VIWANGO: Ni majina tu ndio yatawabeba mastaa hawa kwenye klabu zao

Lionel Messi.
Muktasari:
- Kama inavyotarajiwa, mamilioni ya pesa yatatumika katika kutengeneza vikosi ambavyo vitakuwa na nguvu kubwa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kutakuwa na pilikapilika nyingi kwenye kipindi hicho cha usajili.
LONDON, ENGLAND
UMEFIKA wakati wa klabu za Ulaya kupigana vikumbo kwenye kusaka nyota wapya kwa ajili ya kuboresha vikosi vyao kabla ya msimu mpya kuanza.
Kwenye mchakato huo wa kusaka nyota wapya, katika klabu hizo lazima kutakuwapo na nyota watakaofunguliwa milango ya kutoka kwenye klabu hizo.
Kama inavyotarajiwa, mamilioni ya pesa yatatumika katika kutengeneza vikosi ambavyo vitakuwa na nguvu kubwa kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya. Kutakuwa na pilikapilika nyingi kwenye kipindi hicho cha usajili.
Hata hivyo, kwenye mchakato huo kuna baadhi ya mastaa wenye majina makubwa kwenye Ligi Kuu England watajiona kuwa wenye furaha kwa kubaki kwenye klabu zao wanazochezea kwa sasa utakapofika msimu ujao.
Wakati kikiwa kimefika kipindi cha klabu moja moja kujitathmini na kujijenga upya, kuna wachezaji wachache watabaki kwenye timu zao kwa sababu tu ya majina yao.
Eden Hazard
Si jambo jepesi kulumbana na Jose Mourinho kama mchezaji huyo na kitu ambacho kimefanywa na Eden Hazard kinaweza kuwa mwanzo wa klabu ya Chelsea kufeli kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Staa huyo wa Ubelgiji alifanya kosa kubwa kwa kukosoa mfumo wa timu yake ya Chelsea ambao ndiyo umeifanya timu hiyo ifikie mahali hapo ilipo. Hazard amemkosea adabu kocha wake na alistahili kuadhibiwa.
Juan Mata anaweza kuwa shahidi mzuri kuwa Mourinho si kocha mwoga wa kuwatupa kando wachezaji wake mastaa na jambo hilo linaweza kumgharimu sana Hazard. Kwa sasa kumekuwa na ripoti kwamba Chelsea inaweza kufikiria kumuuza mmoja kati ya mastaa wawili, Oscar na Hazard.
Kwa kile kilichotokea kwa sasa ni hadhi tu na jina ndicho kitu kinachombakiza Hazard klabuni Chelsea kwa msimu ujao.
Karim Benzema
Kwa njia zipi Karim Benzema ataendelea kubaki kwenye kikosi bora kabisa cha Real Madrid. Kucheza straika wa kati mbele ya mastaa kama Gareth Bale, Cristiano Ronaldo, Luka Modric, Isco, Xabio Alonso, Angel Di Maria na wengineo ungemtarajia Benzema awe tishio zaidi kwenye kufunga.
Lakini, staa huyo wa Ufaransa ameshindwa kulifanya hilo na sasa Real Madrid inafikiria mpango wa kumnasa Luis Suarez wa Liverpool. Benzema ni straika mzuri, lakini tatizo lake amekuwa hana makali ya kutisha zinapokuwa mechi kubwa. Benzema ni mara moja tu aliweza kupitisha idadi ya mabao 20 kwenye Ligi Kuu Hispania na hali ilivyo kwa sasa ni jina tu linakalomsaidia abaki klabuni hapo msimu ujao.
Shinji Kagawa
Bado hajaonyesha kiwango chake kilichotarajiwa na wengi ambacho kiliishawishi Manchester United kutoa pesa kumsajili. Kiungo huyo Mjapani, Shinji Kagawa, alishindwa kung’ara tangu timu hiyo ilipokuwa chini ya kocha Alex Ferguson na hadi ilipokuwa na kocha David Moyes.
Pengine kocha mpya atakayekuja klabuni hapo anaweza kuwa na bahati na staa huyo na akapata muda wa kuonyesha makali yake kama alivyokuwa kwenye kikosi cha Borussia Dortmund.
Franck Ribery
Kiti kimekuwa moto Allianz Arena kwa Pep Guardiola baada ya kikosi cha Bayern Munich kukung’utwa na Real Madrid kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, lakini wachezaji wake mastaa wanastahili kubeba lawama kwa matokeo hayo.
Winga Mfaransa Franck Ribery ni mmoja kati ya mastaa waliomwangusha Guardiola. Ribery alikuwa na nafasi ya kumwenyesha Cristiano Ronaldo kwamba ni yeye aliyestahili tuzo ya Ballon d’Or, lakini matokeo yake alifunikwa vibaya na hakuonekana kuwa na kitu chochote cha kufanya uwanjani.
