Simba walioiua Yanga 5-0 wamebaki wawili tu

Sasa watu wote hao hawapo katika benchi la Simba, badala yake kocha ni Zdravko Logarusic, msaidizi wake ni Seleman Matola na kocha wa makipa ni Idd Pazi. Daktari ni Yassin Gembe.
Muktasari:
- Katika mchezo huo wa mwaka juzi, mabao ya Simba yalifungwa na Emmanuel Okwi (mawili), Felix Sunzu, Juma Kaseja na marehemu Patrick Mafisango. Ikiwa ni miaka miwili tu tangu Simba iibuke na ushindi huo mnono, kikosi chake cha kwanza kimebadilika kwa kiasi kikubwa kuanzia benchi la ufundi hadi wachezaji wake.
JUMAPILI ya Mei 6, 2012 kamwe haiwezi kusahaulika miongoni mwa wanachama na mashabiki wa Yanga baada ya timu yao kufungwa mabao 5-0 na Simba katika mchezo wa Ligi Kuu Bara Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Hata hivyo rekodi hii haifiki ile ya mwaka 1977 iliyowekwa na Simba ilipoifunga Yanga mabao 6-0 katika mchezo wa ligi.
Katika mchezo huo wa mwaka juzi, mabao ya Simba yalifungwa na Emmanuel Okwi (mawili), Felix Sunzu, Juma Kaseja na marehemu Patrick Mafisango. Ikiwa ni miaka miwili tu tangu Simba iibuke na ushindi huo mnono, kikosi chake cha kwanza kimebadilika kwa kiasi kikubwa kuanzia benchi la ufundi hadi wachezaji wake.
Katika benchi la ufundi alikuwepo Kocha Milovan Cirkovic ambaye ni raia wa Serbia, msaidizi wake alikuwa Richard Amatre kutoka Uganda huku kocha wa makipa akiwa marehemu James Kisaka. Daktari alikuwa Cosmas Kapinga.
Sasa watu wote hao hawapo katika benchi la Simba, badala yake kocha ni Zdravko Logarusic, msaidizi wake ni Seleman Matola na kocha wa makipa ni Idd Pazi. Daktari ni Yassin Gembe.
Ukitazama kikosi cha Simba siku hiyo kilipangwa hivi; Juma Kaseja, Nassor Masoud ‘Chollo’, Amir Maftah, Shomari Kapombe, Kelvin Yondan, Patrick Mafisango, Uhuru Suleiman, Mwinyi Kazimoto, Felix Sunzu, Haruna Moshi ‘Boban’ na Emmanuel Okwi.
Waliobaki katika kikosi hicho kwa sasa ni wachezaji wawili tu kwa walioanza ambao ni Chollo na Uhuru ambao hata hivyo bado hawana uhakika wa namba kwenye kikosi cha kwanza. Wengine wengine wapo katika timu nyingine ambao ni; Juma Kaseja; yupo Yanga alikosajiliwa Novemba mwaka jana.
Amir Maftah
Kwa sasa hana timu baada ya usajili wake Ashanti kushindikana. Aliondoka katika kikosi cha Simba tangu msimu uliopita. Hata hivyo amekuwa akionekana katika viwanja mbalimbali akifanya mazoezi binafsi na Mwanaspoti linajua kwamba anajisomea masuala ya lugha ya Kingereza ili kutafuta kazi mbadala.
Shomari Kapombe
Alisajiliwa na FC Cannes ya Ufaransa, lakini bado yupo nchini baada ya kutokea kwa mkanganyiko wa kimaslahi kati yake na Cannes huku Simba ikidai ilimuongezea mkataba wa miaka miwili. Yanga pia inatajwa kuwa na haki ya kummiliki.
Kelvin Yondan
Huyu alijiunga na Yanga tangu msimu wa 2012/13 na bado anaichezea timu hiyo kwa mafanikio huku akiwa kikosi cha kwanza.
Patrick Mafisango
Alichangia kwa kiasi kikubwa timu yake kuibuka na ushindi wa mabao 5-0, lakini hakuweza kufurahia sana ushindi huo kwani alifariki kwa ajali ya gari Mei 17, mwaka 2012 eneo la Keko na alizikwa kwao Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo siku chache baadaye. Amepumzika kwenye makaburi ya Kinkole pale Kinshasa.
Mwinyi Kazimoto
Ana msimu mmoja sasa tangu aachane na Simba mwaka jana. Anacheza soka la kulipwa huko Qatar katika klabu ya Al Markhiya. Mara kwa mara anaitwa Taifa Stars na anafanya vizuri katka klabu yake.
Felix Sunzu
Msimu uliopita ulipoisha naye akatimka zake kwao Zambia baada ya kumaliza mkataba wake na Simba. Hata hivyo kiwango chake kilianza kuonekana kinapungua hivyo uongozi wa Simba haukumuongezea mkataba. Anakipiga katika klabu ya Zanaco ya Zambia.
Haruna Moshi ‘Boban’
Kwa sasa anacheza Coastal Union ya Tanga. Utovu wa nidhamu ulitajwa kama tatizo kubwa alilonalo hivyo uongozi wa Simba mara kadhaa ulikuwa ukimsimamisha hadi ulipachana naye kabla kuanza kwa msimu huu.
Emmanuel Okwi
Huyu sasa anachezea Yanga, lakini alikuwa chachu ya ushindi wa Simba kwa Yanga kutokana na ukweli kwamba alisababisha penalti tatu na akafunga mabao mawili.
Kikosi cha Yanga katika mchezo huo kiliundwa na: Yaw Berko, Nsajigwa Shadrack, Oscar Joshua, Athumani Iddi ‘Chuji’, Nadir Haroub ‘Cannavaro’, Juma Seif ‘Kijiko’, Nurdin Bakari, Haruna Niyonzima, Davies Mwape, Rashid Gumbo na Hamisi Kiiza.
Katika kikosi cha Yanga waliopo kwenye timu hiyo mpaka sasa ni Joshua, Cannavaro, Haruna na Kiiza.
Berko yuko Simba, Nsajigwa yuko zake Nepal barani Asia. Kijiko amejiunga na Ruvu Shooting, Nurdin amejisajili Rhino Rangers, Mwape yupo kwao Zambia wakati Gumbo yupo Shelisheli. Chuji yupo Yanga lakini amesimamishwa na uongozi.