Singida Black Stars ni Azam FC na Tabora United tu!

Muktasari:
- Singida, Azam FC na Tabora United zipo kwenye vita kali ya kuwania nafasi ya tatu baada ya zote kucheza michezo 23 zikiachana kwa pointi chache, na hilo limemuibua Ouma kudai kuwa na vita kali na timu hizo, lakini akisisitiza kila mmoja anapaswa kushinda mechi zake.
KOCHA Mkuu wa Singida Big Stars (SBS), David Ouma amesema Azam FC na Tabora United zimeshika hatma ya timu hiyo kumaliza nafasi tano za juu kutokana na kuwa na mechi na timu hizo ambazo pia zinawania nafasi sawa na wao huku akidai wana kazi kubwa ya kufanya, lakini hana hofu kwani ana kikosi bora.
Singida, Azam FC na Tabora United zipo kwenye vita kali ya kuwania nafasi ya tatu baada ya zote kucheza michezo 23 zikiachana kwa pointi chache, na hilo limemuibua Ouma kudai kuwa na vita kali na timu hizo, lakini akisisitiza kila mmoja anapaswa kushinda mechi zake.
Azam FC ipo nafasi ya tatu kwenye msimamo ikiwa imejikusanyia pointi 48 ikiiacha pointi nne Singida Black Stars iliyopo katika nafasi ya nne baada ya kukusanya pointi 44, huku Tabora United ipo nafasi ya tano ikiwa na pointi 37.
Akizungumza na Mwanaspoti, Ouma alisema mechi zilizobaki ndizo zitaamua timu ipi itamaliza nafasi ya tatu, hivyo kila moja ishinde mechi zake ili kufikia malengo. Kocha huyo alisema kuwa wachezaji wake wapo tayari kwa mapambano ya dakika 180 dhidi ya wapinzani wao Azam FC na Tabora United ambazo zitaamua nani apande nafasi moja na mwingine ashuke.
“Kufungwa na Azam FC mzunguko wa kwanza hatuwezi kurudia makosa kutokana na vita iliyo mbele yetu. Tunapambana kuhakikisha na sisi tunapata matokeo mchezo ujao ili kujiweka kwenye mazingira mazuri, lakini pia kupunguza presha ya kufukuzana na aliye chini yetu ambaye pia tutakuwa na mchezo naye nyumbani kwake tuliambulia sare ya mabao 2-2 tunahitaji pointi tatu nyumbani,” alisema.
“Tupo nyuma kwa pointi nne dhidi ya Azam FC ambaye yupo juu yetu kwenye msimamo tunaamini tukipata pointi tatu dhidi yao tutakuwa na gepu la pointi moja ambayo tutaipata kwenye mechi nyingine sita, wenzetu wakishinda na sisi tukapoteza tutaendelea kuongeza mlima mrefu kitu ambacho hatupo tayari kukifanya.”
Kocha huyo alisema mechi saba walizobakiza zote zina umuhimu wa kupata pointi tatu muhimu, lakini sio kazi rahisi bila ya mbinu na mipango imara kuhakikisha wanafanikiwa, lakini itakuwa kazi ngumu kwa kuwa pia timu wanazokutana nazo pia zinahitaji matokeo mazuri.
“Tuna mchezo na Tabora United inahitaji pointi kujihakikishia nafasi ya nne. Tuna Simba ambaye anapambana kusaka taji alilolipoteza misimu mitatu mfululizo, lakini pia tuna mchezo na Prisons ambayo ipo nafasi mbaya kwenye msimamo inapambana kusaka nafasi ya kubaki msimu ujao, hivyo haitakuwa rahisi kwetu.”
Akizungumzia mchezo wao unaofuata baada ya ligi kurejea, alisema ni mgumu ugenini, lakini wanaamini wamejiandaa vyema na wapo tayari kuhakikisha wanakusanya pointi zote tatu na kujihakikishia nafasi waliyopo sasa ikiwa ni pamoja na kupunguza pengo na mshindani wao, Azam FC.