Rais Samia awaahidi Simba Sh30 milioni kila bao fainali CAFCC

Muktasari:
- Simba inatarajia kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane baada ya kutinga hatua hiyo kwa kuifunga Stellenbosch ya Afrika Kusini kwa ushindi wa jumla wa bao 1-0.
Rais Samia Suluhu Hassan, ametoa ahadi ya Sh30 milioni kwa nyota wa Simba kwenye kila bao litakalofungwa kwenye mechi ya fainali.
Simba inatarajia kucheza fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya RS Berkane baada ya kutinga hatua hiyo kwa kuifunga Stellenbosch ya Afrika Kusini kwa ushindi wa bao 1-0.
Msemaji wa Serikali, Gerson Msigwa amesema Rais Samia anawapongeza Simba kwa kutinga hatua ya fainali na anawatakia kila la kheri kwenye mechi mbili za fainali zilizo mbele yao kwa kutoa ahadi ya kununua kila bao watakalofunga kwa Sh30 milioni.
“Mheshimiwa Rais anaamini Simba watabeba taji la michuano hiyo, anatambua kutakuwa na mechi mbili ya nyumbani na ugenini hivyo kwenye mechi zote kila bao watakaloshinda ni milioni 30.
“Mkifunga moja milioni 30, mawili 60, matatu 90 manne Sh120 milioni, mama amefanya hivi kwa lengo la kuwapa hamasa wachezaji wawe na morali, waweke juhudi kiwanjani na kushinda mechi zote mbili,” amesema Msingwa.
Amesema michezo ni uchumi, burudani, ajira na Simba wanaposhinda kwenye hayo mashindano makubwa wanapeperusha bendera ya Tanzania, wanatangaza fursa za uchumi wa nchi, uwekezaji na utalii mapato yake kila Mtanzania atanufaika.
Simba inatarajia kuanza kucheza fainali ya kwanza Mei 17 ugenini na kumaliza fainali ya pili kwenye uwanja wa nyumbani hapa Tanzania Mei 25 kombe likiwa uwanjani.
Hii ni fainali ya pili ya Afrika kwa Simba baada ya 1993 ilipocheza fainali ya Kombe la CAF na kupoteza 2-0 dhidi ya Stella Abdijan ya Ivory Coast kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam. Ilitoka 0-0 ugenini.