Sh 11.8 bilioni zatua akaunti Simba

Muktasari:
- Simba imetinga hatua ya robo fainali ya mashindano ya klabu Afrika mara tano na mara moja imefanikiwa kuvuka hadi hatua ya nusu fainali tangu mfumo wa mashindano hayo ulipobadilika mwaka 2001.
Kufuzu kwa Simba nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika baada ya kuitoa Al Masry kwa mikwaju ya penalti 4-1, kunamaliza kiu ambayo ilikuwa nayo tangu 2018 ilipoanza kujijenga upya baada ya kushindwa kushiriki mashindano ya kimataifa kwa muda mrefu.
Kusonga mbele dhidi ya Al Masry kumelipa kisasi cha timu hiyo ya Misri kuizuia Simba kutinga hatua ya makundi katika Kombe la Shirikisho mwaka 2018 iliposhiriki mashindano ya kimataifa kwa mara ya kwanza baada ya kuyakosa kwa miaka mitano mfululizo.
Kuanzia 2018 hadi sasa, Simba imeishia hatua ya robo fainali ya mashindano ya Klabu Afrika mara tano na imeingia nusu fainali mara moja
Kwa kuishia robo fainali mara tano na safari hii kuingia nusu fainali, Simba kuanzia 2018 hadi sasa, imeingiza takribani Dola 4.4 milioni (Sh11.8 bilioni) kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Ilipotinga robo fainali katika Ligi ya Mabingwa Afrika 2018/2019 na 2020/2021 kila msimu ilipata kiasi cha Dola 650,000.
Msimu wa 2021/2022 ilipata Dola 550,000 kwa kutinga robo fainali Kombe la Shirikisho Afrika na ilipata kiasi cha Dola 900,000 kwa kila msimu pindi ilipoishia robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika 2022/2023 na 2023/2024.
Kwa kutinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu, Simba ina uhakika wa kupata kiasi cha Dola 750,000 kutoka Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF).
Simba kwa msimu huu inaweza kuvuna kiasi kikubwa zaidi cha fedha ikiwa itasonga mbele na kuingia fainali au kuchukua Kombe la Shirikisho Afrika.
Ikiwa itachukua ubingwa wa mashindano hayo, Simba itapata kiasi cha Dola 2 milioni (Sh5.4 bilioni) na kama itamaliza katika nafasi ya pili itapata kiasi cha Dola 1 milioni (Sh2.7 bilioni).
Katika hatua ya nusu fainali, Simba itakabiliana na Stellenbosch ya Afrika Kusini ambapo mchezo wa kwanz utachezwa hapa Tanzania, Aprili 20 na mechi ya marudiano itachezwa Afrika Kusini, Aprili 27.
Timu hizo mbili zote hazijawahi kuingia katika hatua ya fainali ya mashindano hayo tangu mfumo wake ulipobadilika mwaka 2001.
Nusu fainali nyingine ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu itazikutanisha RS Berkane ya Morocco na CS Constantine ya Algeria.