Prisons yakumbushia msimu wa 2014/15

Muktasari:
- Tanzania Prisons ilikaa bila kuonja ushindi tangu ilipoifunga Mashujaa mabao 2-1, Februari 6, 2025, hivyo baada ya ushindi wa Jumapili iliyopita dhidi ya Kagera Sugar, wachezaji wa timu hiyo wamepata nguvu upya.
KITENDO cha Tanzania Prisons kushinda bao 1-0 dhidi ya Kagera Sugar, kimewapa morali na nguvu wachezaji wa timu hiyo kuanza hesabu kali za namna ya kupambana wasishuke daraja.
Tanzania Prisons ilikaa bila kuonja ushindi tangu ilipoifunga Mashujaa mabao 2-1, Februari 6, 2025, hivyo baada ya ushindi wa Jumapili iliyopita dhidi ya Kagera Sugar, wachezaji wa timu hiyo wamepata nguvu upya.
Licha ya ushindi huo, bado Tanzania Prisons imeendelea kusalia nafasi ya 15 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 21 baada ya kucheza mechi 25 ikibakiwa na tano kumaliza msimu huu.
Katibu wa timu hiyo, John Matei, alisema: “Iliwahi kutokea msimu wa 2014/15 tukawa na matokeo mabaya ila mechi za mwisho zikatubakisha Ligi Kuu.”
Msimu huo Prisons ilimaliza ya 11 na pointi 29 katika timu 14. Ilishinda mechi 5 msimu mzima.
Mshambuliaji wa Tanzania Prisons, Jeremiah Juma alisema ushindi huo umewapa nguvu ya kupiga hesabu za jinsi ya kusalia Ligi Kuu Bara kwa msimu ujao.
“Tupo nafasi mbaya kwenye msimamo wa Ligi Kuu ila haina maana tumekata tamaa, tunapambana hadi dakika ya mwisho kuhakikisha tunafanikisha malengo yetu,” alisema.
Kwa upande wa kipa wa timu hiyo, Mussa Mbissa, alisema:
“Ushindi dhidi ya Kagera umetupa nguvu ya kuendelea kupamba kuhakikisha mechi zilizopo mbele yetu tunashinda na kusalia Ligi Kuu.”
Katika mechi tano zilizobaki zenye pointi 15, Tanzania Prisons inatakiwa kushinda zote ili kufikisha 36, huku ikihitaji kuziombea mabaya timu za juu yake ziteleze kufuatia hivi sasa kupishana pointi tano na timu iliyopo nafasi ya 12, Pamba Jiji ambayo haipo katika mstari wa kushuka daraja wala kucheza mechi za play-off.
Mechi hizo tano italazimika kucheza dhidi ya KenGold inayoburuza mkia, kisha itaikabili JKT Tanzania, Coastal Union, Yanga na Singida Black Stars.