Rekodi zaiponza Yanga Morogoro

Wachezaji wa Yanga na makocha wao wakijihamasisha kwa kuomba dua kabla ya kuanza mazoezi yao jana Ijumaa asubuhi kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro. Katika uwanja huo leo Jumamosi timu hiyo itavaana na Mtibwa Sugar katika mechi ya Ligi Kuu Bara.
Muktasari:
- Mechi nyingine itachezwa Uwanja wa Kaitaba, Bukoba kwa kuwakutanisha wenyeji Kagera Sugar dhidi ya maafande wa Prisons kutoka Mbeya.
LIGI Kuu Bara inaendelea leo Jumamosi kwa mechi tatu kuchezwa kwenye viwanja vitatu tofauti. Mabingwa watetezi Yanga wataumana na Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro wakati vinara wa ligi hiyo, Azam wanaikaribisha Coastal Union ya Tanga kwenye Uwanja wa Azam Complex, Chamazi, Dar es Salaam.
Mechi nyingine itachezwa Uwanja wa Kaitaba, Bukoba kwa kuwakutanisha wenyeji Kagera Sugar dhidi ya maafande wa Prisons kutoka Mbeya.
Gumzo la mechi lipo Morogoro ambapo Yanga inacheza na Mtibwa Sugar ikiwa na rekodi mbaya katika mji huo kwani haijapata ushindi wowote tangu Septemba 2009 ilipoifunga timu hiyo kwa mara ya mwisho.
Yanga iliifunga Mtibwa nyumbani mabao 2-1 mwaka huo na tangu hapo, Wanajangwani hawajawahi kupata ushindi mwingine wowote katika mechi ilizocheza na Mtibwa kwenye uwanja huo.
Katika michezo mitatu iliyozikutanisha timu hizo Morogoro tangu mwaka 2010, Yanga imeambulia kipigo kimoja na sare mbili pekee. Yanga ilitoka sare ya 1-1 Septemba 2010, pia ilitoka suluhu Septemba 2011 kabla ya kufungwa mabao 3-0 Septemba 2012.
Hata hivyo, hali pia si nzuri kwa Mtibwa kwenye mechi ilizokutana na Yanga Dar es salam kwani katika kipindi cha miaka mitano iliyopita imeshinda mchezo mmoja pekee.
Mtibwa iliifunga Yanga bao 1-0 Februari 2011 ikiwa ni ushindi pekee katika kipindi cha zaidi ya miaka mitano.
Yanga katika kipindi cha miaka mitano imeshinda michezo minne dhidi ya Mtibwa Dar es Salam huku ikipata sare mbili katika michezo mingine jijini humo. Ushindi mkubwa Yanga iliyoupata nyumbani ni wa mabao 3-1 mara mbili tofauti Februari 2010 na 2012.
Timu hizo zinaingia uwanjani huku Yanga ikiwa nafasi ya tatu na pointi 38 katika mechi 17 ilizocheza huku Mtibwa ikiwa nafasi ya nane na pointi 25 baada ya kucheza mechi 20.
Yanga morali juu
Kocha wa Yanga, Hans Van Der Pluijm alisema; “Nataka ushindi. Matarajio yangu ni ushindi na sioni sababu ya kupoteza mechi hii, nataka tushinde ili tuongeze pointi zitakazotutoa nafasi ya tatu.”
Wachezaji wa Yanga, beki wa kushoto, Oscar Joshua na straika Didier Kavumbagu, wamesema hawana mchecheto na mechi hiyo kwani morali yao ya kufanya vizuri, imeongezeka zaidi licha ya kutolewa na Al Ahly.
Oscar alisema: “Ndiyo tumetolewa Ligi ya Mabingwa, lakini haiwezi kuwa sababu ya kutupoteza morali sisi wachezaji, morali ipo pale pale na pengine imeongezeka zaidi.”
Naye Kavumbagu alisema inauma sana kutolewa na Al Ahly Ligi ya Mabingwa Afrika: “Inauma lakini ndiyo imeshakuwa lakini ili kudhihirisha ubora wetu ule wa Ligi ya Mabingwa tunatakiwa kufanya vizuri kwenye ligi ili kujitengenezea nafasi nzuri zaidi mwakani.”
Mtibwa yakomalia
Kocha wa Mtibwa, Mecky Maxime na nahodha wake, Shaaban Nditi wameapa kutokuwa daraja la Yanga kupata pointi tatu kwani hawakubali kufungwa na wamejiandaa vizuri kushinda mechi hiyo.
“Yanga wasidhani mechi hii itakuwa rahisi kwao, sisi tumejiandaa vizuri tu kuhakikisha tunashinda kwani tunahitaji pointi tatu ili tusonge mbele maana hali katika ligi si nzuri sasa,” alisema Maxime.
Naye Nditi alisema; “Hatupo mahali pazuri katika ligi, tunahitaji pointi tatu ili tukae pazuri na Yanga nao wanataka pointi hizo hizo ili wakae juu ya msimamo wa ligi, mechi itakuwa ya kuvutia sana.”
Mrisho Ngassa, Mbuyu Twite na Haruna Niyonzima hawakushiriki mazoezi ya jana Ijumaa, mjini Morogoro kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo majeruhi.