Tutawa-miss Simba & Yanga

NI mara chache sana Simba na Yanga kucheza kati yao na wachezaji kupona katika tuhuma za kuuza au kununua mechi.
Nyota kadhaa wametoweka katika medani ya soka kwa kashfa za kuuza mechi ambaoz wakati mwingine huwa ni tuhuma tu ambazo hazina ushahidi.
Hadi leo wapo wachezaji wanaopata machungu kutokana na kupewa kashfa za kuuza au kucheza chini ya kiwango katika mechi hizi za Watani wa Jadi, hakuna timu inayokubali kirahisi kwamba wamefungwa uwanjani.
Simba na Yanga zinacheza leo Jumamosi katika Uwanja wa Taifa, katika mechi ya kulinda heshima kwa watani hao wa jadi, kwani kwao hakuna lolote litakalobadilika katika msimamo wa ligi ambayo tayari bingwa ameshapatikana ambaye ni Azam FC.
Yanga ipo nafasi ya pili kwenye msimamo huo ikiwa na pointi 55 wakati Simba ni ya nne na pointi 37 huku Mbeya City ikiwa nafasi ya tatu na pointi 46. Hivyo Yanga akimfunga Simba hawezi kusogea na hata Simba ikiifunga Yanga, haiwezi kwenda popote.
Mechi ya leo kwa watani hao, kuna nyota saba ambao walikuwepo mchezo uliopita wa Nani Mtani Jembe ambao uliishuhudia Simba ikipata ushindi wa mabao 3-1, lakini hawatacheza mechi ya leo kutokana na sababu mbalimbali.
Ni mechi ambayo wachezaji wanatakiwa kuwa makini ili kuepukana na lawama za kuuza mechi zinazopelekea baadhi yao kusimamishwa hasa kipindi hiki wanachoelekea kwenye usajili kwani endapo matokeo yatakuwa mabaya kwa upande mmoja wa timu kunaweza kuchangia wachezaji wengine wakatemwa kwenye usajili wakituhumiwa kuhujumu timu zao.
Hapa chini ni wachezaji ambao hawatakuwepo katika vikosi vya leo;
Juma Kaseja (Yanga)
Amesajiliwa na Yanga katika mzunguko wa pili wa ligi hii, mchezo wake wa kwanza ulikuwa dhidi ya Simba Desemba 22 mwaka jana mechi ya Nani Mtani Jembe, hatakuwepo leo, juzi Alhamisi alikuwa akijifua na timu ya vijana na U-20 ‘Ngorongoro Herous’.
Hata hivyo, imeelezwa kuwa bado hana mvuto kwa mashabiki wengi wa timu hiyo ambao wamekuwa wakidai anafungwa mabao ya kizembe huku wengine wakisema kuna fitna anafanyiwa mkongwe huyo. Uwezekano wa yeye kukaa golini leo ni mdogo mno na kwa wanaojiamini wanasema kabisa hana nafasi. Hakuna ubishi kwamba, kipa Deo Munishi ‘Dida’ ndiye atakayekaa golini ‘
David Luhende (Yanga)
Kumbuka penalti aliyoisababisha katika mechi ya Nani Mtani Jembe kwa kumkwatua Ramadhan Singano ‘Messi’? Tangu hapo amekuwa akisotea benchi akionekana hafai kwa kosa hilo lililoifanya Yanga kufungwa siku hiyo jambo ambalo limempa fursa Oscar Joshua kupata ulaji kirahisi kikosi cha kwanza.
Athuman Idd ‘Chuji’( Yanga)
Mkongwe huyu ambaye anasifika kwa pasi ndefu, hataweza hata kuonekana jukwaani leo, kama unabisha mtafute, amekuwa akipoteza mvuto tangu ilipomalizika mechi ya mwisho ya timu hizi lakini mbaya zaidi mara baada ya mchezo huo alikumbana na kifungo cha muda kutokana na tuhuma mbalimbali ikiwemo kuondoka moja kwa moja baada ya kutolewa mchezo ukiendelea.
Emmanuel Okwi (Yanga)
Alikuwa na sababu kubwa ya mashabiki wa Yanga kuibuka kwa wingi katika mchezo wa Nani Mtani Jembe ili waweze kuona vitu vya straika mpya, Emmanuel Okwi. Hata hivyo mchezaji huo alijitahidi kucheza katika kiwango chake lakini mambo hayakwenda sawa.
Okwi hayupo katika kikosi cha leo kutokana na kuidai timu hiyo sehemu ya fedha zake za usajili baada ya awali kulipwa nusu yake.
Haruna Niyonzima (Yanga)
Alikuwa katika mechi hiyo ambayo ilimalizika kwa Yanga kulala kwa mabao 3-1, leo hatakuwepo kikosini labda baadaye kuwapa pole wenzake vyumbani, amekosekana katika mechi nne zilizopita kutokana na kuugua na hata alipopona kocha wake Pluijm amemwambia apumzike kutokana na kazi nzuri ya Hassan Dilunga anayoifanya mpaka sasa.
Abdulhalim Humud (Simba)
Alikuwepo uwanjani siku ya mechi hiyo ya Nani Mtani Jembe, leo hatakuwepo kabisa na anaweza kuwa jukwaani akiwashuhudia wenzake wakicheza, katika orodha ya wachezaji 19 walioingia kambini kwa maandalizi ya mechi ya leo hakuwemo na yupo kwake na familia yake sababu ikitajwa kuwa kiwango kimeanza kushuka.
Haruna Shamte (Simba)
Alikuwa beki wa kulia katika mchezo wa mwisho baina ya timu hizi, alicheza vizuri siku hiyo tofauti na ilivyokuwa ikifikiriwa, leo hatakuwepo na kama atakuwepo atakuwa jukwaani kutokana na kwanza inaelezwa alikuwa majeruhi ingawa ameonekana akiwa viwanja vya Sigara akijifua binafsi.