Wahispania na ukocha wa soka England

VICENT DEL; Kuzaliwa: Desenba 23, 1950,Mahali: Salamanca, Hispania Urefu: 1.84 m Nafasi: Kocha Taifa: Hispania
Muktasari:
- Ukweli ni kwamba, Wahispania wamekuwa na vipaji vingi katika kiungo, mabeki na washambuliaji. Wamedhihirisha hilo kwao na hapa England pia.
KWA miaka mingi haikuwa rahisi kuwashawishi mashabiki wa soka wa England kwamba Hispania ni wachezaji mahiri wa soka.
Ukweli ni kwamba, Wahispania wamekuwa na vipaji vingi katika kiungo, mabeki na washambuliaji. Wamedhihirisha hilo kwao na hapa England pia.
Baada ya wachezaji wengi wenye asili ya Afrika kupanda chati na kupendwa hapa, ni kana kwamba Hispania imefungua mipaka na wachezaji wake wanatoka na kuwika kwenye nchi nyingine.
Hata hivyo, mada yangu inahusu makocha. Jamaa mmoja alipata kudai kwamba makocha wa Hispania hawawezi kufungisha soka hapan England.
Hispania ambayo ni bingwa wa dunia, timu zake nyingi za ngazi za juu katika soka kwao zinafundishwa na wazawa.
Lakini taratibu mambo yanabadilika na ‘uchawi’ wao umekuwa wazi, Hispania ikileta mapinduzi katika karne hii ya 21.
Vincente Del Bosque ni Mhispania anayeifundisha timu yao ya taifa kwa mafanikio makubwa na wapo wenzake wanaoonesha nguvu, kiwango, kujiamini na kujituma.
Wigan Athletic iliposhuka daraja msimu uliopita na Roberto Martinez akahamia Everton kuchukua nafasi ya David Moyes, baadhi ya mashabiki wa Everton walisikitika wakiona wamechukua garasa.
Lakini sasa amewaongoza vyema mno ‘Toffees’ na walikuwa wakishikilia rekodi ya timu kutofungwa msimu huu mpaka
walipovunjiwa mwiko huo karibuni.
Licha ya Martinez, kuna Wahispania wa kuasili (adopt) hapa kwenye Ligi Kuu England. Hao ni pamoja na Mauricio Pochettino wa Southampton na Michael Laudrup wa Swansea City.
Kocha mwingine aliyepikwa Hispania ni Oscar Garcia ambaye yupo klabu ya Brighton.
Hata hivyo hali hii inaelekea kubadilika kwani kuna ‘kelele’ zinapigwa kutoka klabu yenye historia kubwa ya Middlesbrough na Crystal Palace.
Nimeambiwa kwamba klabu hizo zinamsaka aliyekuwa beki wa kati wa Bilbao, Aitor Karanka, kwa ajili ya kuongoza moja ya klabu hizo zinazosuasua.
Palace inakokota mkia kwenye Ligi Kuu England wakati huu ambapo imeshavuka robo msimu.
Karanka alikuwa msaidizi wa Jose Mourinho pale Real Madrid na wakati wowote anaweza kukalia kitimoto nchini hapa kutoa mwongozo wake kisoka.
Mtu aliyempika, Mourinho, ambaye sasa ni kocha wa Chelsea, ana kawaida ya kuwaungisha wasaidizi wake wa zamani kwenye klabu za hapa, amefanya hivyo kwa Pochettino na pia Brendan Rodgers.
Inasemekana kwamba Karanka anavutiwa zaidi na kujiunga Middlesbrough. Lakini kana kwamba haya ya England hayatoshi, Scotland nao wanaonekana kuanza kuvutiwa na Wahispania.
Inajulikana kwamba klabu za huko hazina bajeti nzito ya kuweza kuajiri makocha wenye majina makubwa.
Ni kwa mara ya kwanza katika historia, klabu za Scotland zimeanza mazungumzo na makocha wa Hispania, wakitaka Wahispania wabunifu na wenye mawazo mapya ya kujenga kivingine mfumo wa soka lao.
Majuzi niliambiwa palikuwa na kuhusishwa kwa Antonio Tapia na klabu za Hibernian wakati Albert Ferrer amekuwa na mazungumzo na klabu ya Kilmarnock.
Kadhalika, Pako Ayestaran aliyekuwa namba mbili kwa kocha, Rafael Benitez na Sanchez ‘Quique’ Flores, nusura ajiunge na Kilmarnock. Benitez alitamba England kwa kuifundisha Liverpool kwa mafanikio makubwa kabla ya kuondoka kisha akarejea kuwa kocha wa muda Chelsea na sasa anaiongoza Napoli ya Italia.
Hata hivyo, ofa ya mwisho iliyokuwa mezani ilikataliwa na sasa ni kocha wa Estudiante Tecos ya Mexico lakini bado mlango haujafungwa kwake kurudi England.
Zaidi ya hapo, Gerard Nus, ambaye kwa sasa ni Meneja Msaidizi wa Melbourne Heart, anatajwatajwa kutaka kujiunga na Partick Thistle.