Siku 35 zaipa akili mpya Coastal Union

Muktasari:
- Wakati kikosi hicho kikiwa na muda huo kutokana na hapo kati ligi kusimama, kocha wa kikosi hicho, Joseph Lazaro amepanga kuandaa program maalum itakayowafanya wachezaji kuendelea kuwa fiti.
BAADA ya kumalizana na Tanzania Prisons, sasa Coastal Union ina takribani siku 35 za kujiandaa na mchezo ujao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Fountain Gate.
Wakati kikosi hicho kikiwa na muda huo kutokana na hapo kati ligi kusimama, kocha wa kikosi hicho, Joseph Lazaro amepanga kuandaa program maalum itakayowafanya wachezaji kuendelea kuwa fiti.
Timu hiyo juzi Jumatatu ilipokea kichapo cha mabao 2-1 kutoka kwa Tanzania Prisons na kuifanya kutokuwa salama katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 31 ikibakiwa na mechi mbili.
Lazaro amesema kusimama kwa ligi hiyo kunaweza kuwaathiri wachezaji kwani siku hizo zote kukaa bila mechi ya kimashindano yoyote inaweza kuwapunguzia makali mastaa wa kikosi hicho.
“Kwakuwa kuna sababu za kusimama ligi, hakuna tatizo, japokuwa mchezaji kukaa siku 30 bila kucheza inampunguzia makali, benchi la ufundi tutaweka program maalumu kukabiliana na kipindi hiki.
“Lazima tujue hadi sasa timu nyingi haziko salama, hata sisi tunahitaji ushindi kwenye mechi zilizobaki kuhakikisha tunakuwa salama kubaki Ligi Kuu, ushindani ni mkali,” alisema Lazaro.
Kocha huyo aliongeza kuwa, katika mchezo uliopita dhidi ya Tanzania Prisons walipolala 2-1, alibaini eneo la ushambuliaji kutokuwa makini akibainisha kuwa atalifanyia kazi ili kuwa imara.