifanyie kazi zaidi, hata Joshua (Oscar) naye ni kati ya wachezaji ninaojivunia kufanya nao kazi.”
Waliokuwa wakimkera
“Hapana hapo siwezi kukwambia wewe Mwandishi wa Habari, nadhani nitakuwa nawakosea haki. Kuna wakati huwa najiuliza, kocha anawezaje kusema mbele za watu kuwa wachezaji hawa ni wabovu, tena kwa kuwataja majina.
“Unapofanya hivyo hadharani hata kama kulikuwa na mtu anamfuatilia huyo mchezaji kwa kutaka kumsajili, anaweza kusitisha mipango yake na baadaye ukaharibu kila kitu.”
Vipi kuhusu Ngassa?
“Nilikuwa namtafuta sana ili nimwachie ujumbe wangu kwake, (Mrisho) Ngassa ni mchezaji mzuri lakini anatakiwa kubadilika haraka hasa kwa kujifunza kukaba, hapo ndipo ninaposema wachezaji wengi wameukosa msingi mzuri,” anabainisha.
“Ngassa ninaweza kumfananisha na Romario, lakini tatizo lake yeye hapendi kukaba. Ni tatizo kubwa katika soka.”
Mechi iliyomchukiza zaidi
“Ni ile tuliyopoteza kule Tanga kwa mabao 2-1 (dhidi ya Mgambo Shooting). Ilikuwa mechi mbaya ambayo ilituharibia kila kitu, ni makosa yetu wenyewe hasa kutokana na makosa ya Kelvin (Yondani) na hata kipa (Juma Kaseja),” anasema.
“Kwa kweli yalikuwa makosa ambayo yalinichefua, lakini ndiyo soka na wao bado ni wachezaji wazuri wanaotakiwa kujirekebisha na kuisaidia timu.”
Tofauti ya soka Tanzania na Ghana
“Ghana wanapiga hatua kubwa kwa kuzalisha vijana wengi watakaokuwa bora baadaye, Tanzania bado kuna siasa katika kuweka mkazo kwenye soka la vijana,” anafafanua.
“Kuna mipango ya muda mfupi kuliko kuangalia mbele zaidi, sijaona nguvu ya shirikisho la hapa katika hilo, lakini Tanzania imepata kocha mzuri (Mart Nooij) wakimtumia vizuri na kumsikiliza watafanikiwa.”
Anafahamu wachezaji walimpa jina la Moyes?
“(Anacheka kidogo), Ninajua kuwa wachezaji wangu walikuwa wananiita hivyo, unajua wachezaji ni kama watoto, walikuwa wanafanya hivyo kwa siri, lakini kuna siku mmoja akajisahau akaniita nikasikia, alikuwa Ngassa. Wenzake wote walishtuka kujua nimesikia, nikamwambia asijali basi wenzake wote wakafurahi,” anasema.
“Nimefanya kazi Afrika kwa zaidi ya miaka kumi, lakini hata mke wangu ameniambia kitu kimoja katika kuishi kwetu kwamba hakuna klabu aliyoipenda kama Yanga. Ile sherehe ndogo ya kuagwa kwangu imekuwa na maana kubwa sana, nitarudi hapa ingawa meneja wangu anapenda sana fedha nyingi, lakini sikutaka kuondoka hapa.”