Prisons inaanzia KMC

Muktasari:
- Mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara imepangwa kupigwa Aprili 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa KMC, Mwenge.
BAADA ya kumaliza kambi ya siku 10 katika Kituo cha Magereza Kiwila mkoani Mbeya, Tanzania Prisons imetua jijini Dar es Salaam kukabiliana na KMC.
Mechi hiyo ya Ligi Kuu Bara imepangwa kupigwa Aprili 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa KMC, Mwenge.
Kocha wa Tanzania Prisons, Amani Josiah alisema japokuwa hakuwa na timu kwa siku tano ambazo alikuwa katika kozi, anatambua kila kitu ambacho kilikuwa kinaendelea chini ya wasaidizi wake kuhusiana na maendeleo ya wachezaji.
“Kabla sijaenda Tanga katika ‘refresher course’ zipo mechi za kirafiki ambazo zilichezwa chini yangu na zingine chini ya makocha wasaidizi. Naamini kupitia hizo zimetupa taswira ya kipi kilihitaji kuboreshwa ili tunaporejea kuendelea na Ligi Kuu tutakuwa na hatua nyingine ya ushindani,” alisema na kuongeza:
“Nakutana na timu Dar es Salaam baada ya kutoka Tanga kwenye kozi, kikubwa ni kujiandaa na mechi na KMC ni muhimu kwetu kupata pointi tatu ambazo zitatufanya tuondoke katika nafasi mbaya kwenye msimamo wa Ligi Kuu.”
Tanzania Prisons iliyopo nafasi ya 15 katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 18, imecheza mechi 23, imeshinda nne, sare sita na kupoteza 13, imefunga mabao 12 ya kufungwa 31.
Katika duru la kwanza timu hizo zilipokutana Uwanja wa Sokoine jijini Mbeya, Oktoba 26, 2024, KMC ilishinda 2-1.