Simba yaichapa Stellenbosch, hesabu zinakubali

Muktasari:
- Mechi ya marudiano ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika itachezwa Durban, Aprili 27, 2025.
Pamoja na kupata ushindi kiduchu wa bao 1-0 dhidi ya Stellenbosch ya Afrika Kusini kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar, Simba bado ina nafasi kubwa ya kutinga hatua ya fainali ya kombe la Shirikisho Afrika.
Ili itinge hatua ya fainali, Simba inatakiwa ipate matokeo ya aina tatu katika mechi ya marudiano itakayochezwa kwenye Uwanja wa Moses Mabhida, Durban, Aprili 27 mwaka huu.
Simba itasonga mbele kwa kupata ushindi, kutoka sare au kupoteza kwa tofauti ya bao moja huku yenyewe ikiwa imepata bao.
Katika mchezo wa leo ambao ulionekana kuwa mgumu, bao pekee la Simba lilipachikwa na kiungo Charles Ahoua katika dakika za nyongeza za kipindi cha kwanza.
Ahoua alifunga bao hilo kwa mkwaju wa faulo uliojaa moja kwa moja wavuni, pigo ambalo lilitokana na Elie Mpanzu kufanyiwa faulo nje ya eneo la hatari la Stellenbosch.
Kabla na hata baada ya kuingia kwa bao hilo, timu hizo zilishambuliana mara kadhaa lakini safu zao za ulinzi zilikuwa imara kuokoa hatari ambazo zilielekezwa kwenye milango yao.
Ahoua angeweza kuiweka Simba katika nafasi nzuri kuelekea mechi ya marudiano iwapo angetumia vyema nafasi aliyoipata katika dakika za lala salama lakini akashindwa kukwamisha mpira wavuni.
Ahoua alipokea pasi nzuri kutoka kwa Mpanzu na kufanikiwa kumpiga chenga kipa wa Stellenbosch, Oscarine Masuluke lakini kwa mshangao wa wengi alipiga nje mpira huo.
Katika mchezo huo, kocha wa Simba, Fadlu Davids alifanya mabadiliko ya kuwatoa Kibu Denis, Steven Mukwala, Chamou Karaboue na Mohamed Hussein ambao nafasi zao zilichukuliwa na Lionel Ateba, Debora Fernandes, Valentine Nouma na Joshua Mutale
Stellenbosch iliwatoa Lesiba Nku, Enyinnaya Godswill, Andre De Jong, Devon Titus na Ibraheem Jabaar ambao nafasi zao zilichukuliwa na
Khomotjo Lokoloane, Athenkosi Mcaba, Sanele Barns, Phili Langelihle na Genino Palace.
Refa Jean Jacques Ndala katika mchezo huo aliwaonyesha kadi za njano Valentine Nouma wa Simba na wachezaji wawili wa Stellenbosch, Enyinnaya Godswill na Ibraheem Jabaar.