Guardiola anaweza kufikiria kumpiga bei tu winga huyo na pesa atakazopata akanunua wachezaji wengine ambao watakuwa na jipya la kuifanyia timu. Ribery hana jipya analoweza kufanya Bayern kwa sasa na kama ataendelea kubaki klabuni hapo hadi msimu ujao hilo litatokana na jina lake tu.
Diego Costa
Kuna mtu mmoja alieleza kwanini Diego Costa, ameweza kufunga zaidi ya mabao 10 katika msimu huu na kuwa mmoja wa mastraika wanaowindwa duniani kwa sasa.
Chelsea inaonekana kushinda mbio za kumnasa staa huyo mwenye umri wa miaka 25 anayekipiga kwenye kikosi cha Atletico Madrid na kwamba klabu yake inasubiri kwa hamu sana pesa zitakazoletwa kwa ajili ya mchezaji huyo.
Kwa ada ya zaidi ya Pauni 30 milioni ambazo zitawagharimu watakaohitaji huduma ya mchezaji huyo, kocha Diego Simeone atakuwa mwenye kukenua kwa bahati ya mchezaji huyo.
Ukweli Costa hana muda mwingi wa kuendelea kutamba na staa huyo mzaliwa wa Brazil aliyechukua uraia wa Hispania ni aina ya mchezaji wa msimu mmoja. Ametengeneza jina msimu huu na kupandisha thamani yake, lakini zaidi ya hilo Costa atabebwa na jina lake.
Mesut Ozil
Mesut Ozil ni mfano mzuri wa wachezaji ambao wamekuwa wakizidiwa na ada zao za uhamisho. Staa huyo aliyesainishwa kwa pesa nyingi na Arsenal amekuwa na msimu mbaya, lakini watu bado wanaitaka Arsenal izidi kusajili kwa pesa nyingi kitu ambacho kimekuwa nadra sana kufanywa na klabu hiyo Ozil kwa kesi yake kwa sasa ni kwamba jina lake ndilo linalombeba lakini si soka analocheza. Ni kitu kinachoeleweka wazi, kama Ozil huyo sasa angeendelea kubaki Real Madrid isingekuwa rahisi kwake kupata namba kwenye kikosi hicho. Pengine hata kwenye kikosi cha Arsenal, anapangwa kutokana na jina lake au hadhi yake kwamba alisajiliwa kwa pesa nyingi.
Robin van Persie
Straika Robin van Persie amekuwa kwenye wakati mgumu msimu huu ambapo ameshindwa kufunga mabao na hata hali yake ya kiafya nayo imekuwa utata mtupu. Ukweli ni kwamba hiki kilikuwa kipindi mwafaka kwa Man United kupeana mkono wa kwaheri na staa huyo.
Ana umri wa miaka 30 na anasumbuliwa na tatizo la kuwa majeruhi mfululizo, jambo hilo litamfanya staa huyo kuwa si mchezaji muhimu kwenye kikosi hicho kwa msimu ujao zaidi ya kuwaongezea bili kwenye mishahara tu.
Wakati klabu hiyo ikipanga kufanya mabadiliko, Van Persie haonekani kuwa sehemu ya mipango hiyo na kwamba kitakachomfanya aendelee kubaki Old Trafford msimu ujao ni jina lake na uswahiba na kocha Louis van Gaal kama atakabidhiwa kuinoa timu hiyo.
Juan Mata
Kocha, David Moyes, amebeba lawama kwamba hakustahili kutumia pesa nyingi kwenye kuinasa saini ya Juan Mata. Mengi yanasemwa kwamba Man United imesajili mchezaji aliyekuwa akisugua benchi Chelsea na tangu atue kwenye klabu hiyo amekuwa tofauti.
Mata amefunga mabao matano tangu atue Man United Januari mwaka huu, lakini wachambuzi wa soka wanaamini usajili huo ulifanywa kwa kuhamaki baada ya mambo kwenda kombo.
Kitu ambacho Man United itakitaka kwa sasa ni wachezaji wanaotumia nguvu na kasi ya kuwarudisha katika hadhi yao, lakini Mata si mchezaji wa aina hiyo.
Lionel Messi
Staa wa Barcelona, Lionel Messi ni mwanasoka mahiri kwenye sayari hii, lakini msimu huu kiwango chake kimeshuka. Japo kwamba si kitu kinachopaswa kufanywa kwa haraka katika kumkosoa staa huyo, lakini dalili zimeonekana kwamba mchezaji huyo ameanza kupungua kasi yake ya awali hasa kutokana na sasa kusumbuliwa na hali ya kuwa majeruhi mara kwa mara.
Klabu yake ya Barcelona kwa sasa inamtazama Mbrazili Neymar kama mtu atakayeweza kuipandisha tena timu hiyo na si Messi. Kwa Messi, Barcelona sasa si mahali ambapo ataweza kucheza kwa ubora wake wa zamani.
Mabadiliko kitakuwa kitu muhimu sana kwa staa huyo mshindi mara nne wa tuzo ya Ballon d’Or. Lakini, Barca watabaki naye kisa jina na umaarufu wake.